![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEguXAhb7FmpM11rurOlQ_6pWXedfrqYlhsslhJFng7G6vH3YyDbPfO53zNHhnSDqDptEMgINOk6mbYSe9yOb6cRii8d97oxopBcJZ25WJwszl4XQm3azoHZW2pm8ujO5p64q1pmzKkFNJRI/s640/jk%252Bbungeni%252Bpx.jpg)
Rais Jakaya Kikwete akilihutubia Bunge.PICHA|MAKTABA
Dodoma:Rais Jakaya Kikwete amesema Tanzania haitajitoa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), licha kuwapo kwa vitendo alivyoviita vya ubaguzi vinavyofanywa na wakuu wa nchi za Uganda, Kenya na Rwanda.
Rais Kikwete akilihutubia Bunge jana mjini Dodoma
alifichua kwamba sababu kubwa ya viongozi hao kuonekana kama wanaitenga
Tanzania ni msimamo wake kuhusu masuala ya Shirikisho la Kisiasa,
Uhamiaji, Ardhi na Ajira.
Rais alikuwa akirejea matukio ya hivi karibuni ya
marais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, Uganda, Yoweri Museveni na Rais wa
Rwanda, Paul Kagame kukutana na kujadiliana kuhusu masuala kadhaa
yanayohusu EAC bila Tanzania kuwapo.
“Hatuna mpango wa kuondoka, tupo na tunaendelea
kuwepo na napenda niwahakikishie kwamba Tanzania haijafanya jambo lolote
baya kwa jumuiya yetu au kwa nchi mwanachama mmoja mmoja na tumekuwa
waaminifu na watiifu kwa jumuiya wakati wote,”alisema Rais Kikwete.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Aliwashutumu viongozi wao akisema kuwa kauli zao
kwamba wanakutana kwa sababu wako tayari ni za kibaguzi kwani katika
mikutano yote waliyoifanya Entebbe nchini Uganda, Mombasa – Kenya na
Kigali nchini Rwanda hawakuwahi kuialika Tanzania.
“Hali hii haijawahi kuwapo na ni kwa mara ya
kwanza tunaanza kuwa na makundi ndani ya jumuiya yetu; huku Kenya,
Uganda na Rwanda, kule Tanzania na Burundi,”alisema Kikwete katika
hotuba yake iliyochukua saa1:15 na kuongeza:
“Ikiwa itakuja kutokea jumuiya ikadhoofika au
ikafa, Mungu apishilie mbali Tanzania isije ikanyooshewa kidole kwamba
ndiyo chanzo cha kudhoofika huko au kufa huko”.
Alisema ataendelea kuzungumza na viongozi wa nchi
hizo, na kwamba tayari ameanza ili kuhakikisha utekezaji wa mambo yote
ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki unafanywa kwa kuzingatia mkataba
ulioanzisha jumuiya hiyo.
Rais Kikwete alisema kwa mujibu wa mkataba huo
mambo yote yanapaswa kutekelezwa kwa kuzingatia kalenda ambayo inaweka
bayana mambo hayo kuwa ni Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja, Umoja wa
Sarafu na hatimaye Shirikisho la Kisiasa.
Alisema licha ya kuwapo kwa mambo hayo kwenye
mkataba ambao umesainiwa na nchi wanachama, Kenya, Uganda na Rwanda
wamechukua baadhi ya mambo ambayo kimsingi ni ya jumuiya na kuanza
kuyaweka chini ya himaya yao.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni Umoja wa Forodha na
Shirikisho la Kisiasa ambayo taarifa zake zilipaswa kuwasilishwa katika
Mkutano wa Wakuu wa Nchi uliopangwa kufanyika Kampala, Uganda, Novemba
30 mwaka huu.
Kuhusu Umoja wa Forodha, Rais Kikwete alisema
walikubaliana kwamba bidhaa zitozwe ushuru pale zinapoingizwa tu na
baadaye kuwepo utaratibu wa nchi iliyotoza ushuru husika kwenda katika
nchi ambayo bidhaa hizo zinapelekwa, lakini kabla ya utekelezaji
waliwaagiza mawaziri kuandaa utaratibu mwafaka.
Shirikisho la Kisiasa
Kuhusu Shirikisho la Kisiasa, alisema nchi wanachama katika
mkutano wa Novemba 30 mwaka jana walikubaliana kwamba lifanyiwe kazi na
kwamba taarifa yake pia inapaswa kuwasilishwa katika mkutano wa Kampala.
“Na maagizo yetu katika mkutano wa 15 wa wakuu wa
nchi utakaofanyika Novemba 30 mwaka huu mjini Kampala taarifa hiyo
itolewe na uamuzi ufanyike, hata hivyo, tunashangaa wenzetu katika mambo
waliyokubaliana wanataka kuanza mara moja, wanaanza kwa utaratibu
upi?,”alihoji.
