HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» »Unlabelled » HOJA YA USHOGA BUNGENI



Mbunge wa Nyamagana(Chadema), ambaye ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Ezekia Wenje, akitolewa nje ya Ukumbi wa Bunge na askari wa Bunge huku akionyesha alama ya ‘V’, baada ya wabunge wa CUF kutaka kumpiga, kutokana na hotuba yake waliyodai kuwaudhi wabunge hao. Picha na Emmanuel Herman. 


Dodoma. Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai ameahirisha mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, baada ya msemaji wa kambi ya upinzani kwa wizara hiyo kukataa kuomba radhi kulingana na maagizo ya kiti cha Spika.
Ndugai alikuwa amemwamuru msemaji huyo wa Upinzani, Ezekiah Wenje aombe radhi kwa kile alichoeleza ni kukashifu chama cha CUF na afute maneno ya kashfa hizo kwenye hotuba yake.
Wenje alikubali kutosoma maneno hayo yaliyokuwa kwenye hotuba hiyo lakini akakataa kuomba radhi kwa maelezo kuwa yaliyoandikwa ni ya ukweli na ana ushahidi.
Awali wakati wa asubuhi pia Ndugai alilazimika kuahirisha kikao cha Bunge, baada ya kuzuka vurugu kubwa kati ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wananchi (CUF).
Vurugu hizo zilizuka baada ya Mbunge wa CUF (Mtambile) Masoud Salim, kutoa hoja ya kutaka Msemaji wa Kambi rasmi ya Upinzani bungeni katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Ezekiel Wenje, kusitisha hotuba yake kwa kile alichoeleza kuwa “imejaa uzushi, uhuni, uzandiki, uongo na ushenzi.”
Salim alitoa hoja hiyo saa 6:15 mchana, wakati Wenje akiwa anasoma hotuba hiyo katika ukurasa wa tatu.
“Mwongozo wa Spika,” alisema Salim muda mfupi kabla Naibu Spika Ndugai, hajampa fursa ya kutoa hoja yake.
Salim aliendelea: “Natoa hoja kwamba hotuba hii ni ya kizushi. Huu ni uhuni, uongo, ushenzi na uzandiki. Siyo ya kusomwa bungeni.”
Alitoa kauli hiyo akinukuu maneno yaliyoko kwenye ukurasa wa 8 wa kitabu cha hotuba hiyo yanayoeleza kuwa,”...Kwa upande wa CUF, kutokana na itikadi zake za mrengo wa kiliberali ambazo miongoni mwa misingi yake mikuu ni pamoja na kupigania haki za ndoa ya jinsia moja, usagaji na ushoga…’
Kipengele kilichowaudhi CUF kilisema hivi: “Hii ni kwa mujibu wa tangazo lao (CUF) kwenye mtandao wao wa umoja wa maliberali ulimwenguni, likiungwa mkono na Waziri wa Haki na Usawa wa Uingereza, Lynn Featherstone kutoka chama cha Liberal Democrats wakati chama hicho kilipokuwa kinapitisha azimio la kuruhusu ndoa za jinsia moja kama haki ya mtu mmoja mmoja.
Salim alikiomba kiti cha Spika, kuamrisha Chadema waombe radhi, wafute kauli hiyo na Kamati ya Maadili iifanyie kazi taarifa yao kwa kuwa si ya kistaarabu.
“Kwanza wakome, wakome kwa asilimia 100. Wahuni hawa na tunataka wachukuliwe hatua za kinidhamu,” alisema Salim, huku akishangiliwa na Mbunge wa Nkasi (CCM), Ali Kessy ambaye aliibuka kitini na kuitikia,” Apigwe, apigwe, Msagaji mwenyewe (Wenje).”
Baadaye Ndugai alimuuliza Wenje kama ana ufafanuzi wowote wa hoja za wabunge hao.
Akizungumza kwa upole na nidhamu, Wenje alisema,” With due Respect (kwa heshima kubwa) ningeomba wabunge wenzangu wangenisikiliza kwanza.”
Aliendelea; “Hapa tumeeleza Chadema, CCM na CUF na uhusiano wao na mataifa ya nje. Ni ukweli kwamba CCM wako mrengo wa kushoto, Chadema mrengo wa kati na CUF mrengo wa kiliberali. Hii ni misingi ya idiolojia…”
Kabla hajaendelea, wabunge wote wa CUF walisimama na kushika kitabu cha hotuba hiyo juu, wakitaka kumfuata Wenje mbele alikokuwa amesimama kuisoma wakisema;
“Ondoa uchafu wako hapa, tena ukome, koma kabisa huna adabu, toka hapa. Wasagaji wenyewe.”
Vurugu hizo zilizoondoa kabisa utulivu bungeni, zilimfanya Naibu Spika Ndugai kuahirisha Bunge hadi jioni, huku akitaka Kamati ya Maadili kuketi kwa dharura kwa ajili ya kuipitia hotuba hiyo.

