Arusha. Mtuhumiwa mmoja kati ya tisa waliotiwa mbaroni kuhusiana mlipuko wa bomu katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Arusha na kusomewa mashtaka 21 yakiwamo ya mauaji na kujaribu kuua.
Mbele ya Hakimu Mkazi, Devotha Kamuzora, mtuhumiwa
huyo, Victor Ambrose (20), dereva wa Bodaboda na mkazi wa eneo la Kwa
Mromboo, Arusha alisomewa mashtaka hayo yakiwamo matatu ya mauaji ya
watu watatu waliofariki katika tukio hilo lililotokea Mei 5, mwaka huu.
Wakisoma kwa kupokezana hati ya mashtaka, Mawakili
wa Serikali, Zachariah Elisaria na Haruna Matagane walidai Calist pia
anatuhumiwa kwa makosa 18 ya kujaribu kuua.
Mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo
kimyakimya akiwa chini ya ulinzi wa maofisa wa polisi na hakutakiwa
kujibu lolote kwa sababu mashtaka yanayomkabili yanapaswa kusikilizwa na
Mahakama Kuu.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 27, mwaka huu itakapotajwa tena na mtuhumiwa amerudishwa mahabusu.
Saa moja kabla ya Ambroce kupandishwa kizimbani
saa nne asubuhi, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas
aliitisha mkutano na waandishi wa habari kitendo ambacho kiliwafanya
baadhi yao kushindwa kufuatilia vyema tukio hilo.
Waarabu waachiwa huru
Polisi imewaachia huru raia wanne wa kigeni
waliokuwa wakishikiliwa kuhusiana na tukio hilo baada ya uchunguzi
uliofanywa na Polisi wa Tanzania, Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI)
na Polisi wa Kimataifa (Interpol) na kubaini hawakuhusika.
Kamanda Sabas aliwaambia waandishi wa habari
ofisini kwake jana kuwa raia hao walikamatwa baada ya kutiliwa shaka
walipoonekana wakitoka kwenye hoteli moja karibu na Kituo Kikuu cha
Mabasi Arusha, muda mfupi baada ya tukio hilo.
Raia watatu wa Falme za Kiarabu(UAE), walioshikiliwa na kuachiwa wamegundulika kuwa ni watumishi wa Serikali.
Kamanda Sabas aliwataja kuwa ni Abdul Azziz
Mubarak (30), (Mamlaka ya Mapato), Fouad Saleem Ahmed Al Hareez Al Mahri
(29), (Zimamoto) na Daeed Abdulla Saad (28), ambaye ni Askari wa
Usalama Barabarani.
Mtaalamu mwingine alichambua bomu
Raia hao pamoja na mwenzao, Al-Mahri Saeed Mohseen (29) kutoka
Saudi Arabia, walikabidhiwa kwa Idara ya Uhamiaji kuchunguzwa iwapo
waliingia nchini kihalali.
Waliachiwa katika kipindi ambacho Serikali ya
Tanzania ilikuwa ikikabiliwa na shinikizo kutoka kwa mabalozi wa nchi
wanakotoka wakipinga kukamatwa kwao na kutangazwa kwenye vyombo vya
habari. Mabalozi wa nchi hizo za Mashariki ya Kati walifuatana na
wanasheria wao kwenda kuangalia hali za watuhumiwa kutoka nchi zao huko
Arusha.
Balozi wa Saudi Arabia, Hani Abdalla Momenah aliliambia gazeti la Al-Hayat la nchi yake akidai watu wao alikamatwa kwa hisia tu.
“Tuna matumaini makubwa kuwa watu wetu wataachiwa
huru na tutaendelea kufuatilia suala lao hadi tuone mwisho wake,”
alieleza Balozi huyo, ambaye akisisitiza asingeondoka Arusha hadi
kieleweke.
Kaimu Kamanda wa Uhamiaji Mkoa wa Arusha, Kamishna
Msaidizi, Vitalis Mlay alisema tayari wageni hao wameondoka nchini
kupitia Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam.
Raia hao waliingia nchini Mei 4, mwaka huu, siku
moja kabla ya tukio hilo la bomu na walifika Arusha alfajiri ya siku ya
tukio na kwamba wangekaa nchini kwa shughuli za kitalii kwa siku tatu.
Mtaalamu mwingine alichambua bomu
Ofisa Usalama Mwandamizi katika Shirika la Umoja
wa Mataifa (UN) ameunga mkono kauli Polisi mkoani Arusha kwamba
uchunguzi wa awali umeonyesha kwamba bomu lililolipuliwa
halikutengenezwa kienyeji akisema maelezo aliyopata huenda
limetengenezwa kiwandani.
Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ), aliyekataa kutaja jina lake, alisema msingi wa maelezo
yake ni kutokana na vyuma vilivyotawanyika na kuumiza zaidi ya watu 20.
“Mabomu ya aina hii nayafahamu kwani yanatumika vitani zaidi na ni mahsusi kwa kutupa kwa mkono,” alisema.
MWANANCHI
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment