HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» »Unlabelled » JWTZ WAITULIZA MTWARA


Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Devis Mwamunyange
*Wazunguka mitaani kwa amani kulinda usalama
*Watu 91 wamakatwa, msako mkali kila kona
*Mabasi yagomea Lindi,watoto wapoteana na wazazi
UWAMUZI wa Serikali kupeleka askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) mkoani Mtwara kwa ajili ya kuongeza nguvu ya kukabiliana na wimbi la vurugu, zimeanza kuzaa matunda. Matunda hayo yalianza kuonekana mapema jana askari hao walipoanza kupita katika mitaa mbalimbali ya mji wa Mtwara, ambao juzi uligeuka uwanja wa vita.
Katika vurugu za juzi, polisi walilazimika kutumia risasi za moto, mabomu ya machozi na maji ya kuwasha kukabiliana na wananchi ambao waliamua kujichukulia sheria mkononi kwa kufanya vurugu na kusababisha uharibifu mkubwa.
Lakini jana askari wa JWTZ, walionekana katika mitaa ya Mnarani, Shangani, Sokoni, eneo la Stendi Kuu ya Mabasi na Bima. Wakati wote ambao askari hao walipita katika maeneo hayo, walikuwa watulivu na hawakuchukua hatua zozote za kukamata mtu, jambo ambalo lilionekana kupokelewa kwa furaha na wananchi.
Mmoja wa wananchi wa eneo la Bima, Salimini Mohamed aliipongeza serikali kwa uamuzi wake wa kupeleka askari hao.

“Tumeona mabadiliko makubwa leo (jana), si kama jana (juzi) ambako polisi walitumia nguvu kukamata watu, tunaamini JWTZ ndiyo mkombozi wetu hapa.

“Nimeshuhudia kwa macho yangu mwenyewe namna ambavyo askari wamepita na kuwaambia wananchi watulie, tofauti na polisi ambao wanaendesha kamatakamata kali.

“Katika maeneo ya pembeni mwa mji, wanapita na kuwataka wananchi warudi kwenye makazi yao bila wasiwasi,”alisema Mohamed.

 VIFO
Idadi ya watu walipoteza maisha imeongezeka na kufikia wawili, baada ya mama mjamzito kudaiwa kupigwa risasi akiwa nyumbani kwake eneo la Magomeni.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Mohamedi Kodi alithibitisha kupokea mwili wa mjamzito ukiwa na tundu la risasi tumboni.

“Ni kweli kwa leo (jana), tumepokea maiti moja ya mwanamke ambaye ni mjamzito wa miezi saba, amepigwa risasi tumboni” alisema Kodi.

Alisema pia jana hiyo, walimpokea mwanafunzi wa shule ya sekondari Chuno ambaye alivunjwa miguu yote kwa risasi

MSAKO
Jana kutwa nzima, polisi wenye silaha walikuwa wakizungumza mitaa mbalimbali kuwasaka watu ambao wanaaminika kushirika vurugu hizo.

“Magomeni A, hatuna amani askari wanaingia majumbani mwetu wanatupiga na kutunyang’anya simu,tumepoteza watoto na hatujui hata waume zetu wako wapi,” alisema Paulina Idd.

 SERIKALI
Katika hatua nyingine, Spika wa Bunge, Anne Makinda kwa mara nyingine jana asubuhi, alilazimika kuahirisha Bunge hadi leo asubuhi litakapokutana tena kuendelea na shughuli zake.

Spika Makinda,aliahirisha Bunge ili Kamati ya Uongozi ya Bunge, ipate muda wa kutosha kujadili suala hilo. Kutokana na hali hiyo, alisema Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini iliondolewa katika orodha za shughuli za jana hadi itakapopangiwa ratiba nyingine.

Hiyo ni mara ya pili kwa Spika Makinda kuahirisha Bunge kutokana na machafuko ya Mtwara. Mara ya kwanza alifanya hivyo jusi baada ya Bunge kurejea katika kipindi cha jioni.

