Mazingira duni ya kujifunzia kama ilivyo katika darasa hili la shule
moja ya msingi katika Kijiji cha Lula Kawala, mkoani Rukwa, yanatajwa
kuwa chanzo cha wanafunzi kushindwa kujifunza ipasavyo stadi za kusoma,
kuhesabu na kuandika. Picha ya Maktaba
Nje ya darasa la pili katika Shule ya Msingi Ilala iliyopo Manispaa ya Iringa, baadhi ya wanafunzi wanamsimanga mwenzao mmoja kwa kumwita mtoro.
Nje ya darasa la pili katika Shule ya Msingi Ilala iliyopo Manispaa ya Iringa, baadhi ya wanafunzi wanamsimanga mwenzao mmoja kwa kumwita mtoro.
Mmoja anapaza sauti na kusema: “Sharafi hajui
kusoma’’ Ni kweli Sharafi (jina siyo lake) anayesoma darasa la pili
shuleni hapo, anaelezwa na mwalimu wake kuwa hajui kusoma na pia ni
mtoro aliyekubuhu, japo mwenyewe anakana kuwa siku hizi siyo mtoro tena.
Mwalimu wake Esther Sanga, anasema baadhi ya
wanafunzi darasani mwake wana matatizo ya kutokujua kusoma licha ya kuwa
hivi karibuni watamaliza darasa la pili, akiwamo Sharafi anayesema
anaweza kukaa hata mwezi mmoja hajaonekana shuleni.
Tukiwa darasani namwomba mwalimu huyo tumjaribu
Sharafi kujua uwezo wake wa kusoma. Tunamwandikia ubaoni neno ‘baba’,
kwa sekunde zisizozidi 10 analisoma na kulipatia. Kisha tunamwandikia
neno ‘iba’, akachukua sekunde zaidi kulisoma na kulipatia.
Neno lingine lilikuwa ‘bobu’. Hapa Sharafi
anatafakari zaidi huku akilikazia macho neno hilo. Baada ya sekunde
nyingi kupita anafanikiwa kulisoma kwa usahihi japo anaonyesha
kutokujiamini na alichokisoma.
ENDELEA KUSOA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Darasa analosoma lina watoto karibu 40 ambao licha
ya kubakiwa na muda mchache kujiunga na darasa la tatu, bado hawajaweza
kusoma kwa ufasaha hasa herufi mwambatano,
Mwalimu Sanga anasema wanafunzi hao wanasoma,
lakini kwa kile anachokiita usomaji wa kudonoadonoa. Anasema: ‘’ Hawa
wanasoma kwa kudonoadonoa, hawasomi kwa mfululizo na sababu ni kwamba
wako wengi darasani na walikosa walimu wenye ujuzi.’’
Bila shaka wanafunzi hawa ni ushahidi wa kuwapo
wanafunzi wengi wanaovuka darasa la pili wakiwa hawajui kusoma, kuandika
na kuhesabu, maarufu kwa kifupi cha KKK au K3
Ilivyo mfumo wa elimu wa Tanzania, unamtarajia
mtoto akimaliza darasa la pili awe ana uelewa mkubwa wa stadi hizo
-muhimu katika mchakato wa ujifunzaji.
Kisa cha Shule ya Msingi Ilala kinashadadiwa na
matokeo ya utafiti uliofanywa mwaka 2010 na Uwezo Tanzania, na kubaini
mwanafunzi mmoja kati ya watano wanaohitimu elimu ya msingi, hajui
kusoma japo hadithi ya kiwango cha darasa la pili.
Utafiti huo ulioitwa ‘ Je watoto wetu
wanajifunza? Ulihusisha sampuli ya watoto 42,033 kutoka kaya 22,800
katika wilaya mbalimbali nchini. Watoto hao walipimwa uwezo wa kusoma na
kuhesabu.
Sababu za kutojua kusoma
Walimu katika Shule ya Msingi Ilala wanasema sababu kuu
inayochangia wanafunzi kufika darasa la pili bila kujua kusoma ni
kubadilishwa kwa utaratibu wa ufundishaji wa masomo katika madarasa ya
chini.
Wanasema zamani msisitizo ulikuwa kuwafundisha
watoto hao stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu pekee. Lakini sasa
wanafunzi hao wamebebeshwa mzigo wa masomo yapatayo sita.
Wanataja masomo hayo kuwa ni pamoja na Hisabati,
Lugha ya Kiswahili, Lugha ya Kiingereza, Sayansi, Stadi za kazi na Haiba
na Michezo. Kinachosikitisha ni kuwa wakati orodha ya masomo
ikiongezeka, ufundishaji wa K3 umekosa msisitizo katika shule nyingi.
“Zamani tulijua kusoma, leo kuna masomo mengi,
zamani ilikuwa ni kusoma, kuandika na kuhesabu. Nashauri darasa la
kwanza na la pili wafundishwe K3 kisha masomo mengine yaendelee madarasa
ya juu,’’ anasema mwalimu Tumaini Mungule.
Sababu nyingine ni wingi wa wanafunzi darasani.
Wanasema hata kama K3 pekee zitafundishwa tena na walimu mahiri,
haitosaidia kama madarasa yataendelea kuwa na mrundikano wa wanafunzi
kama ilivyo sasa katika shule nyingi za umma.
“ Kwa shule za mjini idadi ya wanafunzi ni 100, 90
au 80 wakiwa na mwalimu mmoja. Kuwamudu wote haiwezekani, baadhi kama
10 au 15 utawaacha nyuma,’’ anaeleza mwalimu Imelda Ibobo anayefundisha
darasa la pili katika Shule ya Msingi Mapinduzi mkoani Iringa.
Anaungwa mkono na Mratibu wa Tathmini ya Uwezo
Tanzania kwa Wilaya ya Iringa Mjini, Ellen Binagi anayesema mbali ya
wanafunzi hao kuwa wengi, bado mazingira ya madarasa mengi ni duni
katika utoaji wa taaluma.
“Sasa hivi wanasukumwa tu bora liende. Darasani
watoto wako kama utitiri na wamekaa chini, mwaka huu kuna swali
linauliza asilimia ngapi ya wanafunzi wanakaa chini,’’ anaeleza.
Uwezo inayosimamiwa na asasi isiyo ya kiserikali
ya Twaweza, kwa miaka kadhaa sasa imekuwa ikiendesha tafiti zinazolenga
kupima uwezo wa kusoma na kuhesabu kwa wanafunzi wa umri wa miaka saba
hadi 16.
Utoro nao unachangia
Ni dhahiri mtoto asiyehudhuria masomo tangu akiwa
madarasa ya chini, ana uwezekano mkubwa wa kutojua kusoma asiposimamiwa
barabara. Tafiti na uzoefu vinaonyesha utoro ni moja ya sababu kuu
zinazochangia watoto kutojua kusoma, kuandika na kuhesabu.
Kwa Shule ya Msingi Ilala mfano mzuri wa hoja ya
utoro ni mwanafunzi Sharafi anayeelezwa kutoroka hata kwa muda wa mwezi
mzima. Uwezo mdogo darasani unaosababishwa na utoro umemfanya aendelee
kubaki darasa la pili badala ya darasa la tatu.
Hata hivyo, mwenyewe anasema sababu za kuwa mtoro hasa siku za
nyuma ni kuchoshwa na adha ya kutembea umbali mrefu kwenda shuleni na
kurudi. Zamani alikuwa anaishi eneo la Ikonongo ambalo ni zaidi ya
kilomita tatu kutoka shuleni.
“Zamani nilikuwa naishi mbali, nilikuwa nakuja
siku moja nyingine siji. Wazazi waliponiuliza kama nakuja shule nilisema
nakuja,’’ anasema Sharafi ambaye tofauti na maelezo ya mwalimu wake,
anadai amebadilika na kuwa mtoto mwema.
Ukiondoa utoro walimu, wazazi na wadau wengine wa
elimu wanasema mambo mengine yanayochangia tatizo hili ni ukosefu wa
walimu hasa kwa shule zilizopo vijijini na baadhi ya wanafunzi kuwa na
matatizo binafsi kama uwezo mdogo wa akili unaosababishwa na magonjwa na
mambo mengine.
Wazazi wanasemaje?
Mzazi na mkazi wa Mtaa wa Dabodabo katika Manispaa
ya Iringa, Hashim Mori anasema kwa shule za mjini zenye walimu, hali
hiyo inaweza kusababishwa na wanafunzi wenyewe kwa kuwa watoro au
walimu kutowajibika.
“Walimu hawawajibiki ipasavyo, kwa sababu wizara
na ofisa elimu hawawafuatilii, ‘’anasema na kuongeza kuwa kudorora kwa
elimu katika shule za umma kunasababishwa pia na viongozi kukosa
uchungu kwa kuwa hawana watoto wanasoma katika shule hizo.
Kwa upande wake, mzazi Asha Rajabu anasema walimu
wasitupiwe mzigo wa lawama, bali wa kulaumiwa ni wazazi anaosema
hawawajibiki ipasavyo kwa watoto wao.
“Mzazi hamfuatilii mwanawe akirudi shule na wala
hashirikiani na walimu. Walimu wana mbinu nyingi. Siku za nyuma
mwanangu hakuwa anaandika nilipomkagua, nikapiga simu kwa mwalimu na
kugundua hakuwa anahudhuria shule, tukaweka mkakati wa
kumdhibiti,’’anasema .
Hali mbaya
Ni dhahiri kuwa hali syo nzuri katika shule nyingi
nchini, ukitoa ripoti ya Uwezo Serikali imeshakiri kuwepo kwa idadi
kubwa ya wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika katika shule za msingi.
Cha ajabu wapo wanaofikia hatua ya kumaliza shule na hata kuchaguliwa
kuingia kidato cha kwanza.
Kwa mfano, April mwaka jana, Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi ilitangaza kuwabaini wanafunzi 5,200 waliokuwa kidato
cha kwanza katika shule mbalimbali nchi nzima lakini hawakujua kusoma
wala kuandika.
““Hili ndilo janga la kitaifa sasa. Lazima
tujiulize kwa nini watoto wanamaliza darasa la saba wakiwa hawajui
kusoma wala kuandika na halafu wanafaulu? ‘’ alisema Naibu Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo kama alivyonukuliwa na Mwananchi siku za nyuma.
Tatizo la dunia
Hali ikiwa mbaya kwa shule za Tanzania , huku
kiwango cha watu wazima wasiojua kusoma na kuandika nacho kikiongezeka
nchini kwa asilimia nane kuanzia mwaka 1990. Ripoti ya kimataifa ya hivi
karibuni inasema dunia ina watu 774 milioni wasiojua kusoma na
kuandika.
Aidha, ripoti hiyo iliyotolewa Septemba mwaka huu
na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco),
inasema mbumbumbu wengi wapo katika nchi za mabara ya Afrika na Asia.
Kwa Tanzania takwimu zinaonyesha kuwa kumbukumbu
zinaonyesha hadi mwishoni mwa mwaka 2002, watu wasiojua kusoma walikuwa
milioni sita na laki mbili.
MWANANCHI
MWANANCHI




No comments:
Post a Comment