
Na Mwandishi Wetu
WIKI iliyopita kuliibuka sakata
zito lililochukua nafasi kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii,
lililomuhusisha mama mmoja aliyejulikana kwa jina la Hezelina Mrema mkazi wa
Mbezi Beach, eneo la Tangi Bovu jijini Dar es Salaam, kuamua kuishi juu ya paa
la iliyodaiwa kuwa ni nyumba yake.
Taarifa za maamuzi ya
Hezelina kuishi juu ya paa la nyumba yake, zilipokelewa kwa hisia tofauti na
baadhi ya watu, ambapo ilifikia hatua baadhi ya vyombo vya habari vyenye
kuheshimika viliupotosha ukweli kwa kuliangalia suala hilo kwa upande mmoja.
Hatua hiyo ilisababisha
baadhi ya wanaharakati kujitokeza na kuahidi kumsaidia mama huyo, aliyedai kuwa
anataka kutolewa kwa nguvu ndani ya nyumba yake halali, ambayo ameijenga na
mumewe Samwel Opulukwa.
UKWELI WA MAMBO
Ukweli juu ya suala hilo ni
kwamba Hezelina hahusiki kwa namna yeyote na nyumba hiyo, ambayo ni ghorofa
moja, kwani imebainika kuwa si mke halali wa Opulukwa na badala yake wana
mahusiano ya kimapenzi.
Imebainika kuwa mke halali
wa Opurukwa alisha achana nae na mke wake huyo tayari alishaweka pingamizi
Mahakamani la kutaka hati ya nyumba hiyo isibadilishwe mmiliki.
Mbali ya Hazelina kutokuwa
mke halali wa Opulukwa pia imebainika kwamba mwanaume huyo aliitumia nyumba
hiyo kuweka dhamana ya mkopo kwenye benki ya TIB.
Imebainika kuwa hatua ya
Opulukwa kuweka nyumba yake dhamana ilikuja baada ya rafiki yake ambaye ni
mmiliki wa kampuni ya Asasu Express Ltd kuhitaji fedha za kuendeshea bishara
yake, lakini alikumbana na kikwazo cha kutakiwa kuwa na nyumba jijini Dar es
Salaam, ambapo kwa kuwa hakuwa nayo aliona amtumie rafiki yake huyo kufanikisha
mkopo wake kwa makubaliano kuwa ataulipa bila tatizo.
Hata hivyo mmiliki huyo wa
kampuni ya Asasu alishindwa kulipa mkopo huo wa mamilioni ya fedha, ambapo
benki husika ilianza harakati za kutaifisha mali zake ili kufidia deni hilo,
hata hivyo hazikutosha na ndipo walipoamua kuiuza nyumba hiyo ya Mbezi Beach
iliyopo kiwanja namba 235 Block D.
Imeelezwa kuwa benki ya TIB
ilimpa Opulukwa taarifa zote za deni husika pamoja na kumpa Notisi ya kumtaka alipe
deni husika ambalo ni 274,854, 256. 84 kutokana na rafiki yake kushindwa kulipa
deni husika pamoja na mali zake kutaifishwa.
Ili kufuata taratibu za
kisheria za kutaifisha nyumba ya Opulukwa, benki hiyo ilitoa tangazo la kutoa
tenda ya kuuza nyumba hiyo, ambalo lilitolewa kwenye gazeti la serikali Januari
10,2011.
Hata hivyo Opulukwa hakutoa
ushirikiano wowote, hali iliyosababisha benki ya TIB kuipiga mnada nyumba
hiyo na kufanikiwa kupata mteja, ambaye aliinunua kihalali ikiwa ni pamoja na
kubadilisha hati miliki ya nyumba hiyo.
Jambo la kushangaza
Opulukwa aliendelea kuishi ndani ya nyumba hiyo, TIB ilifanya harakati za
kumtoa kwa kuyatumia makampuni kadhaa ya udalali ambayo yalishindwa kufanikisha
kazi hiyo na ndipo Machi mwaka huu, jukumu hilo la kumtoa Opulukwa lilipelekwa
kwa kampuni ya udalali ya Msama Auction Mart, ambayo kwa weledi wa hali ya juu
ilifanikiwa kumtoa mkopaji huyo.