Kuhusu Shirikisho la Afrika Mashariki, Rais
Kikwete alisema katika mkutano wa 14 wa Novemba 30 mwaka 2012 jijini
Nairobi, walipokea taarifa ya hatua iliyofikiwa kuhusiana na kuanzishwa
kwa Shirikisho la Afrika Mashariki.
“Mkutano kujadiliana zaidi kuhusiana na mpango
kazi wa kufikia shirikisho la kisiasa na mpango wa kufikia mambo
mengine, kukawa na timu ya watalaamu na inategemewa Baraza la Mawaziri
litawasilisha mpango huo katika mkutano ujao;
“Kwa kweli unajiuliza hadi unachoka, wenzetu hawa wamekosa imani na jumuiya?
Wanataka kuunda yao ama wanaichukia nchi yetu? Na hivyo wameamua kutufanyia vitimbi tutoke au sijui wanachuki na mimi,”alisema.
Shirikisho la Kisiasa
Rais Kikwete alitumia muda mwingi kufafanua suala
la Shirikisho la Kisiasa akisema hatua hiyo kama inavyoonekana kwenye
mkataba ni ya mwisho na inapaswa iridhiwe na nchi wanachama kwa kura ya
maoni.
“Sisi tuna uzoefu maana tumekuwa na muungano kwa
miaka 50, tumewaambia mara nyingi wenzetu kwamba jamani, ili kufikia
katika ngazi hiyo lazima kwanza tujenge uchumi wetu maana huo ndio
msingi imara wa kuwa na shirikisho,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Tunataka shirikisho lijengwe kwenye msingi imara
baada ya kuwapo na mtangamano wa kiuchumi, tukifanya hivyo tutakuwa
tumefanya kazi nzuri kwa manufaa ya nchi wanachama na wananchi katika
katika nchi zetu, msukumo haupaswi kuwa shirikisho la kisiasa”.
Alisema msukumo wa kutaka kuharakishwa kwa hatua
hiyo ndani ya EAC haujaanza leo kwani 2001 iliundwa tume ya aliyekuwa
Mwanasheria Mkuu wa Kenya, Amos Wako ambayo iliweka wazi hisia za
Watanzania katika masuala ya msingi ndani ya jumuiya hiyo.
Alisema 2006 wakati hoja ya kutaka kuharakishwa
kwa shirikisho ilipoibuliwa tena, Tanzania iliunda tume iliyoongozwa na
Profesa Samuel Wangwe na matokeo yake yalionyesha kuwa asilimia 74 ya
Watanzania walikuwa wakitaka kuwapo shirikisho, lakini kati yao ni
asilimia 24 tu waliotaka kuharakishwa kwake.
Mambo yasiyo ya EAC
“Kwa hiyo sisi tunatekeleza matakwa na uamuzi wa Watanzania kwa
Serikali yao ambao walitaka tutekeleza mambo haya kwa hatua, msimamo huu
uko wazi na tumekuwa tukiusema katika vikao halali na siyo kwa kificho
hata kidogo,”alisisitiza.
Kuhusu tuhuma kwamba Tanzania imekuwa kikwazo cha
utekelezaji wa mipango ya EAC, Rais Kikwete alikanusha akisema siyo
kweli kwani ushiriki wake umewezesha kutekelezwa kwa mipango mingi
ikiwamo ya ujenzi wa mtandao wa barabara katika nchi wanachama.
“Tuhuma hizo hazina mashiko maana mtu mwenye akili
timamu huwezi kulipa ada ya Dola milioni 12 za Marekani kila mwaka,
maana tunalipa halafu tukawa watu wa kukwaza jumuiya, haiwezekani hata
kidogo,”alisema Kikwete.
Mambo yasiyo ya EAC
Rais Kikwete alisema Tanzania haikuwa na tatizo na
baadhi ya mambo ambayo nchi hizo zimeyafanya na miongoni mwake ni
matumizi ya vitambulisho vya Taifa kama hati ya kusafiria na viza ya
pamoja ya utalii.
“Tuliamua kwa pamoja nchi wanachama waliokuwa
tayari waanze. Waliposema tutumie vitambulisho vya Taifa kama hati ya
kusafiria badala ya hati ya kusafiria tukasema sisi Tanzania bado
hatunavyo,” alisema.
Alisema Tanzania haijafanya jambo lolote dhidi ya jumuiya au nchi yoyote mwanachama na kwamba kama kuna ushahidi waseme.
“Sisi ni wanachama waaminifu na watiifu kwa
jumuiya, tunatimiza ipasavyo kwa jumuiya na kushiriki ipasavyo katika
kuijenga,”alisema.
Alisema sababu ya nchi tatu zilizopo katika jumuiya hiyo kufanya mambo peke yao bila kuishirikisha Tanzania hayaeleweki.
MWANANCHI
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment