JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limemkamata
Alquine Claud (42) mkazi wa Yombo Buza wilayani Temeke kwa tuhuma za kujifanya
ofisa Usalama wa Taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,
Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova alisema kuwa baada ya mtuhumiwa
kuhojiwa alikiri kuwa hakuwa mfanyakazi wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Kova alisema kuwa siku ya tukio mtuhumiwa alikamatwa na
vielelezo mbalimbali ikiwemo bastola aina browning yenye namba A.956188-CZ83
ikiwa na risasi 12 ndani ya magazine.
Kwamba alipopekuliwa nyumbani kwake alikutwa na bastola nyingine
aina ya Maknov yenye namba BA4799 ikiwa na risasi 19 pamoja na kitabu cha
mmiliki silaha hiyo chenye namba CAR 0007168 na jina la P.1827 LT COL Mohamedi
Ambari, kitambulisho cha JWTZ No.7001-E. 1075.
Mbali na vielelezo hivyo, mtuhumiwa alikutwa na nyaraka
mbalimbali zikiwemo za Ikulu pamoja na mihuri ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP)
na vyeti bandia vya shule.
Katika tukio jingine, jeshi hilo linawashikilia watu saba
wanaodaiwa kuwa ni majambazi wakiwa na silaha, sare za polisi na simu za upepo.
Kova alisema tukio hilo lilitokea saa tatu asubuhi eneo la
Kiluvya wilayani Kinondoni ambako watuhumiwa walikuwa wakitumia gari lenye
namba za usajili T 546 BWR Toyota Cresta GX100 yenye rangi nyeupe.
Alisema baada ya watuhumiwa hao kuona wamezingirwa, walianza
kufyatua risasi hewani, lakini polisi walipambana na kuwakamata.
Endelea kusoma habri hii kwa kubofya hapa chini
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Khamis Mkalikwa (40) mkazi wa
Mbagala, Magira Werema (31) mkazi wa Mabibo na Nurdini Bakari (46) mkazi wa
Temeke.
Wengine ni Materu Marko (32) mkazi wa Mbweni, Louis Omagoda (34)
mkazi wa Kimara Kona, Amosi Enorck (23) mkazi wa Tegete Kibaoni na Amiri
Mohamedi (45) mkazi wa Magomeni Mikumi.
Kova alisema baada ya kukamatwa watuhumiwa hao walikutwa na
bastola moja aina ya Brown B.3901 ambayo ilikuwa na risasi nne na ganda moja la
risasi, sare za polisi pea mbili za cheo cha station surgeant (major), moja ya
pea ikiwa ina beji inayosomeka kwa jina la SSGT A. M. Mduvike.
Watuhumiwa hao wanaendelea kushikiliwa kwa mahojiano huku
wengine wawili wakipelekwa hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu baada ya
kujeruhiwa sehemu za miguu wakati wakikamatwa.
TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment