TAMASHA LA UTAMADUNI HANDENI NA MIPANGO KABAMBE YA KIMAENDELEO
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu, pichani.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
ILI kujenga jamii bora na yenye kujua tamaduni zao, kunahitajika kuandaliwa
matamasha muhimu yenye dhamira ya kweli katika kona mbalimbali za nchi yetu.
Huo ni mpango mzuri na wenye tija.
Katika suala hilo, wale wadau wanaotarajia au waliowahi kuandaa matamasha ya
aina hiyo ni dhahiri wanatakiwa waungwe mkono badala ya kukatishwa tamaa.
Kwa sasa, tamasha ambalo linatajwa katika vinywa vya watu wengi ni lile la
Handeni, linalotarajiwa kufanyika Desemba 14, wilayani Handeni mkoani Tanga.
Tamasha hilo la utamaduni na michezo linatambulika kwa jina la ‘Handeni
Kwetu,’ jina lililotokana na mtandao ‘blog’ ya Handeni Kwetu.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Mratibu wa Tamasha la Handeni, Kambi Mbwana, pichani.
Vyovyote litakavyotajwa na wadau wa matamasha duniani kote, ili mradi
linatimiza na kutoa majibu halisi ya namna ya kutangaza na kukuza utamaduni wa
Tanzania, si vibaya na njia ya kulitangaza mbele ya jamii.
Katika mazungumzo yaliyofanyika mapema wiki hii, mwishoni mwa wiki
iliyopita, Mratibu Mkuu wa tamasha hilo, Kambi Mbwana, anasema kuwa lengo la
kuandaa tamasha hilo ni kushirikiana na serikali na wananchi wote kujua mbinu
imara za kuutangaza utamaduni wetu.
Mbunge wa Handeni na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt Abdallah Kigoda, pichani.
Anasema kwa maeneo kama Handeni na kwingineko, kumekuwa na changamoto kubwa
za wananchi kuacha utamaduni wao na kufuata wa wenzao jambo linalotakiwa
lipingwe vikali.
“Nilikaa chini na kutafakari namna gani ya kuwaunganisha watu wote katika
tukio moja na kuwa sehemu ya wao kuangalia ngoma zetu, nyimbo zetu na mbinu za
kijamii kwa ujumla wake.
“Naamini katika umri wa taifa letu la Tanzania, kuna mengi yametokea na
yaliwahi kutokea hasa wakati wa ukoloni, hivyo naamini siku hiyo tutajua ni
kiasi gani watu wa asili ya Handeni walikuwa na mchango kwenye jamii yao,”
alisema Mbwana.
Mbwana ambaye ni mwandishi wa habari na mmiliki wa ‘blog’ ya Handeni Kwetu
(www.handenikwetu.blogspot), anasema kwamba kwa kukutana watu wote ni sehemu ya
kuangalia namna ya kulitumikia taifa letu la Tanzania na kubuni mbinu za
kujikomboa kiuchumi.
Mdau huyo wa mambo ya utamaduni, michezo na sanaa kwa ujumla wake ukiwamo
muziki, anasema kwamba Handeni ni miongoni mwa wilaya zenye changamoto kubwa
hivyo kuna haja ya wadau wote kukutana kwa pamoja na kuangalia namna ya
kuzitatua, hasa kwa kupitia tamasha hilo.
“Huu si wakati wa kuangalia Mkuu wa Wilaya (DC) Muhingo Rweyemamu anafanya
nini au Mbunge Abdallah Kigoda na viongozi wote wa serikali, ila jambo la
muhimu ni kushirikiana nao kuleta maendeleo.
“Mtu wa kwanza katika maendeleo ni mwananchi mwenyewe, hivyo naomba
kuwakaribisha Watanzania na hata wale wasiokuwa Watanzania kukutana pamoja na
sisi kwenye tamasha hili,” alisisitiza Mbwana.
Aidha, Mbwana anatumia muda huo kuwaomba wadau wote, wakiwamo viongozi wa
serikali, mashirika na kampuni kujitokeza kudhamini tamasha hilo litakalokuwa
la aina yake.
Tamasha la Utamaduni la Handeni Kwetu linafanyika kwa mara ya kwanza,
likipangwa kuanza saa tatu asubuhi hadi saa 12 jioni, ambapo vikundi mbalimbali
vya sanaa vitashiriki.
Ili kuleta hali ya kimkoa, Mbwana anasema juhudi zinafanyika kupata vikundi
katika baadhi ya wilaya za Mkoa wa Tanga ili kuimba nao, kucheza nao na
kushiriki nao katika jambo la kimaendeleo.
Mdau huyo wa habari anasema kwamba hadi sasa wadau kadhaa wamejitokeza
kudhamini tamasha hilo linalotikisa katika maeneo ya Handeni na Tanzania kwa
ujumla.
Anawataja wadau hao kuwa ni pamoja na Yusuphed Mhandeni, ambaye ni Mchumi wa
CCM Kata ya Makumbusho kwa kupitia Kampuni yake ya Yusuphed Trans, yenye magari
yanayotoka Dar es Salaam kwenda Mkata, wilayani Handeni, Grace Products, Screen
Masters na mtandao wao wa Saluti5.com, Dullah Tiles & Construction Ltd,
Katomu Solar Specialist, Country Business Directory (CBD) na Michuzi Media
Group.
Wengine ni duka la mavazi la Chichi Local Ware, Smart Mind & Arters
chini ya Anesa Company Ltd, ikidhamini kwa kupitia kitabu chao cha ‘Ni Wakati
Wako wa Kung’aa’, Lukaza Blog, Kajunason Blog, Jiachie Blog na Taifa Letu.com.
Mbwana anasema kwamba kwa kupitia tamasha hili, wadau wote watapata fursa ya
kutangaza biashara zao, ukizingatia kuwa tamasha hili linatarajia kukutanisha
watu wengi zaidi sehemu moja.
“Tunaomba udhamini kwa watu wote ili tushirikiane katika kufanikisha tamasha
hili la kihistoria, huku tukiamini kuwa wenzetu wa Kilindi, Korogwe tutakuwa
nao pamoja.
“Maandalizi yanaendelea kuhakikisha kuwa tunafanya kitu cha tofauti katika
tamasha hilo, nikiamini kuwa mguso huu utaendelea kushika kasi na habari hizi
njema kuenea nchini kote,” alisema.
Mbwana anasema kwamba wazo la kufanyika kwa tamasha hilo limepewa baraka na
viongozi wote, akiwamo DC Rweyemamu na Mbunge, Abdalah Kigoda, ambaye pia ni
Waziri wa Viwanda na Biashara.
Anasema kuwa kwa kufanyika kwa tamasha hili ni muendelezo wa mipango mingi
mizuri ya kimaendeleo itakayoandaliwa kwa kushirikiana na Watanzania wote,
hususan wananchi wa Handeni.
Mwisho kabisa Mbwana alitumia muda huo kuwakumbusha wafanyabiashara
mbalimbali wilayani Handeni na Tanga kwa ujumla, kuingia moja kwa moja katika
tamasha hili la aina yake.
Post a Comment