Dar es Salaam. Idadi ya watahiniwa waliofaulu
mtihani wa kidato cha nne mwaka jana imeongezeka kwa kati ya asilimia 20
na 23 baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), kufanya marekebisho
alama za viwango vya ufaulu, Mwananchi limebaini.
Habari ambazo gazeti hili imezipata zinasema
matokeo hayo ambayo yamewezesha kiwango cha ufaulu kupanda na kufikia
asilimia kati ya 54 na 57, huenda yakatangazwa wiki hii pamoja na yale
ya kidato cha sita ambayo pia yamechelewa kutangazwa.
Chanzo cha habari kutoka Necta kimesema matokeo
hayo mapya yanaonyesha kuwa, ufaulu wa kuanzia daraja la kwanza hadi la
nne umeongezeka kutoka asilimia 34.5 kwa matokeo yaliyotangazwa awali na
huenda yakafikia asilimia 57. Hii inamaanisha kwamba watahiniwa wapatao
82,000 ambao awali walikuwa wamepata sifuri katika matokeo ya awali
sasa wamepanda na kupata madaraja ya ufaulu katika matokeo mapya.
Kwa matokeo hayo, watahiniwa wa mwaka 2012
watakuwa wamefanya vizuri kuliko wa mwaka 2011, ambao watahiniwa 225,126
sawa na asilimia 53.37 ya 349,390 waliofanya mtihani huo walifaulu.
Msemaji wa Necta, John Nchimbi alisema upangaji wa
matokeo hayo ulikuwa bado unaendelea. “Ninachojua kwa sasa ni kuwa
mchakato unaendelea na matokeo yatatangazwa mapema tu ili watoto waweze
kujiunga na shule mapema,” alisema Nchimbi.
Pia alisema usahihishaji wa mitihani ya kidato cha sita umekamilika.
Matokeo ya awali
Matokeo ya awali yaliyotangazwa na Waziri wa Elimu
na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa yalionyesha kuwa kati ya
watahiniwa 367,756 waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana,
waliokuwa wamefaulu kwa daraja la kwanza mpaka la tatu walikuwa 126,847
sawa na asilimia 6.4. Waliopata daraja la nne walikuwa ni 103,327 sawa
na asilimia 28.1.
Katika matokeo hayo, watahiniwa 240,909 sawa na
asilimia 65.5 walipata sifuri, hesabu ambayo imebadilika katika matokeo
mapya ambayo yanaonyesha kuwa sasa waliopata daraja hilo ni 158,100
ambayo ni asilimia 43.
Hata hivyo, habari kutoka Necta zinasema kuwa
licha ya kuwezesha kuongezeka kwa waliofaulu, matumizi ya kanuni mpya ya
kukokotoa matokeo hayo yalisababisha zaidi ya wanafunzi 2,500 kushuka
ufaulu ikilinganishwa na awali.
Maofisa mbalimbali wa Necta pamoja na wale wa
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na taasisi zake, walikutana
mwishoni mwa wiki iliyopita kukubaliana masuala mbalimbali juu ya
matokeo hayo pamoja na suala la matokeo ya wanafunzi hao 2,500 kabla ya
kutangazwa wiki hii.
“Baada ya wajumbe kujadili suala lile, busara
ilibidi itumike kwa hiyo hakuna mwanafunzi ambaye alama yake itashuka,
kwa kawaida isingewezekana mtoto ambaye matokeo yalitoka akiwa amefaulu
leo umwambie ameshuka,” kilieleza chanzo chetu.
MWANANCHI
Matokeo ya awali ndiyo chimbuko la kupitiwa upya baada ya wadau
kuyalalamikia na kumlazimisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuunda tume ya
kuyachunguza Februari 23, mwaka huu.
Kabla ya tume hiyo kuhitimisha shughuli zake,
ilitoa taarifa ya awali ambayo ilipendekeza kufutwa kwa matokeo hayo kwa
maelezo kwamba Necta ilitumia kanuni mpya ya kukokotoa matokeo bila
kushauriana na wadau.
Serikali ilitoa taarifa bungeni kwamba imeamua
kufuta matokeo ya 2012 na kuamuru yapangwe upya kwa kufuata madaraja
yaliyotumika mwaka 2011.
Ratiba ya Bunge
Wakati hayo yakiendelea, ratiba ya vikao vya Bunge
la bajeti imefanyiwa marekebisho na kusogeza mbele zamu ya Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambayo awali, ilikuwa imepangwa kusoma hotuba
yake ya makadirio ya matumizi leo, badala yake nafasi hiyo imepewa
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Wizara ya Elimu sasa imepangiwa kuwasilisha hotuba
yake Juni 4 mwaka huu, hatua ambayo inatajwa kwamba lengo ni kusubiri
kutangazwa kwa matokeo hayo ya kidato cha nne na kidato cha sita.
Wakati Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete
alipokutana na wabunge wa chama chake Mei 19, mwaka huu mjini Dodoma,
walisema hawako tayari kujadili hotuba ya wizara hiyo hadi matokeo ya
kidato cha nne na sita yatakapotangazwa.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment