MZOZO wa nani achinje nyama kati ya Waislamu na Wakristo
haujapata ufumbuzi baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kusema mazoea ya
tangu zama za kale yanayowaruhusu Waislamu kuchinja, yaendelee hadi hapo
uamuzi mwingine utakapofikiwa na serikali.
Hata hivyo, Pinda ameagiza kuundwa kamati maalumu itakayohusisha pande
zote mbili za Waislamu na Wakristo, ambayo itashughulikia mgogoro huo,
na kwamba kazi hiyo ifanyike haraka iwezekanavyo na kisha ripoti yake
iwasilishwe serikalini kwa hatua zaidi za kimaamuzi.
Waziri Pinda alisema hayo jana alipokuwa akitoa ufafanuzi kwa
waandishi wa habari, kuhusiana na kikao chake cha pamoja na viongozi wa
Kikristo na Kiislamu, kilichofanyika katika Ukumbi wa Benki Kuu ya
Tanzania (BoT), tawi la Mwanza, kwa lengo la kutatua mgogoro huo.
Alisema kutokana na hali ilivyo sasa, serikali imeagiza kuundwa kamati
hiyo kisha kupewa adidu rejea kwa ajili ya kushughulikia mgogoro huo wa
kidini, na kwamba kabla na wakati kamati hiyo ambayo hakusema itatumia
muda gani katika kazi zake, suala la kuchinja litaendelea kubaki kwa
Waislamu, kwani ndiyo mazoea ya toka zama za kale.
"Kikao changu na viongozi wetu wa kiroho kilikuwa na mvutano mkali
sana. Wakristo wanasema hivi, Waislamu nao wanasema hivi. Lakini
nimeagiza uongozi wa Mkoa wa Mwanza uunde kamati maalumu
itakayoshughulikia tatizo hili.
"Hili suala la uchinjaji halipo kisheria. Hakuna sheria inayosema
Waislamu pekee ndiyo wachinje, isipokuwa tumeishi kwenye mazoea hayo
tangu enzi za kale. Sasa, wakati kamati hii ikiendelea kufanya kazi
zake, suala la kuchinja liendelee kufanywa na Waislamu maana ndiyo
mazoea na desturi zetu hadi hapo maamuzi mengine yatakapotolewa,"
alisema Pinda.
Alisema kamwe serikali haitakubali kuona Wakristo na Waislamu
wanakuwa na mabucha yao, na kwamba iwapo suala hilo litaruhusiwa,
litaleta athari na ubaguzi mkubwa wa kidini, kwani hata bungeni, kwenye
usafiri na maeneo mengine wafuasi wa dini hizo watakuwa wanajitenga na
wafuasi wa dini nyingine jambo ambalo halikubaliki hata kidogo.
Kauli hiyo ya Waziri Mkuu Pinda, imekuja siku chache baada ya kutokea
mapigano makali baina ya wafuasi wa dini ya Kiislamu na Kikristo kuzuka
huko Buseresere-Katoro katika Wilaya ya Chato mkoani Geita, ambapo
mchungaji mmoja aliuawa kwa kuchinjwa huku watu wengine kadhaa
wakijeruhiwa vibaya.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Pinda haitofautiani na iliyowahi kutolewa na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira
alipokutana na viongozi wa dini wa pande zote katika ukumbi wa jiji la
Mwanza hivi karibuni kabla ya kutokea umwagaji damu kule
Buseresere-Katoro mkoani Geita.
Alipoulizwa na mwandishi wa habari hizi sababu za serikali kuamua
kuunda kamati kwa ajili ya kutatua mgogoro huo badala ya kutoa uamuzi
ulioathiri pande zote, Pinda alisema: "Unataka serikali ifanyeje, na
itatueje kwa haraka suala hili?"
Aidha, Waziri Mkuu Pinda alikemea vikali vurugu za kidini zilizotokea
mkoani Geita, na kuwataka viongozi wa madhehebu yote ya dini
kuheshimiana, kujenga mshikamano na kutohasimiana, kwani wao ni watu
muhimu sana katika maendeleo na utulivu wa nchi.
Alisema umwagaji damu uliotokea Buseresere ni kitendo kibaya sana
katika taswira ya taifa la Tanzania ambayo ni kisima cha amani, upendo
na utulivu, na aliwaagiza wakuu wote wa mikoa nchini kuhakikisha
wanakutana mara kwa mara na viongozi wote wa dini, ili kujenga na
kuimarisha mahusiano mazuri baina ya pande zote.
"Kwanza nawapeni pole sana viongozi wote wa dini kutokana na matukio
yaliyotokea kule Buseresere-Katoro na Nyehunge Sengerema. Naamini kabisa
hakuna kiongozi wa kidini aliyependa itokee umwagaji damu kama
ilivyotokea.
"Lakini, nawaombeni sana viongozi wangu wa kiroho, jengeni mshikamano,
na kila mmoja aheshimu dini ya mwenzake. Nchi yetu bado ina sifa nzuri
ya kuwa na amani, upendo na utulivu...na serikali hatutaki kuona dini
zinahasimiana," alisema Pinda.
No comments:
Post a Comment