Katibu
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willbroad
Slaa, amelaani kitendo cha Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo cha kukumbatia wawekezaji wa nje katika rasilimali ya gesi na
kuwanyima wawekezaji wa ndani.
Amesema waziri huyo anataka kuwagawia wazungu vitalu vya gesi ili
wachimbe mabomba kuisafirisha Ulaya badala ya kusambaza nchini itumike
kama nishati kuwaletea wananchi maendeleo.
Alisema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha
Mwangoye jimbo la Bukene wilayani Nzega mkoani Tabora katika ziara yake
ya kutembelea mikoa ya Kigoma, Tabora na Singida.
"Waziri Muhongo amekuwa muongo kama jina lake lilivyo, anasema
Watanzania hatuwezi kuwekeza kwenye miradi mikubwa kama ya gesi, uwezo
wetu ni kutengeneza juisi na maji, mimi nasema kama hatuwezi basi gesi
hiyo ikae ardhini hadi tutakapokuwa na uwezo," alisema.
Alisema waziri Muhongo amefikia hatua ya kuwagawa Watanzania katika
ardhi yao kwa kutoa rasilimali zao kwa wazungu jambo ambalo ni hatari.
Aliongeza kuwa waziri huyo anapenda waje wazungu kutoa nje wachukue ardhi ya Tanzania ili Watanzania waachwe na kukaa pembeni.
Dk. Slaa ambaye wakati akizungumzia suala hilo alikuwa
akishangiliwa na mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano huo alisema,
Mwalimu Nyerere alishawahi kusema madini yakikaa chini ya ardhi
hayawezi kuoza kama ndizi.
Alisema kama Watanzania hawana uwezo na utaalam wa kuchimba gesi
iachwe chini ya ardhi ili watoto wasomee na kuichima wenyewe kunufaisha
watanzania wote badala ya wazungu anaowang’angania Waziri Muhongo.
Dk. Slaa alisema Waziri Muhongo na serikali yake wanataka kuwagawia
wazungu ambao lengo lao la kutengeneza mabomba kutokea Mtwara
kupitishia chini ya ardhi ili wauze Ulaya kabla Watanzania hawajanufaika
nayo.
Alisema badala ya kutengeneza mabomba kwa ajii ya kuuza gesi Ulaya
kuna haja kwa serikali ikajenga mabomba kila kijiji iweze kutumika na
Watanzania wote.
Alisema Watanzania kama watachangia hata kama ni shilingi moja na
kuunda kampuni wataweza kupata fedha za kuchimba gesi yao na ndiyo maana
ya kujenga nchi.
“Mengi amekuwa akitetea rasilimali ya gesi kama mwenyekiti wa PSPF
kwa hiyo ametanguliwa na wafanyabiashara wa Tanzania na hivyo
hakuzungumza suala hilo kama Mengi mwenyewe,” alisema Dk. Slaa.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI




No comments:
Post a Comment