Dar es Salaam. Kauli ya Serikali iliyotolewa bungeni juu ya kufutwa kwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne na sababu za kufeli kwa wanafunzi wengi, imeibua utata baada ya taarifa kadhaa kuonyesha kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilibariki mabadiliko ya mfumo mpya wa kupanga madaraja.
Taarifa ya Serikali iliyosomwa bungeni Mei 3,
mwaka huu na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge,
William Lukuvi ilisema Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), lilifanya
mabadiliko ya mfumo bila kushirikisha wadau.
“Baraza la Taifa la Mitihani lilikuwa linachakata
alama za mwisho kwa kutumia mfumo ambao ulikuwa unabadilika kwa
kutegemeana na hali ya ufaulu wa mwanafunzi... lakini mwaka 2012
lilitumia mfumo mpya wa kuwa na viwango maalumu vya kutunuku (fixed
grade ranges).”
“Tume imebaini kwamba, pamoja na mfumo huo
kuandaliwa kwa nia nzuri, utaratibu huo mpya haukufanyiwa utafiti na
maandalizi ya kutosha kabla ya kutumika.
“Baraza la Taifa la Mitihani limeelekezwa
kuzingatia kuwa pamoja na kwamba sheria ya kuanzishwa kwake inawaruhusu
kufanya marekebisho ya mchakato wa mtihani, lakini marekebisho yoyote ya
kubadilisha utaratibu wa kupanga viwango vya ufaulu na madaraja ya
matokeo ya mtihani lazima yahusishe wadau wote wanaohusika na mitalaa,
ufundishaji na mitihani.”
Kwa mujibu wa vielelezo vilivyochapishwa na Gazeti
la Wiki la Jamhuri, mfumo huo ulipitishwa na Serikali kupitia Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Nyaraka hizo zinaonyesha kuwa, kikao kilichokutana
na kujadili mapendekezo ya Necta ya kubadili mfumo huo kiliongozwa na
Waziri wa Elimu, Dk Shukuru Kawambwa na Katibu wake alikuwa Naibu Waziri
wa Elimu, Philip Mulugo.
Muhtasari wa kikao hicho unaonyesha wajumbe wa
mkutano huo walikuwa ni pamoja na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo
Selestine Gesimba, Kamishna wa Elimu, Profesa Eustell Bhalalusesa,
Paulina K Mkonongo, Marystella Wassena, T.E. Temu, Katibu Mtendaji wa
Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte), Dk Primus Nkwera, Bunyanzu
Ntmabi, H.A Lihawa wote wakiwa wajumbe kwa upande wa Wizara.
Kutoka Necta wajumbe walikuwa ni Dk C.E Msonde,
Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk Joyce Ndalichako, Mwenyekiti wa Bodi
ya Necta, Profesa Rwekaza Mukandara pamoja na Profesa Sifuni Mchome,
ambaye ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU).
Aidha, Gesimba alimwandikia barua Katibu Mtendaji
wa Necta yenye kumbukumbu namba CAC.109/437/01N Desemba 12 mwaka jana
akiliagiza kutumia mfumo mpya wa kukokotoa alama za mitihani ya kidato
cha nne na sita.
“Tafadhali rejea kikao kilichofanyika tarehe
10/12/2012 katika ukumbi wa mikutano wa wizara kuhusu somo tajwa hapo
juu (Maagizo ya kuhusu utaratibu wa matumizi ya viwango vya ufaulu
katika mitihani ya kidato cha nne na sita).
“Viwango vya ufaulu vilivyopendekezwa na Baraza la
Mitihani la Tanzania vitumike kwa mitihani ya Kidato cha Nne 2012 na
Kidato cha Sita kwa mwaka 2012 tu
“Viwango vya kutunuku (grade rage) vifanyiwe kazi zaidi ili
kupunguza au kuondoa mrundikano (bunching) wa alama katika kundi moja.”
“Necta ifanye utafiti kuhusu matumizi ya alama za
maendeleo kwa O level (kidato cha kwanza mpaka cha sita) na A Level
(kidato cha tano na sita) na kutoa mapendekezo mapya ya matumizi ya
alama za maendeleo (continuous assessment).”
“Utekelezaji wa maagizo haya ufanyike mapema ili
mapendekezo yaliyowasilishwa yaweze kuanza kutumika katika Mwaka wa
Fedha 2013/2014.”
Mbali na barua hiyo, Profesa Bhalalusesa aliandika
barua kwa Katibu Mtendaji wa Necta, Novemba 14, mwaka huu kuhusu
utaratibu wa matumizi ya alama za maendeleo ya mtihani na viwango vya
ufaulu katika mitihani ya taifa.
“Rejea kichwa cha habari hapo juu na barua yako
yenye kumbu Na. MTS. 1/29/VOL.XII/61 ya tarehe 20/09/2012. Kutokana na
maelezo ya barua yako, Wizara imeridhia mapendekezo ya uwiano wa alama
za maendeleo ya wanafunzi (CA) na alama za mtihani wa mwisho
kubadilishwa kutoka alama 50:50 na kuwa 30:70.”
“Wizara inaridhia pia alama 15 zitokane na mtihani wa kidato cha pili kwa wanafunzi wa kidato cha nne.”
“Aidha, wizara inataka mlete mchanganuo wa jinsi
alama 15 zilizobakia zitakavyopatikana ili kuleta uelewa wa pamoja.
Vivyo hivyo, mchanganue utaratibu wa mgawanyo wa alama za maendeleo ya
mwanafunzi wa kidato cha sita,” ilisema.
Akizungumza na mwandishi wetu jana, Dk Kawambwa
alisema hawezi kuzungumza chochote na badala yake atafutwe Mwenyekiti wa
Tume ya Kuchunguza Kushuka kwa Kiwango cha Ufaulu wa Mtihani huo,
Profesa Sifuni Mchome kwa kuwa kwa sasa masuala yote yapo chini yake.
“Naomba nisi-comment (nisizungumze) chochote kwa
sasa, muulizeni Profesa Mchome kwa kuwa sasa hivi mambo yote yapo chini
ya tume, nikizungumza nitawaudhi,” alisema.
Hata hivyo, jana Profesa Mchome ambaye pia alikuwa
mjumbe wa kikao kilichopitisha mapendekezo hayo ya awali, hakupatikana
kuzungumzia madai hayo lakini juzi akizungumza na mwandishi wetu alisema
tume yake ilibaini kuwa Necta na wizara walikubaliana mwaka jana kuanza
kutumia kanuni hiyo na utekelezaji wake ukaanza mwaka jana jambo ambalo
halikuwa sawa.
Alisema mabadiliko makubwa kama hayo yalipaswa
kuchukua angalau miaka minne ili watoto waandaliwe kuanzia kidato cha
kwanza na waje wapimwe wanapofika kidato cha nne.
“Vyote hivi ni vyombo vya Serikali (Necta na
Wizara ya Elimu) kwa hiyo kujikosoa siyo tatizo, sisi tumeona hilo ni
tatizo na tukapendekeza hivyo na Serikali ikaamua kujikosoa,” alisema.
Alisema kuwa baada ya mabadiliko yanayoweza kufanyika bila kushirikisha wataalamu wengi lakini suala la alama za mtihani kwa kuwa tayari matokeo yake yameonekana baada ya kujaribiwa, ni vyema wadau wakashirikishwa zaidi.
MWANANCHI
Alisema kuwa baada ya mabadiliko yanayoweza kufanyika bila kushirikisha wataalamu wengi lakini suala la alama za mtihani kwa kuwa tayari matokeo yake yameonekana baada ya kujaribiwa, ni vyema wadau wakashirikishwa zaidi.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment