Mbunge wa Jimbo la Monduli, Edward Lowassa
Dar es Salaam. Ofisi ya Bunge jana ilitangaza majina ya wenyeviti na makamu wapya wa Kamati za Kudumu za Bunge huku Mbunge wa Jimbo la Monduli, Edward Lowassa akichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Kuchaguliwa kwa Lowassa kuongoza kamati hiyo
kunaibua upya vita kati yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe, kutokana na wote kutajwa kutaka kugombea
urais katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015.
Awali, Lowassa alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya
Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, ambayo iligawanywa hivi karibuni na
kuzaliwa kamati mbili; ya Ulinzi na Usalama na Kamati ya Mambo ya Nje.
Kushinda kwa Lowassa kunakuja siku moja, baada ya
wabunge wote wa CCM kukutana katika kikao cha ndani kilichofanyika
Ukumbi wa Karimjee na kujadili masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na
jinsi ya kuwachagua wenyeviti na makamu wa kamati hizo.
Habari za ndani kutoka katika kikao hicho
zilieleza kuwa moja ya ajenda zilizozungumzwa ni kuwataka wabunge
kuwachagua wenyeviti kwa kufuata taratibu na utendaji wao wa kazi.
Hata hivyo, Naibu Spika Job Ndugai aliliambia
Mwananchi Jumamosi kwamba kikao hicho ni cha kawaida na walikuwa
wakijadiliana matatizo yaliyopo katika majimbo yao na jinsi ya
kuyawasilisha serikalini.
Katika uchaguzi huo, Musa Azzan Zungu ambaye
alikuwa makamu wa Lowassa kabla ya kugawanya kwa kamati hiyo,
amechaguliwa tena kushika nafasi hiyo.
Uchaguzi wa wenyeviti na makamu wao ulifanyika
jana katika Ofisi Ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam, ikiwa ni siku
moja baada ya ofisi ya Bunge kutaja majina ya kamati mpya 16 pamoja na
wajumbe wake.
Uchaguzi huo umefanyika ukiwa umepita mwezi mmoja
tangu kumalizika kwa mkutano wa 10 wa Bunge ambapo, Spika wa Bunge, Anne
Makinda alitangaza mabadiliko ya kamati hizo, huku akiifuta Kamati ya
Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa
Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
Kutokana na mabadiliko hayo, shughuli za POAC sasa zitafanywa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC).
Kamati nyingine iliyofutwa ni ile ya Sheria Ndogo
wakati zimeundwa kamati mpya za Bajeti, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa na ya Ulinzi na Usalama.
Taarifa za ndani kutoka katika chaguzi hizo
zinaeleza kuwa Zitto ambaye alikuwa akichuana na John Cheyo, alipata
kura 13 kati ya 17 zilizopigwa na wajumbe wa kamati yake, hivyo Zitto
sasa ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC).
Mbunge wa Ludewa, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa POAC, Deo Filikunjombe, amechaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa PAC.
Kushindwa kwa Cheyo kulianza kuonekana mapema
kutokana na Zitto, ambaye alilalamikia kitendo cha kuvunjwa kwa kamati
ya POAC, kuanza kampeni za chinichini ili kumtoa Cheyo, ambaye
ameshikilia nafasi ya uenyekiti wa PAC tangu mwaka 2005.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu
Katibu wa Bunge, John Joel aliwataja walioshinda kuwa ni Mohamed Mgimwa
ambaye amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi ambapo
makamu wake ni Luke Kitandula.
Alisema Kamati ya Bajeti, mwenyekiti wake
ameteuliwa na Spika Anne Makinda kuwa ni Andrew Chenge katika utaratibu
ambao haufanani na wa kamati nyingine.
Hata hivyo, alisema kwa upande wa makamu
mwenyekiti wa kamati hiyo atachaguliwa na wajumbe wa kamati kama ilivyo
kwa kamati nyingine.
“Kwa leo (jana) uchaguzi wa makamu mwenyekiti
umefanyika, lakini kura zikawa sawa hivyo makamu hakupatikana, hivyo
uamuzi umefikiwa kuwa uchaguzi huo utarudiwa Jumatatu ijayo,” alisema
Joel.
Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za
Mitaa (LAAC) amekuwa Rajab Mbarouk Mohammed na makamu wake ni Suleiman
Zedi,” alisema Joel.
Awali, mwenyekiti wa LAAC alikuwa mbunge wa Vunjo
(TLP), Augustino Mrema ambaye katika uteuzi mpya amekuwa Mjumbe wa
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
Kwa upande wa Kamati ya Ulinzi na Usalama,
aliyekuwa makamu wake, Iddi Azzan amebwagwa katika uchaguzi huo, sasa ni
mjumbe wa Kamati ya Masuala ya Ukimwi.
Joel alisema Margareth Sitta amekuwa Mwenyekiti wa
Kamati ya Huduma za Jamii na makamu wake ni Stephen Ngonyani.Wengine
waliochaguliwa ni Jenister Mhagama ambaye anakuwa Mwenyekiti Kamati ya
Maendeleo ya Jamii na makamu wake ni Saidi Mtanda.
Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini ni
Victor Mwambalasa na makamu wake ni Jerome Bwanausi. James Lembeli
amekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira na makamu
wake ni Abdulkarim Shah.
Peter Serukamba amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa
Kamati ya Miundombinu na makamu wake ni Profesa Juma Kapuya. Hamisi
Kigwangalla amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa na makamu wake ni John Lwanji.
Kamati ya Masuala ya Ukimwi mwenyekiti ni Lediana Mng’ong’o, makamu wake ni Diana Chilolo.
Anna Abdallah amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa
Kamati ya Ulinzi na Usalama na makamu wake ni Mohammed Seif
Khatib,.Pindi Chana amekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na
Utawala, makamu wake ni William Ngeleja.
Kamati ya Maadili mwenyekiti ni Brigedia mstaafu
Hassan Ngwilizi na makamu wake ni John Chiligati na Kamati ya Kilimo,
Mifugo na Maji mwenyekiti wake ni Profesa Peter Msolwa na makamu wake ni
Said Nkumba.
MWANANCHI
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment