MJUMBE wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar na aliyekuwa mwakilishi wa
Jimbo la Kiembe Samaki kupitia CCM, Mansour Yussuf Himid, ambaye
anaonekana kugeuka kuwa shujaa visiwani hapa kutokana na msimamo wake wa
kutaka mamlaka kamili ya Zanzibar, ameibuka na kutangaza kujitoa kwenye
siasa. Mansour alitoa msimamo huo jana, baada ya kuwa kimya kwa
takribani wiki moja, tangu avuliwe uanachama na Halmashauri Kuu (NEC) ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM), iliyoketi Dodoma hivi karibuni.
Mansour, ambaye anajulikana kwa msimamo wake huo tangu mwaka 2011 na hivyo kupata ushujaa kutoka kwa wapenda mabadiliko, alitoa kauli hiyo wakati akizungumza kwenye kongamano la kamati hiyo, lililokuwa likijadili Rasimu ya Katiba Mpya, katika ukumbi wa Bwawani, mjini hapa.
Sanjari na hilo, alisema hatakata rufaa mahakamani kupinga uamuzi huo, kwa kuwa alichaguliwa kihalali na wananchi, hivyo hawezi kuwa mwakilishi tena kwa kutumia njia nyingine.
Alisema amejiondoa katika ulingo wa siasa akiwa amelinda heshima yake kwa kutetea haki na maslahi ya Wazanzibari.
Akizungumzia kitendo cha kuvuliwa uanachama kilichofanywa na chama hicho, alisema kinaashiria ukosefu wa ukomavu kisiasa.
Alisema CCM kimeonyesha wazi ulimwengu kuwa siasa za Tanzania zimegubikwa na ubaguzi na chuki binafsi.
Alifafanua kuwa CCM ni chama chenye historia kubwa, lakini kimetawaliwa na viongozi wasiopenda mabadiliko ya kifikra, wanaozuia uhuru na maoni ya wenzao yasiheshimiwe, hasa yakiwa yanasimamia ukweli.
“Nilichosema
juu ya Zanzibar kuwa na uhuru, mamlaka kamili na muungano wa serikali
tatu, siyo dhambi, bali nilitoa maoni yangu binafsi, hatuwezi kuvumilia
ufisadi wa kuhujumu nchi yetu wakati sisi tupo, tutaendelea kudai
mamlaka kamili.
Endelea kusoma habari hii kwa kubofya hapa chini
“Nitaendelea kusimamia ukweli huo, japokuwa viongozi wengi wa CCM hawataki niseme, sina ugomvi na chama wala sijachukizwa na uamuzi huo, kwani hayo ndiyo malipo yangu niliyotumikia kwa muda mrefu,” alisema Mansour.
Mansour alisema sababu ya kuvuliwa uanachama haifahamu, isipokuwa alisikia tetesi kuwa ni kutokana na kitendo chake cha kutamka wazi kuwa, Muungano wa Zanzibar na Tanganyika ni ubabaishaji na upo kwa maslahi binafsi, pamoja na gesi asilia kurudi mikononi mwa Zanzibar.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, NEC iliazimia kumvua uanachama Mansour, kutokana na kudaiwa kukiuka mambo matatu, ikiwemo kushindwa kutimiza malengo ya CCM na kutekeleza malengo ya uanachama.
Sababu nyingine ni kushindwa kutekeleza wajibu wa uanachama, kukiuka maadili ya uongozi, ikiwa ni pamoja na kuikana na kuisaliti Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010-2015.
Mwanasiasa huyo, ambaye amevuliwa uanachama akiwa Waziri katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), alijiunga na CCM mwaka 1977, na kushika nafasi mbalimbali za uongozi.
MTANZANIA
No comments:
Post a Comment