Taifa Stars
imemaliza vibaya mechi za mchujo za Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika
baada ya kufungwa na Gambia huku Kocha Kim Poulsen akisema timu yake
imefungwa mabao mepesi.
Wenyeji Gambia wameshinda mabao 2-0
katika mechi hiyo iliyochezwa leo (Septemba 7 mwaka huu) kwenye Uwanja
wa Independence ulioko hapa jijini Banjul ukiwa ni ushindi wake wa
kwanza katika kundi hilo la C ambapo imemaliza ikiwa ya mwisho ikiwa na
pointi nne.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Kocha
Poulsen amesema Gambia ilistahili kushinda kwa vile ilitengeneza nafasi
nyingi kuliko timu yake, na kuongeza kuwa mabao iliyopata Gambia
yalikuwa mepesi.
"Hatukutengeneza nafasi nyingi za
kufunga, lakini tukaruhusu mabao mapesi. Nawapongeza Gambia kwani
walistahili ushindi. Unapofanya makosa unaadhibiwa. Gambia ilikuwa timu
nzuri leo, kwani ilitengeneza nafasi nyingi za kufunga, sisi tukatoa
mabao mepesi," amesema Kim.
Taifa Stars inayodhaminiwa na
Kilimanjaro Premium Lager imemaliza katika nafasi ya tatu katika kundi
hilo lililokuwa na timu nne ikiwa na pointi sita ilizozipata nyumbani
kwa kuzifunga Morocco na Gambia.
Hata hivyo, Kim amesema sababu
nyingine ya kutofanya vizuri ni kuwakosa wachezaji wanaocheza nje ya
nchi na wengine wa kikosi cha kwanza ambao ni majeruhi.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Mabao yote ya Gambia katika mechi hiyo
iliyochezeshwa na Munyemana Hudu kutoka Rwanda yalifungwa na nahodha wa
timu hiyo Mustapha Jarjue. Alifunga la kwanza dakika ya 44 na kupachika
lingine dakika ya 51, mabao yaliyotokana na wachezaji wa Stars kutokuwa
makini.
Katika mechi hiyo Stars iliwakilishwa
na Juma Kaseja, Vincent Barnabas, Erasto Nyoni/David Luhende, Nadir
Haroub, Henry Joseph, Frank Domayo, Haruni Chanongo, Amri Kiemba, Mrisho
Ngasa, Simon Msuva na Khamis Mcha/Juma Liuzio.
Taifa Stars inaondoka Banjul kesho
(Septemba 8 mwaka huu) saa 6 mchana kwa ndege ya Arik hadi Dakar,
Senegal ambapo itaunganisha kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Nairobi
ambapo itawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)
keshokutwa (Septemba 9 mwaka huu) saa 8.05 mchana.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)




No comments:
Post a Comment