Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Dar/mikoani. Watu wa kada mbalimbali wameupongeza uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wa mawaziri wanne waliotajwa kushindwa kusimamia vizuri utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili, huku wakimtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda naye kufuata nyayo hizo.
Wasomi na wanasiasa hao waliozungumza na gazeti
hili mbali na kupongeza hatua hiyo, wamesema tatizo linaloikabili nchi
ni kuwa na mfumo mbovu wa utawala hivyo kupendekeza wote waliohusika
kuchukuliwa hatua za kisheria na siyo kuhukumiwa mawaziri pekee.
Juzi ripoti ya Kamati ya Maliasili, Ardhi na
Mazingira iliwasilishwa bungeni na Mwenyekiti wake, James Lembeli na
kuwang’oa mawaziri hao kutokana na kushindwa kusimamia vizuri
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Waziri Mkuu Pinda alilitangazia bunge kuwa Rais
Jakaya Kikwete ametengua uteuzi wao, baada ya kuwasiliana naye kwa
mashauriano akiwa nchini Marekani kwa matibabu.
Mawaziri waliong’olewa kutokana na ripoti ya
kamati hiyo iliyoongezewa shinikizo na michango ya wabunge wengi ni
Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamisi Kagasheki, Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi,
Dk Mathayo David Mathayo.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Waziri wa kwanza kutangaza kujiuzulu alikuwa ni
Kagasheki huku uamuzi wa mawaziri watatu kujiuzulu ukitangazwa na Waziri
Mkuu Mizengo Pinda.
Katibu Mkuu wa (Chadema) Dk Willbrod Slaa
akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mwangoye na Bukene wilayani Nzega
mkoani Tabora, alisema kuondolewa kwa mawaziri hao haitoshi kwani
anayepaswa kujiuzulu ni waziri mkuu kutokana na kuruhusu Polisi na
vyombo vingine vya dola kuwapiga watu, kauli ambayo aliitoa bungeni.
“Wala msilindane kama ripoti ya kamati imebainisha
unyama huu, basi wasiishie kwa hao mawaziri wanne, waziri mkuu naye
anapaswa kupima na kujiuzulu, kwani hii itasaidia pia kuwaondoa mawaziri
wengine ambao wamekuwa wakielezwa na CCM kuwa ni mzigo,” alibainisha Dk
Slaa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki
za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo-Bisimba alisema, kung’olewa kwa
mawaziri hao hakutoshi bali hata Waziri Mkuu Pinda naye awajibike.
“Hao mawaziri wameng’olewa kutokana na wizara zao
kukosea, lakini Waziri Mkuu Pinda ndiye msimamizi wa kazi za Serikali,
kama wizara zimekosea na yeye amekosea hivyo awajibike mwenyewe na kama
atagoma basi mkuu wake amwajibishe kwani ameshindwa kuwasimamia mawaziri
wake,” alisema Dk Bisimba.
Aliongeza: “Pinda angeweza kupona endapo
angechukua hatua mapema za kuwawajibisha hao mawaziri pindi taarifa
alipozipata za uteswaji, ubakaji, mauaji ya wananchi wasiokuwa na hatia
na si kusubiri hadi Bunge lichachamae. Hapa Serikali yake imevurunda,
naye aondoke.”
Dk Bisimba alisema; “Mawaziri sawa wameng’olewa
lakini watendaji wote waliohusika wachukuliwe hatua, ikiwemo
kufunguliwa mashtaka mahakamani kutokana na kusababisha vifo, mateso na
majeraha kwa watu na mifugo.”
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa George Shumbusho
alisema; “Waziri Mkuu naye anatakiwa kuondoka kwani yeye ndiye kiongozi
wa shughuli za Serikali na kilichotokea kilikuwa chini yake.”
Aliongeza; “Ngoja tuone labda alifikiri akijiuzulu
wakati Rais hayupo anaweza kuiweka nchi katika matatizo hivyo ngoja
tusubiri itakuwaje.”
Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Samwel
Ruhuza alisema; “Nadhani Baraza zima la mawaziri linatakiwa kumulikwa
maana operesheni hii ilipitishwa na mawaziri wote, sasa iweje wawajibike
wanne tu.”
Alisema ni jambo la kushangaza kutokea kwa matukio
ya kutisha katika operesheni hiyo bila vyombo vya ulinzi na usalama vya
mikoa na wilaya kubaini lolote. “Inaonekana kama waliotekeleza
operesheni hii walijipanga na walijua jambo wanalokwenda kulifanya,”
aliongeza.
Aliongeza; “Bunge limefanya kazi yake lakini jambo
kubwa ambalo linatakiwa kufanyika ni kuhakikisha kuwa wote waliohusika
kutekeleza operesheni hiyo wanachukuliwa hatua, ikiwa ni pamoja na
kufikishwa katika vyombo vya sheria.”
Mkazi wa Mji mdogo wa Mirerani, wilayani Simanjiro
mkoani Manyara, Gulam Obela alimpongeza Waziri Kagasheki kwa kujiuzulu,
ila alisikitishwa na Dk Mathayo, Dk Nchimbi na Nahodha waliosubiri
kuondolewa na Rais Kikwete.
“Nampongeza Kagasheki kwani amefuata nyayo za
Edward Lowassa ambaye yeye alijiuzulu kutokana na makosa ya viongozi wa
chini yake, sasa Kagasheki japo hakushiriki unyama wa Operesheni
Tokomeza Ujangili lakini amejiuzulu kwa ridhaa yake,” alisema Obela.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa
Chris Peter Maina alisema; “Ni jambo zuri kuona utaratibu uliokuwepo
miaka ya nyuma wa viongozi na watendaji wa Serikali kujiuzuru unarejea.”
Profesa Maina ambaye kitaaluma ni mwanasheria
alisema miaka ya 1970, Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi wakati
huo akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alijiuzulu kutokana na
kukithiri kwa matukio ya kuuawa kwa watu waliokuwa wakidhaniwa kuwa ni
wachawi.
“Siyo Mwinyi tu, hata aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa
Mwanza, Peter Kisumo na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Marko
Mabara pamoja na Waziri wa Nchi anayeshughulikia Usalama, Peter
Siyovelwa walijiuzulu. Mawaziri hawa wanne wamefanya vyema kuonyesha
uwajibikaji kwa makosa yaliyofanywa na waliopo chini yao” alisema Maina.
Mhadhiri mwingine wa chuo hicho, Bashiru Ally
alikuwa na mtazamo tofauti kuhusu hatua hiyo kwa maelezo kuwa jambo
kubwa linalotakiwa kutazamwa ni mfumo wa utawala.
“Kama utakumbuka sakata la Richmond watu
walijiuzulu, sakata la akina Jairo na hata vurugu zilizotokea mkoani
Mtwara kupinga gesi kutoka nje ya mkoa huo,” alisema na kuongeza;
“Matukio hayo yote bunge liliunda Kamati ambazo zilitoa ripoti,
lakini kuna ripoti ambazo hazijawekwa wazi na hata kama zimewekwa wazi
mapendekezo yake hayajatekelezwa hadi leo hii,” alisema.
Bashiru alitolea mfano Wizara ya Maliasili na
Utalii kuwa kwa kipindi kifupi imekuwa na mawaziri watatu tofauti,
lakini wote wameondoka kwa mtindo unaofanana jambo ambalo linaonyesha
kuwa tatizo ni mfumo.
“Bunge linatakiwa kutazama jambo hili kwa kina ili
kuepuka kutumiwa kisiasa, ndani ya miaka 10 Bunge letu limekuwa na
maspika wawili ambao wameunda kamati nyingi za kuchunguza mambo
mbalimbali, lakini bado ripoti hatuzioni na hata utekelezaji hakuna,”
alisema.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa
Ibrahim Lipumba, alisema kitendo hicho ni matokeo ya watendaji wa
Serikali, hususani vyombo vya dola kukosa uadilifu.
Alisema operesheni hiyo badala ya kutokomeza ujangili, imefanya kazi ya kutokomeza wananchi kwa kuwatesa na kuwanyanyasa.
Aliongeza kuwa Rais Kikwete anapaswa kutafakari juu ya utendaji kazi wa mawaziri, kwa kuwa wengi wanaonekana kuwa mzigo.
“Ukweli utabaki kuwa Rais anapaswa kuangalia
watendaji wake, mawaziri wengi ni mzigo wakiongozwa na Waziri wa
Tamisemi (Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa-Tamisemi) na Waziri wa Elimu, ”alisema Lipumba.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha
Mapinduzi (UVCCM) wa Mkoa wa Manyara, Regina Ndege alisema;
“Nimewasikiliza baadhi yao wakizungumzia kuhusu hilo sidhani kama kuna
tatizo hiyo ni sehemu ya uwajibikiaji unapoona wengi wanakulalamikia
unapofanya kazi siyo wote watapongeza tatizo kubwa ni mawasiliano ya
utekelezaji wa ile operesheni.”
Katibu wa Chadema Wilaya ya Simanjiro, Frank
Oleleshwa alisema huo ni uthibitisho wa wazi kabisa kuwa Rais Kikwete
amekuwa akiteua watendaji wabovu na dhaifu kwani haiwezekani kila wakati
viongozi wabovu wanapewa nafasi ya kuongoza.
Mwasisi wa Chadema, Edwin Mtei alisema kuwa
operesheni hiyo iliacha makovu mengi hususan kwa raia ambao ni wanyonge
hapa nchini na kushangaa hatua kutochukuliwa mapema kwa watu
kutowajibishwa.
“Kila siku nilikuwa naomba kwa Mungu kuhusu hawa
viongozi wabovu nashukuru salamu zangu zimesikika hatimaye yametimia,
Crime does not pay(uhalifu haulipi) ipo siku ukweli utajulikana tu,”
alisema Mtei.
Imeandaliwa na Ibrahim Yamola, Fidelis
Butahe, Elizabeth Edward, (Dar), Frederick Katulanda (Tabora), Joseph
Lyimo (Manyara)na Moses Mashalla (Arusha)
MWANANCHI
MWANANCHI



No comments:
Post a Comment