Bayern
Munich imeshinda taji la EUFA Super Cup kwa kuichapa Chelsea mabao 5-4
kupitia mikwaju ya penalti katika mechi iliyochezwa jana usiku kwenye
uwanja wa Eden Arena mjini Prague, Jamhuri ya Cheki.
Beyern Munich, ikiongozwa na kocha wao
mpya, Pep Guardiola, imelipiza kisasi kwa kushindwa na Chelsea katika
fainali ya Champions League mwaka 2012 baada ya kuifunga klabu hiyo
mabao 5-4 kupitia mikwaju ya penalti kufuatia mtanange wa kuwania kombe
la UEFA Super Cup kuishia sare ya mabao 2-2 baada ya muda wa ziada
kumalizika.
Bao la Bayern sekunde chache kabla
mchezo kumalizika, liliufungua mlango wa kuelekea ushindi kupitia
penalti dhidi ya Chelsea chini ya kocha wao mpya, Jose Mourinho. Penalti
zote tisa ziliutikisa wavu kabla mkwaju wa penalti wa mchezaji wa
Chelsea, Romeu Lukaku, kuokolewa na kipa wa Bayern Munich, Manuel Neuer,
na hivyo kuwapa ushindi mabingwa wa Ulaya, Bayern Munich, dhidi ya
mabingwa wa ligi ya Ulaya, Chelsea.
Ushindi wa kwanza katika historia
Endelea kutizama tukio hili kwa kubofya hapa chini
Hii ni mara ya kwanza kwa Bayern
Munich kushinda kombe la UEFA Super Cup katika historia yake, baada ya
kupoteza fainali nyengine tatu. Fernando Torres aliifungia Chelsea bao
la kwanza dakika ya nane ya mchezo, pale alipopewa mpira na Mjerumani
Andre Shuerrle. Frank Ribery alisawazisha dakika ya 47 katika kipindi
cha pili kupitia mkwaju mkali akiwa mita 25 kutoka lango la Chelsea,
mkwaju ambao kipa wa Chelsea, Petr Cech, hakuweza kuuzuia.
"Nina furaha sana kwa ajili ya timu
yangu na kocha wangu. Ilikuwa siku maalumu sana kwake katika uhasama
wake wa kihistoria na hasimu wake Mourihno," amesema Frank Ribery baada
ya kuinua kikombe hicho. "Tulikuwa na bahati leo. Nadhani ushindi huu
utatusaidia na utatupatia motisha zaidi," akaongeza kusema Ribery.
Kiungo wa Chelsea, Ramires, alitolewa
uwanjani dakika ya 85 kwa kuonyeshwa kadi nyekundu baada ya kumfanyia
madhambi Mario Goetze wa Bayern. Hata hivyo vijana 10 wa Jose Mourinho
walifunga bao la pili dakika ya tatu ya kipindi cha kwanza cha muda wa
ziada kupitia Mbelgiji Eden Hazard. Hazard aliwachenga walinzi wawili wa
Bayern katika wingi ya kushoto na kuvurumisha mkwaju uliopita mikono ya
mlinda lango wa Bayern, Manuel Neuer, na kuutikisa wavu. Timu ya Pep
Guardiola iliendelea kukidhibiti kindumbwendumbwe hicho, kama
ilivyofanya wakati ilipokuwa ikiongozwa na kocha wa zamani, Jupp
Heynckes, katika fainali ya Champions League miezi 15 iliyopita, lakini
juhudi zao za kufunga mabao zilikwamishwa na kipa wa Chelsea, Petr Cech,
aliyekuwa macho sana kila mara akiokoa mabao ambayo yalikuwa yaingie
wavuni.
Ilionekana kana kwamba Chelsea
wangeshinda mpambano huo kwa mabao 2-1, hadi pale Javi Martinez wa
Bayern, aliposawazisha sekunde chache tu kabla kipyenga cha mwisho
kupulizwa kumaliza kipindi cha mwisho cha muda wa ziada. "Wanachukua
kikombe lakini timu bora imeshindwa. Wapinzani wetu wamefunga magoli
mawili na sisi pia tumefunga mawili. Lakini wamefunga penalti moja zaidi
kuliko sisi. Ni wazi kabisa timu bora imepoteza mechi hii," amesema
kocha wa Chelsea, Jose Mourinho, wakati wa mahojiano yake na Sky Sports.
"Kwangu mimi tulikuwa timu bora zaidi.
Bayern walikuwa na dakika 15 katika kipindi cha pili ambazo walitawala
mchezo na kuudhibiti mpira, lakini licha ya kuwa na wachezaji 10,
tulicheza vizuri sana. Tumecheza dhidi ya mabingwa wa Ulaya na wachezaji
wangu walikuwa timu bora - tuna sababu za kujivunia kuamini katika siku
zijazo. Napendelea kusema tu kwamba timu bora imeshindwa na nitabaki na
msimamo huo," akaongeza kusema Mourinho.
Akifurahia ushindi wake wa nane dhidi
ya Mourinho katika michuano 16 iliyopita, Pep Guardiola amempongeza
mtangulizi wake, Jupp Heynckes, aliyeiongoza Bayern kushinda mataji
matatu msimu uliopita. "Nataka kumshukuru Jupp Heynckes kwa fursa ya
kucheza katika fainali hii. Ni kwa sababu ya bidii yake kwamba tuko
hapa."
Maoni na hisia tofauti
Guardiola ametofautiana na msimamo wa
Mourinho kwamba timu bora imepoteza mechi hiyo. "Naamini timu bora ndiyo
iliyoshinda. Sisi tulitengeneza nafasi nyingi za kufunga magoli.
Chelsea ina wachezaji wenye uzoefu mkubwa kama vile Petr Cech, Frank
Lampard, John Terry na Ashley Cole. Walikuwa na nafasi zao, lakini
tulistahili kushinda." amesema kocha huyo wa Bayern.
Wakati huo huo, mlinda lango wa
Chelsea, Petr Cech, amesema, "Tulitaka sana kushinda kombe hili na wao
pia walitaka. Walilitafuta bao la kusawazisha na sisi tulikuwa
tukiwazuia na kuimarisha kwa bidii safu yetu ya ulinzi. Inauma sana
jinsi walivyofaulu kukomboa." Cech ameongeza kusema, "Kila mtu
anaichukulia Bayern kama timu yenye nafasi nzuri ya kushinda Champions
League msimu huu na kama timu bora duniani wakati huu, lakini
tumeonyesha umahiri mkubwa, wakati mambo yalipokuwa yakituendea kombo."
Ni mchuano wa kwanza kuwania Super Cup
kutochezwa Monte Carlo tangu mwaka 1997 na bila shaka ndio umekuwa wa
kusisimua zaidi na wenye kumbukumbu nyingi kuliko michuano mingine yote.
Pia ni fainali ya kwanza ya Super Cup ambapo mshindi amepatikana
kupitia penalti.
No comments:
Post a Comment