Aliyekuwa Mhasibu Mkuu wa Kampuni ya Jambo Concepts Tanzania Limited, marehemu Vick Mgoyo
MHASIBU Mkuu wa Kampuni ya Jambo Concepts (T) Limited inayochapisha
gazeti la Jambo Leo, Staa Spoti, Dar Metro na jarida la Jambo Brand
Tanzania, Vicky Mgoyo (49), amefariki dunia.
Meneja Mkuu wa Jambo Concepts, Ramadhani Kibanike, alisema marehemu
Vicky Mgoyo alifariki dunia leo asubuhi kwenye Hospitali ya Kairuki
jijini Dar es Salaam alikokimbimbizwa kupatiwa matibabu baada ya
kuzidiwa usiku wa kuamkia leo.
Alisema kifo cha Vicky zaidi akijulikana kwa jina la Mama Mgoyo kimeacha
pengo kubwa si tu kwa familia yake bali pia kwa Kampuni ya Jambo
Concepts kutokana na kwamba alikuwa ni mtu mwaminifu kazini, lakini pia
uhusiano mzuri na wafanyakazi wenzake.
"Tumepoteza mfanyakazi ambaye ni mchapa kazi na kipenzi cha wengi,
tutamkumbuka kwa hilo. Naomba wafanyakazi tuungane na ndugu na jamaa
katika kuomboleza msiba wa kipenzi chetu huku tukiamini kuwa haya ni
mapenzi ya Mungu.
"Bado hatujapata taarifa rasmi za maziko, ila taratibu za kusafirisha
mwili wa marehemu kwenda mkoani Kilimanjaro nyumbani kwao zinaendelea
kufanyika," alibainisha Kibanike.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Juma Pito alitoa mwito kwa
wafanyakazi kuonesha mshikamano katika kipindi hiki kigumu na cha
majonzi kwa kuondokewa na mfanyakazi mwenzao.
Mhariri Mkuu wa Jambo Leo, Anicetus Mwesa, akizungumzia msiba huo
alisema Mama Mgoyo ametwaliwa na Mungu ilhali akiwa bado anahitajika na
familia pamoja na ofisi yake, hivyo ameacha pengo ambalo litachukua muda
kuliziba.
"Mwenzetu ametangulia nasi tupo nyuma yake, zaidi tumwombee ili Mungu ampumzishe katika raha ya milele," alisema Mwesa.
Kwa upande wake Mpiga Picha Mkuu wa gazeti hili, Richard Mwaikenda,
alisema atamkumbuka Vicky kwa kuwa ni mwanamke shupavu ambaye alikuwa
anazingatia maadili ya kazi yake ya uhasibu.
Pia alisema alikuwa ni mama mjane makini ambaye alihakikisha anasimamia
watoto wake katika suala la kuwapa elimu bora, ambapo katika hilo
alikuwa akifanya kila anachoweza kuhakikisha anasomesha nje ya nchi tena
kwenye shule bora na makini.
Vicky Mgoyo aliyezaliwa Novemba 26, 1964, ameacha watoto watatu huku wawili kati yao ni wanaume.
Alilazwa katika Hospitali ya Kairuki wiki iliyopita ambako alipatiwa
matibabu kwa muda wa siku nne na kuruhusiwa.Jumatatu aliripoti kazini na
kuendelea na kazi hadi jana jioni, ambapo usiku alizidiwa na hatimaye
leo asubuhi Mungu alimchukua. Mungu ailaze pema peponi roho ya Vicky
Mgoyo.
No comments:
Post a Comment