Pinda azuru waathirika, adaiwa kubagua
Magari ya deraya ya kijeshi (APC), yakipita
kwenye mitaa ya mji wa Mtwara jana. Hali katika mji wa Mtwara imetulia
baada ya ghasia za siku tatu za kupinga ujenzi wa bomba la kusafirisha
gesi asilia kutoka mikoa ya Kusini kwenda jijini Dar es Salaam.
Mji wa Mtwara jana uligubikwa na harakati nzito za uzinduzi wa kiwanda cha sementi cha kampuni ya Dangote Group hafla iliyohudhuriwa na idadi kubwa ya viongozi wakiwamo, mawaziri watatu wakiongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda pamoja na mabalozi kadhaa.
Katika hafla hiyo iliyotumika kujibu harakati za wananchi wa Mtwara wanaodai kunufaika zaidi na gesi asilia inayochimbwa mkoani humo wakipinga mipango ya kuisafirisha kwa bomba kwenda Dar es Salaam ambazo zilisababisha vurugu kubwa na maafa wiki iliyopoita. Mbalozi waliokuwapo ni wa Urusi, Misri, Angola, Nigeria na Kenya.
Mawaziri waliohudhuria ni pamoja na wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk. Mary Nangu, kila mmoja alijenga hoja ya kuwatuliza wakazi wa Mtwara jinsi watakavyofaidi na gesi hiyo kutokana na uwekezaji.
Akiweka jiwe la msingi katika eneo litakalojengwa kiwanda hicho kikubwa cha saruji Afrika Mashariki na Kati katika kijiji cha Hiari, kata ya Namayanga, Pinda alisema ujenzi wa kiwanda hicho ni mchango mkubwa kwa maendeleo ya taifa kwa kuwa sekta ya ujenzi inachangia katika kasi ya ukuaji wa uchumi.
“Mahitaji ya saruji nchini kwa sasa ni tani milioni tatu na viwanda vinne vilivyopo nchini kwa sasa vinazalisha tani milioni 1.2 sawa na mifuko 70,000 kwa siku, kiasi ambacho ni kidogo sana,” alisema Waziri Mkuu.
Aidha, alisema kiwanda hicho kitaweza kuzalisha tani milioni tatu kwa mwaka sawa na mifuko 150,000 kwa siku na kutoa ajira za moja kwa moja 1,000 na ajira zisizo za moja kwa moja 9,000.
Waziri Mkuu alisema viwanda vilivyopo nchini vinakabiliwa na changamoto mbalimbali kama kukosekana kwa umeme wa uhakika, malighafi
ya mawe ya chokaa ambayo huhitajika kwa asilimia 80 kwenye uzalishaji, gesi ya kuyeyusha mawe hayo na kwamba gharama kubwa ya saruji inasababisha isinunulike.
Alisema kutokana na kugundulika kwa gesi asilia mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Lindi na Mtwara, itakuwa maalum kwa ajili ya viwanda vya saruji kwa kuwa malighafi muhimu ya gesi na mawe inapatikana kwa uhakika hasa mkoani humo katika kijiji cha Msijute.
Alisema iwapo saruji itapatikana italeta mabadiliko makubwa kwani wanachi wa mkoa huo watainunua kwa bei rahisi na kujenga nyumba za kisasa.
KAMPUNI 51 KUWEKEZA MTWARA
Kadhalika, Pinda alisema kampuni 51 zimewasilisha maombi ya kuwekeza mkoani humo katika Kutuo cha Uwekezaji (TIC).
Kampuni hizo na idadi ya miradi kwenye mabano kuwa ni mitambo ya luninga na redio (3), kilimo (2), usindikaji korosho (7), majengo ya kampuni na ofisi (2), majisafi (2), bidhaa zitokanazo na saruji (3), mbolea (1), mikate (1), matangi ya mafuta (2), kiwanda cha ujenzi wa maboti (1), mbao (1), utalii (14), uchimbaji na watafutajia wa mafuta (1), usafirishaji (8) na plastiki (1).
Alisema katika kukuza uchumi wa mkoa huo na mingine, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), imeitisha zabuni kwa ajili ya ujenzi wa gati nne za meli kubwa kwenye Bandari ya Mtwara.
Alisema serikali inaangalia uwezekano wa kuboresha eneo la Mikindani ili meli za abiria na mizigo zitie nanga kwenye eneo hilo.
Aliongeza kuwa serikali iko kwenye mazungumzo na serikali za Denmark na Korea kuangalia uwezekano wa kupata meli kubwa ya kusafirisha mizigo na abiria.
RELI MTWARA HADI NJOMBE
Kwa mujibu wa Pinda, serikali itajenga reli kutoka Mtwara hadi Mchuchuma na Liganga mkoani Njombe na zabuni ya kazi hiyo imeshatangazwa sambamba na ujenzi wa barabara za kuunganisha wilaya na makao makuu ya mkoa kwa kiwango cha lami.