Zogo kikao cha jioni
Zogo hilo lilianza kwa Ndugai kutoa nafasi kwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Maadili ya Bunge, John Chiligati atoe maelezo ya usuluhishi.
Chiligati alisema kamati ilimwita Wenje lakini akajitetea kuwa kauli yao siyo ya kupakazia bali ni ya kweli na ushahidi wanao.
Pamoja na vielelezo kadhaa ambavyo Wenje alifikisha mbele ya kamati hiyo, Chiligati alisema waliona kuwa ipo haja ya msemaji huyo kusahihisha kifungu hicho.
Ndugai alitoa dakika tano kwa Wenje kutekeleza agizo hilo lakini yeye alitumia muda huo kujitetea.

Kutokana na mvutano huo, Ndugai alitoa nafasi kwa Mbunge wa CUF, Masoud Salim ambaye alisisitizia msimamo wa kamati ukaziwe na Mbunge wa Chadema, John Mnyika ambaye alikosoa mwenendo mzima wa kuamua juu ya mzozo huo.
Ndugai baada ya kuona hakuna mwafaka alisema analirudisha shauri hilo kwa Kamati ya Maadili na kuahirisha Bunge hadi leo ambapo watajadili makadirio ya matumizi na mapato kwa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
Kuhusu Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje, alisema ofisi ya Spika itaamua baada ya kupitia uamuzi mpya utakaotolewa na Kamati ya Maadili ya Bunge.
Nje ya ukumbi wa Bunge, wabunge wengi walikataa kuzungumzia suala hilo hasa wakitupia jukumu hilo kwa wabunge wa CUF na Chadema.
Hata hivyo, wabunge wa CUF waliozungumza na gazeti hili walisisitiza kuwa kauli ya msemaji huyo wa upinzani wanaichukulia ni mpango wa makusudi uliotengenezwa na Chadema kukichafua chama chao.
Mbunge wa CUF, Muhammad Ibrahimu Sanya alikiri kuwa wana uhusiano na mfumo huo wa kiliberali lakini kamwe hawaungi mkono ndoa za jinsia moja.
“Unaweza ukafuata mfumo fulani lakini siyo kila kitu. Mtu anaweza akakuona unazungumza na jirani yako ambaye ni jambazi lakini hapaswi kukuchukulia na wewe ni jambazi. Uhusiano wenu ni kuishi jirani,” alisema Sanya.
Gazeti hili lilipowasiliana na Mnyika (Chadema), alisema anaamini kabisa Spika na Kamati ya Maadili imepotoka kwa sababu alichosema Wenje ana ushahidi na upande wa pili umeshindwa kujinasua kwenye kitanzi hicho.
Alisema Ndugai amekiuka kabisa kanuni kwa sababu Kamati ya Maadili ya Bunge haina kabisa mamlaka au majukumu ya upatanishi.
Alisema kamati hiyo ina mamlaka ya kuchunguza na kutoa mapendekezo kwa Bunge ambalo ndilo lenye mamlaka ya uamuzi.
“Naibu Spika amepoteza muda bure na fedha za walipakodi badala ya kuachia ukweli usemwe. Kama kulikuwa na wenye maoni tofauti wangejibu wakati wanachangia kwenye mjadala,” alisema Mnyika.E & P


MWANANCHI

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: