Mkuu wa Dawati la Jinsia Nkasi, CPL-Anna
Kisimba (kushoto) akipitia kitabu cha orodha ya matukio ya dawati hilo.
Kulia ni msaidizi wake.
Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri wa Wilaya ya Nkasi, Oscar Mdenye
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
JESHI
la Polisi Wilaya ya Nkasi kupitia dawati la Jinsia na Watoto,
linamshikilia Pius Jacob Mkazi wa Kijiji cha Chala kwa kosa la kuoa mtu
na dada yake, ambapo mdogo mtu alikuwa ni mwanafunzi wa darasa la tano
katika Shule ya Msingi Kabwe wilayani Nkasi.
Jacob alikamatwa na Polisi wa Dawati
la Jinsia na watoto Kituo cha Nkasi ikiwa ni wiki moja tangu amchukue
kwa nguvu binti huyo wa darasa la tano (umri miaka 12) na kuja kuishi
naye kama mke na mume huku akiwa tayari amemuoa binti mwingine wa kwanza
mwenye umri wa miaka 16 ambaye pia ni dada wa binti wa pili.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa
Dawati la Jinsia Nkasi, CPL-Anna Kisimba alisema walimfuatilia Jacob na
kumkamata baada ya wao kupewa taarifa na mmoja wa majirani wa mtuhumiwa
kuwa alikuwa akiishi kinyumba na wanafunzi hao.
"...Tulikuwa katika ziara zetu za
kawaida zilizoambatana na siku 16 za kupinga ukatili tukizunguka baadhi
ya vijiji vya wilaya yetu, ndipo raia wema walituarifu kuwepo kwa tukio
hilo na kuanza kufuatilia hatimaye kumkamata mtuhumiwa," alisema
Kisimba.
Tayari mtuhumiwa huyo amefikishwa
mahakamani kwa mara ya kwanza Desenba 10, 2013 kwa kosa la kumuoa
mwanafunzi na kubaka katika Mahakama ya Wilaya ya Nkasi, Mkoa wa Rukwa
kujibu mashtaka ya tuhuma zake.
Akizungumzia tukio hilo, Ofisa Ustawi
wa Jamii wa Halmashauri wa Wilaya ya Nkasi, Oscar Mdenye alisema baada
ya kufuatilia zaidi wamebaini hata binti (16) aliyemuoa wa kwanza
alikuwa ni mwanafunzi haijulikani alitumia mbinu gani za kumpata na
kuanza kuishi naye kama mke na mume.
Aidha ameongeza kuwa kwa mujibu wa
tarifa ambazo walizipata kutoka kwa majirani inadaiwa binti wa pili
alimpata kwa kutumia nguvu na vitisho, kwani alimfuata nyumbani kwao na
kudai anakuja kuwasalimia lakini baada ya kufika kwake alimjulisha binti
huyo kuanzia sasa wewe ni mke wangu na kuanza kuishi naye.
"...Hadi Polisi na Ofisi ya Ustawi wa
Jamii tunafikiwa na taarifa hizo inadaiwa mtuhumiwa huyu alikuwa tayari
ameishi na binti huyu wa pili kwa wiki nzima nyumbani kwake, na majirani
walijua baada ya binti wa pili (12) kuanza kulalamika kwao kuwa alikuwa
amechukuliwa kwa nguvu na kulazimishwa kuolewa," alisema Mdenye.
Juhudi za kumpata mtuhumiwa
kuzungumzia tuhuma zake hazikuweza kuzaa matunda baada ya kuwa mahabusu
akisubiri mwenendo wa kesi yake inayomkabili.
Hata hivyo matukio ya ukatili
yanayoripotiwa polisi kupitia Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Nkasi
yamekuwa yakipungua kutoka mwaka hadi mwaka, kwani kwa mujibu wa
takwimu za dawati hilo kwa mwaka 2012 kulikuwa na kesi 224 za ukatili
zilizoripotiwa, ilhali kwa mwaka 2013 jumla ya kesi 143 zimeripotiwa
wilayani hapo.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa ushirikiano na TAMWA





No comments:
Post a Comment