Aliwataka wananchi wa mkoa huo kudumisha amani na utulivu kwa kuwa bila hivyo maendeleo kusudiwa hayawezi kufikiwa na watafukuza wawekezaji.
“Gesi itakayochukuliwa kwenda Dar es Salaam ni gesi safi, wananchi wa Mtwara wataunganishiwa gesi ya kupikia nyumbani kwa bei ya Shilingi 25,000 kwa mwezi tofauti na sasa mtungi huuza kwa zaidi ya Shilingi 50,000 na haimalizi mwezi,” alisema Pinda.
Alibainisha kuwa serikali imekuwa ikitumia zaidi ya Sh. trilioni 1.6 kwa ajili ya ununuzi wa mafuta mazito na dizeli ya kuzalisha umeme, hivyo
kiasi cha asilimia moja cha gesi ndicho kitachukuliwa kwenda Dar es Salaam kuzalisha umeme.
“Nia ya serikali ni njema sana, ni lazima tutumie rasilimali hizi kwa amani na utulivu, miaka yote tumekuwa tukinufaika na rasilimali za
nchi bila kubaguana,” alisema Pinda.
Awali, Mkurugenzi wa Dangote, Alhaji Aliko Dangote, alisema ujenzi wa kiwanda hicho utamalizika baada ya miezi 22 na utagharimu
Dola za Marekani milioni 500 (Sh. bilioni 802.5)
Alisema kampuni yake itajenga soko, kliniki na shule. Pia imeshatenga Sh. milioni 450, kwa mgawanyo wa kila idara kupata Sh. milioni 150, kwa vikundi vya kinamama, vijana na watoto, lengo likiwa ni kuikomboa Afrika ijitegemee kiuchumi kwa kuwa naye ni Mwafrika.
Waziri Nangu alisema Baraza la Utekelezaji litakwenda mkoani humo kutoa mafunzo kwa wananchi kujua jinsi ya kuchangamkia fursa zilizoletwa na uwekezaji.
Sherehe hizo zilihudhuriwa pia na viongozi wa dini, wanasiasa na viongozi wa mashirika mbalimbali.
PINDA AZURU WALIOATHIRIKA, ABAGUA
Katika hatua nyingine, jana Pinda alitembelea maeneo ya taasisi na nyumba za viongozi yaliyofanyiwa hujuma, kuchomwa moto na uharibifu wa mali uliosababishwa na vurugu za kupinga gesi asilia kusafirishwa kwa bomba.
Pinda alitembelea nyumba za Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mtwara,
Mohamed Sinani; Mbunge wa Mtwara Vijijini na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia, zilizochomwa moto na kubomolewa katika mtaa wa Sinani.
Pia alitembelea ofisi ya CCM ya Wilaya Mtwara Vijijini, Mahakama ya Mwanzo ya Mikindani, ofisi ndogo ya Mbunge wa Mtwara Mjini na ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Mikindani.
Hata hivyo, Waziri Mkuu hakutembelea maeneo ya nyumba za wananchi zilizochomwa
moto wala kutembelea Hospitali ya Mkoa wa Mtwara walikolazwa majeruhi wa vurugu hizo.
Serikali mkoani Mtwara haikueleza sababu za kutompangia Waziri Mkuu ratiba ya kutembelea nyumba za wananchi na hospitali ya mkoa.
Kutokana na hali hiyo, wananchi walilalamikia hatua hiyo kwa kudai ni ya kibaguzi kwa kuwa hujuma na uharibifu ulitokea ulizathiri pande zote.
Mariam Abdalah, mkazi wa Magomeni, ambaye alidai kuchomewa nyumba yake na askari polisi na hadi sasa analala nje, alisema alitarajia ujio wa viongozi wa serikali ungekuwa faraja kwake kwa kuwa hakuhusika katika vurugu hizo, lakini ameathirika.
Mei 24, mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, alitembelea maeneo yaliyoathirika zikiwamo nyumba tatu za askari polisi, na wakati akiwa katika nyumba ya mwandishi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Kassim Mikongolo, mama mmoja, Shakela Kaiza, aliwasilisha kilio chake kwa Waziri huyo cha kuchomewa nyumba na askari polisi na kumtaka Waziri kuitembelea.
Hata hivyo, Waziri Nchimbi alimuhoji askari wa Zimamoto ambaye alisema kitaalamu moto huo ulikuwa wa bahati mbaya na ilitokana na bomu la machozi.
Pinda wakati akiangalia nyumba za taasisi na za viongozi zilizoathiriwa na ghasia hizo, alifuatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na hakusema chochote zaidi ya kusikiliza maelezo kutoka kwa wahusika.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment