Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba
WATU wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wamevamia nyumbani kwa Naibu
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba kwa lengo
la kufanya uhalifu.
Hata hivyo majambazi hao ambao walimfunga kamba mlinzi wa nyumba hiyo na kuingia ndani, hawakufanikiwa kuiba chochote.
Naibu Waziri Makamba aliliambia gazeti hili kuwa
tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana wakati yeye akiwa safarini
jimboni kwake Bumbuli ila familia yake ilikuwapo nyumbani hapo.
Makamba alisema baada ya majambazi hao kuingia ndani, walimfunga kamba na kumziba mdomo mlinzi.
“Ujambazi huo ulitaka kufanyika nyumbani kwangu
Masaki karibu na Ubalozi wa Afrika Kusini. Mimi sikuwepo nyumbani.
Walivamia chumbani mke wangu akabonyeza kengele iliyopiga kelele ndio
wakakimbia, baada ya majirani kuwasili eneo la tukio, wakatokomea
kusikojulikana,” alisema Makamba na kuongeza:
“Waliingia kwenye ofisi yangu ya pale nyumbani na
kupekua. Lakini cha ajabu ni kwamba sebuleni kulikuwa na Ipad na laptop
(kidadavuzi mpakato) lakini hawakuvichukua.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles
Kenyella alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba watu hao
walitaka kufanya ujambazi, lakini hawakufanikiwa.
Kamanda Kenyella alisema tukio hilo lilitokea saa
10 alfajiri ya kuamkia jana, lakini majambazi hao hawakufanikiwa
kutimiza azima yao.
“Walimfunga kamba mlinzi na kufungua dirisha,
kisha kuingia ndani. Lakini hawakufanikiwa kuchukua chochote,” alisema
Kamanda Kenyella.
Kamanda Kenyella alieleza kuwa majambazi hao
hawakufanikiwa kuiba chochote kwa kuwa wakazi wa eneo hilo, walisikia
purukushani na kupiga kelele zilizosababisha watu hao kutokomea.
“Haijulikani walikuwa wangapi kwa kuwa hakuna mtu
yeyote aliyewaona, lakini katika tukio hilo hakuna aliyejeruhiwa,”
alisema Kamanda Kenyella.
Alisema baada ya tukio hilo Jeshi la Polisi
Kinondoni, inaendesha msako wa kuwatafuta watu hao ili kuweza kuwatia
nguvuni na kuwafikisha mahakamani.“Tuna msako mkali na ninaapa kwamba lazima tutawakamata popote walipo na tutawashughulikia ipasavyo,”alisema Kenyella.
MWANANCHI
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment