JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII
UFAFANUZI WA TAARIFA MBALIMBALI
ZILIZOTOLEWA KWENYE VYOMBO VYA HABARI DHIDI YA DAWA BANDIA YA
KUPUNGUZA MAKALI YA UKIMWI YENYE JINA LA BIASHARA TT-VIR 30 TOLEO NAMBA
0C.01.85.
Tarehe 9 Mei, 2013, Mhe. Dkt. Hussein
A. Mwinyi (Mb) Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, katika kuhitimisha hoja ya bajeti
ya Wizara alitolea ufafanuzi suala la dawa bandia ya ARV kufuatia hoja
zilizokuwa zimetolewa na Mhe. Zarina S. Madabida (Mb) kuhusu kuhusika kwa
kiwanda cha dawa cha Tanzania
Pharmaceutical Industries Ltd (TPI) katika sakata la dawa bandia ya ARV.
Baada
ya ufafanuzi huo wa Mhe. Waziri kutolewa, kumekuwa na taarifa mbalimbali
kupitia vyombo vya habari zinazoleta mkanganyiko kwa wananchi kuhusu suala
hili.
Ili
kuondoa mkanganyiko ambao umeanza kujitokeza, Wizara inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu tamko lililotolewa na Mhe. Waziri wa
Afya na Ustawi wa Jamii. Aidha, kama
ilivyoelezwa katika taarifa mbalimbali za umma zilizokwisha kutolewa na Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na
TFDA kuhusiana na suala hili,
bado inasisitizwa kwamba kampuni ya TPI Ltd iliiuzia Bohari ya Dawa (MSD) dawa bandia aina ya TT-VIR 30
toleo Na. 0C.01.85, kwa mujibu wa nyaraka zilizopo.
Tunapenda
kusisitiza kwamba, Mhe. Waziri katika hotuba yake hakukanusha kuwa kampuni ya
TPI Ltd iliiuzia MSD dawa bandia bali alieleza kwamba uchunguzi wa awali katika
kiwanda cha kampuni hiyo haukuonesha dawa hiyo ilizalishwa na TPI Ltd bali vifungashio ni vya TPI Ltd na nyaraka
zinaonesha TPI Ltd kuiuzia MSD dawa hizo bandia. Aidha, alieleza kuwa vyombo
vya usalama bado vinaendelea kulichunguza suala hilo ili kubaini chanzo na
wahusika wakuu wa dawa hizo bandia.
Kwa kuzingatia unyeti wa suala hili, Wizara inatoa wito kwa vyombo vya
habari kusubiri hatma ya uchunguzi unaofanywa na vyombo vya usalama na kuepuka
kutoa taarifa ambazo zinaweza kupotosha umma na jitihada kubwa za Serikali
katika kupambana na dawa bandia nchini.
N. Mwamwaja
MSEMAJI
16 Mei, 2013.
No comments:
Post a Comment