Baada ya Kampuni ya Msama
Auction Mart kufanya taratibu zake za kikazi na kuridhishwa na uwepo wa deni
husika, Juni 8, mwaka huu ilifika eneo la tukio na kuanza kumtoa Opulukwa.
Hata hivyo zoezi hilo
lilikuwa gumu kutokana na baadhi ya maofisa wa Polisi wa Wilaya ya Kinondoni
kuingilia kati, ambapo waliitisha kikao cha pamoja kati ya maofisa wa kampuni
ya Msama Auction Mart na Opulukwa, ambapo maamuzi yalikuwa ni kusimamisha zoezi
hilo hadi pale mkopaji huyo atakapopata baraka za Mahakama juu ya uhalali wa
kuendelea kuishi kwenye nyumba hiyo.
Baada ya maamuzi hayo ya
jeshi la polisi, Opulukwa alifungua kesi ya madai ya kuvunjiwa nyumba yake na
kuibiwa vifaa vyenye thamani ya shiringi 195 milioni, jambo ambalo halikuwa na
ukweli wowote.
Juni 11, mwaka huu mara
baada ya Opulukwa kukosa vielelezo vilivyompa uhalali wa kuendelea kuishi ndani
ya nyumba hiyo kama alivyoagizwa na Mkuu wa Polisi wilaya Kinondoni, kampuni ya
Msama Auction Mart iliendelea na zoezi la kumuondoa.
Wakati maofisa wa kampuni
ya Msama Auction Mart wakiwa na uhakika wa kukamilisha zoezi lao pamoja na
kuondoka eneo hilo,ghafla walipigiwa simu na walinzi walioachwa kwenye eneo
hilo kuwa kuna mtu yupo ndani ya nyumba, ambaye inaelezwa aliruka ukuta ili
kufanikisha lengo lake.
Hatua hiyo ya Hazelina
iliwashangaza maofisa wa Msama Auction Mart, ambao walichukua jukumu la kupiga
simu polisi ili kuhakikisha mama huyo anaondolewa kwa njia ya amani na utulivu.
Wakati huo tayari Hazelina
alikuwa ameshapanda juu ya paa la nyumba hiyo, huku akitishia kujirusha ili
kuutoa uhai wake endapo angetolewa kwa nguvu.
Aidha alikwenda mbali zaidi
kwa kuvua nguo ili kuonesha utupu wake, lengo lake likiwa ni kutowapa nafasi
walinzi wa kiume kutomsogelea.
Hatua ya mama huyu kuonesha
utupu wake na kuendelea kukaa juu ya paa la nyumba hiyo ilizua maswali na
kuwafanya baadhi ya waandishi wa Habari kufika eneo hilo ili kujua ukweli wa
mambo.
Kutokana na kauli za uongo
za mama huyo, alifanikisha kuwaaminisha waandishi wa habari kuwa kuna
hila zinafanyika ili kupora nyumba yake, ambayo alidai kuwa ni halali yao.
Hata hivyo maamuzi ya mama
huyo kuendelea kukaa juu ya paa la nyumba hiyo, yalidumu kwa muda wa siku
mbili, ambapo Juni 13, mchana kwa hiyari yake aliamua kushuka baada ya kumuona
jamaa yake akiwa ameshikilia karatasi zilizodaiwa kuwa zimetoka Mahakama ya
Kinondoni.
Uchunguzi wa gazeti hili
umebaini kuwa Opulukwa hakumueleza ukweli mama huyo, ambapo ukweli halisi wa
zoezi zima la kuhamishwa kwenye nyumba hiyo analijua.
Aidha imebainika kuwa
mwanamama huyo si mke wa Opulukwa, kwani mke wake halali anajulikana kwa jina
la Rachel Paulo Ng’wahi, amabaye ndiye aliyefungua kesi ya kupinga hatua ya
mume wake kutumia nyumba yao kumuwekea dhamana ya mkopo rafiki yake ambaye ni
mmiliki wa kampuni ya Asasu.
Ukweli ni kwamba benki ya
TIB na kampuni ya Msama Auction Mart, walikuwa sahihi kumuondoa Opulukwa kwenye
nyumba hiyo, hakuna sheria yeyote waliyoivunja na hawakuwa na nia ovu ya
kutaka kumpora mama huyo na Opulukwa aliyedai kuwa ni mumewe nyumba kama
alivyodai kwenye vyombo vya habari.
SOURCE: HABARI MSETO
No comments:
Post a Comment