Arusha. Watu watatu, waliofariki katika
shambulio la bomu katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi,
Parokia ya Olasiti, mkoani Arusha wamezikwa jana na mamia ya watu, huku
ulinzi ukiwa umeimarishwa kuliko kawaida na viongozi wa dini na
Serikali kutoa kauli nzito.
Marehemu hao, ni Regina Loning’o Laizer (45),
James Gabriel(16) na Patricia Joachim Assey(9) walizikwa katika eneo la
kanisa hilo Katoliki, mazishi yaliyohudhuriwa na maaskofu wanane wa
majimbo tofauti ya Kanisa Katoliki, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania(KKKT), Askofu Alex Malasusa, Waziri Mkuu Mizengo
Pinda na viongozi mbalimbali wa dini, Serikali na kisiasa.
Kauli za viongozi
Katika ibada hiyo ya viongozi mbalimbali wa
kidini, walitoa salama zao akiwamo Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa
Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa aliyeitaka
Serikali kutumia msamiati wa mwenye macho haambiwi tazama na kukomesha
mpasuko wa kidini aliosema unalitafuna taifa.
Askofu huyo alisema kuwa miongo mitatu sasa,
Serikali imekaa kimya, ikishuhudia mafundisho na mihadhara ya kidini
inayochochea na kuhamasisha uhasama kati ya Ukristo na Uislamu, bila
kuchukua hatua kukomesha hali hiyo.
“Matukio mbalimbali yanayoashiria uhasama wa
kidini yanayotokea nchini. Kuna mihadhara, CD, DVD, machapisho na
mafundisho yanayotishia maisha na usalama wa viongozi wa kanisa na
waumini wao, ambayo yamefuatiwa na uchomomaji wa makanisa,” alisema
Askofu Ngalalekumtwa.
Alitaja mfano wa kongamano la Januari 15, mwaka
juzi iliyofanyika Ukumbi wa Diamond Jubillee jijini Dar es Salaam kuwa
moja ya mikutano iliyojaribu kuchochea chuki ya kidini kati ya Waislamu
na Wakristo kwa kudai kuwa Serikali ya Tanzania inaongozwa kwa mfumo
Kikristo ulioasisiwa na Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Askofu huyo alisema kwamba katika kongamano hilo,
washiriki waliaminishwa kuwa Serikali inatoa fedha za ruzuku kujenga
shule na taasisi za kanisa kutokana na kuwapo mkataba maalumu kati ya
kanisa na Serikali, jambo ambalo siyo kweli.
“Kinachosikitisha zaidi ni kwamba Serikali
haikukanusha madai na uchochezi huo, licha ya mambo hayo kufanyika na
kusemwa hadharani kwa wahusika kuzunguka nchi nzima kueneza chuki na
uchochezi huo,” alisema Askofu Ngalalekumtwa.
Mkuu wa Kanisa la KKKT, Askofu Dk Alex Malasusa
alisema kuwa tukio la Arusha ni la kikatili na aibu kwa taifa akiwataka
wenye dhamana ya ulinzi na usalama kuchukua hatua kudhibiti hali hiyo
akionya kuwa wasipofanya hivyo watahukumiwa kwa kosa la kukaa kimya
mambo yakiharibika mikononi mwao.
“Wote wenye jukumu la kulinda na kuitunza amani
waifanye kazi hiyo bila uoga. Wasipofanya hivyo iko siku watahukumiwa,”
alisema Dk Malasusa
Mwakilishi wa Muungano wa Madhehebu ya Kikristo
mkoani Arusha, Askofu Stanley Hotay aliwataka viongozi wa kisiasa
kuepuka kutumia jukwaa la dini kutimiza malengo ya kisiasa, akionya kuwa
makanisa hayana itikadi, bali waumini ndiyo wenye itikadi mbalimbali.
Salamu za Serikali
Ulinzi waimarishwa
MWANANCHI
“Sote tuliomo ndani ya jahazi lazima tuwakemee na kuwadhibiti
vichaa wanaojaribu kutoboa jahazi letu kwani tusipofanya hivyo maji
yatajaa ndani, chombo kitazama na sote tutaangamia,” alisema Askofu
Hotay.
Ibada hiyo iliyohudhuriwa pia na baadhi ya
viongozi wa dini ya Kiislamu, ilioongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa
Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali
Pengo aliyetoa wito kwa waumini wa kanisa hilo, kutolipiza kisasi,
akisema kuwa waliohusika ni watu wasiofuata dini.
“Tusilipize uovu kwa uovu, yapaswa kushinda uovu
kwa wema…; Tuache kunyoosheana kidole kutokana na tukio hili,” alisema
Kardinali Pengo.
Pengo ambaye hivi karibuni, alinukuliwa na vyombo
vya habari akieleza kuwa shambulio hilo halina uhusiano na masuala ya
kidini hasa kutokana na taarifa za uhakika alizopewa akisema
waliotekeleza shambulio hilo ni waovu wenye nia ya kuligawa taifa na
kuliingiza katika migogoro ya kidini.
Viongozi wa kisiasa waliohudhuria ni pamoja na
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi,
James Mbatia na wabunge kadhaa.
Salamu za Serikali
Akitoa salamu za Serikali katika ibada hiyo ya
mazishi, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alitoa pole kwa tukio hilo akaeleza
kuwa yoyote anayedhani kuua muumini mmoja, Askofu au Mufti ataua
Ukristo au Uislamu, hajui kuwa hiyo haitawezekana.
Pinda alisema Serikali imetoa Sh100 milioni ikiwa
ni rambirambi zake akiongeza kuwa dini za Kikristo na Kiislamu zina
historia ndefu duniani.
“Itakuwa ni kujidanganya kuwa ukiua kiongozi wa
dini leo utaifuta dini hiyo, kwani kwa kuamini hivyo hiyo ni ndoto,”
alisema Pinda.
Waziri Mkuu, alisema kwamba Serikali imeagiza
vyombo vyote vya usalama nchini, vifanye kazi usiku na mchana
kuhakikisha amani na utulivu unaendelezwa nchini.
Aliwataka Watanzania kuwa watulivu, hasa
watakaposikia kamatakamata inaendelea na kueleza kuwa lengo la hatua
hiyo ni kulinda amani ya nchi.
Ulinzi waimarishwa
Ulinzi uliimarishwa eneo lote kuzunguka kanisa hilo, barabara za
kuingia Parokia hiyo na katikati ya Jiji la Arusha. Maofisa wa Polisi
na Usalama kutoka makao makuu jijini Dar es Salaam na Maofisa Usalama wa
Taifa kutoka maeneo mbalimbali waliimarisha ulinzi.
Askari wenye silaha za moto na mabomu, waliranda
juu ya kanisa hilo kwa kupeana zamu, huku baadhi wakiwa na miwani na
kuona mbali. Maeneo mengine askari wanafunzi wa Chuo cha Polisi Moshi,
walikuwa wameimarisha ulinzi na kuwapekua waliowatilia shaka
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment