Waombolezaji wakitoa mwili wa marehemu Zulu kuiingiza kwenye gari |
Mwili wa Ofisa Habari Mkuu
wa Bunge, Ernest Zulu (56) aliyefariki Mei 23 mwaka huu nchini Malaysia
alikokuwa masomoni, umewasili nchini majira ya saa 1.30 asubuhi kwa ndege ya
Shirika la Ndege la Qatar.
Majira ya mchana mke wake
Theresia Zulu na watoto wake walifika kumtambua marehemu na kisha kundi la
waombolezaji lilimsindikiza marehemu katika gari ili kuanza safari
yake ya mwisho kabla ya kwenda kupumzika milele kijiji kwao ndilima, Songea
vijijini.
Kwa wakazi wa dare s salaam
Zulu ataagwa kesho nyumbani kwake Ubungo Kibangu.
Baadhi ya watu waliokuwapo
mchana wa leo uwanja wa ndege kuupokea mwili wa Zulu ni Katibu wa Bunge, Dk
Thomas Kashililah na waumini wa Kituo cha Maombezi cha Marian Ubungo,
wakiongozwa na Padri Felician Nkwera.
Kwa mujibu wa ndugu wa
karibu wa marehemu ambaye hakuwa tayari kutaja jina gazetini , Zulu
alikutwa damu zikimtoka sehemu ya kichwa na kuegama mezani akiwa
ameshika msalaba na picha ya Bikira Maria vilivyokuwa chumbani. Awali, taarifa ya Katibu
huyo kuhusu kifo hicho, iliyotolewa na Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na
Uhusiano wa Kimataifa Ofisi ya Bunge, Dodoma ilieleza kuwa Zulu alikuwa
akisumbuliwa na maradhi ya kichwa kwa muda mrefu.
Zulu
aliyeacha mjane na watoto wanne, Philomena, Maria Emmaculate, Felistas na
Augustina, alikuwa nchini Malaysia, akisoma Shahada ya kwanza ya
Mawasiliano na Usimamizi wa Vyombo vya Habari katika Chuo Kikuu cha Taylor
tangu Julai 2010, na alitarajiwa kumaliza masomo yake Julai, mwaka huu.
Alizaliwa Julai 10 mwaka
1957 huko Songea. Alipata elimu ya msingi na sekondari Songea kabla ya kusomea
uandishi wa habari katika Chuo cha Uandishi wa Habari (TSJ) (sasa SJMC-UDSM)
jijini Dar es Salaam.
Aliwahi kufanyakazi katika
Shirika la Utangazaji la Tanzania (RTD) sasa TBC Taifa mwaka 1976 kama
Mwandishi wa Habari Msaidizi na hatimaye kupandishwa cheo kuwa Mwandishi wa
Habari kabla ya kuhamia Shirika la Magazeti la Chama (Uhuru na Mzalendo) kama
Mwandishi Mwandamizi mwaka 1985.
Mwaka 1986 hadi 1987 alipata
fursa ya kusomea masomo ya Uandishi wa Habari ya Kimataifa huko nchini Urusi.
Mwaka 1991 aliajiriwa kama Mhariri Msaidizi katika gazeti la The Express kabla
ya kujiunga na Sauti ya Ujerumani ambapo alifanya kazi kama Mwandishi
Mwandamizi kuanzia mwaka 1995.
Aliajiriwa na Bunge mwaka
1998 kwa cheo cha Ofisa Habari Mwandamizi, mpaka mauti inamkuta alikuwa Afisa
Habari Mkuu Daraja la Pili.
No comments:
Post a Comment