KAULI YA SERIKALI
Akitoa kauli ya Serikali bungeni jana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi alisema Serikali inasikitishwa na vurugu hizo na itahakikisha wahusika wanasakwa ndani na nje ya nchi.

Dk. Nchimbi alitoa kauli hiyo, baada ya Kaimu Mnadhimu wa Serikali, Dk. Mary Nagu kutengua kanuni ya 38 kutoa fursa kwa Waziri Mkuu kutoa kauli ya Serikali kuhusiana na vurugu hizo.

Dk. Nchimbi ambaye alikuwa akitoa kauli hiyo kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema dalili za kuibuka kwa vurugu zilionekana mapema baada ya kundi moja kusambaza vipeperushi.

“Walisambaza vipeperushi vyenye lengo la kuhimiza wakazi wa Mtwara, kuwa siku ya Ijumaa Mei 17, wasikilize hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini.

Akizungumzia madhara, Dk. Nchimbi alisema askari wanne wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), walifariki dunia katika ajali ya gari wakiwa njiani kuelekea Mtwara kuzima machafuko hayo.

“Waziri wa Ulinzi alikubali na kuelekeza Jeshi la Wananchi (JWTZ), waende mara moja. Katika kutekeleza agizo hilo, askari 32 wa jeshi hilo walianza safari kutoka Nachingwea kuelekea Mtwara.

“Walipofika njiani katika eneo la Kilima Hewa, gari lao lilipata ajali ambako askari wanne walifariki dunia na 20 walijeruhiwa.

“Askari hawa wamekufa na kujeruhiwa wakati wakiwa kazini kutekeleza wajibu wa kuwalinda Watanzania wenzao, damu yao haitamwagika bure,” alisema Dk. Nchimbi.

Mbali na askari hao, Dk. Nchimbi alisema mtu mmoja, Karim Shaibu, alifariki dunia katika vurugu hizo juzi, huku askari wawili wakijeruhiwa kwa bomu la kishindo.

Alisema katika vurugu hizo, ofisi ya Mbunge wa Mtwara Mjini, Hasnain Murji iliyopo Mikindani iliharibiwa na kuibwa vitu mbalimbali.

“Tunalo taifa moja la Tanzania ambalo maliasili zake ni za Watanzania wote, tabia inayoanza kujengeka ya kila eneo kutaka linufaike peke yake na rasilimali za eneo hilo, italigawa taifa letu vipande vipande. Hadi jana watu 91 walikuwa wamekamatwa.

 Kamati teule
Katika kutafuta kiini cha tatizo, Kamati Teule ya Bunge huenda ikaundwa muda wowote kuanzia sasa, iweze kufanya uchunguzi kubaini msingi wa mgogoro huo.

Habari za kuaminika zilizolifikia MTANZANIA kutoka ndani ya kikao cha Kamati ya Uongozi ya Bunge zilisema hatua hiyo inakuja kutokana na mapendekezo ya wajumbe.

Chanzo hicho kilisema wajumbe katika kikao hicho kilichokuwa kikiongozwa na Spika Makinda, walitoa pendekezo hilo lililoungwa mkono.

 Mabasi yagoma Lindi
Abiria wa mabasi wa kutoka Lindi kwenda mkoani Mtwara, jana walijikuta wakikwama baada ya madereva ya mabasi hayo kugoma kusafiri kwa hofu wa usalama wao.

Mkoa wa Lindi, husafirisha abiria zaidi ya 400 kwenda katika mikoa ya Mtwara na Dar es Salaam. Kutokana na hofu hiyo wamiliki wa mabasi na abiria walijikuta wakiwa na msimamo mmoja wa kutosafiri jana.

MTANZANIA ilifika katika kituo kikuu cha mabasi mjini Lindi na kushuhudia msongamano wa mabasi, huku Jeshi la Polisi lililoongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, George Mwakajinga, akilazimika kutumia ushawishi wa kila aina kwa madereva na abiria waliokuwapo kituoni hapo wasafiri wakiahidi kuyasindikiza magari hayo.

MTANZANIA

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: