TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Baada ya kupokea barua yake ya mashtaka 11 tarehe 01/12/2013 ambayo anashitakiwa nayo na iliyomtaka ajitetee kwa maandishi.
Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe (MB) jana tarehe 10/12/2013 amefanya hivyo kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Uendeshaji za Chama Pia
Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe (MB) ametoa taarifa kwa Katibu Mkuu wa
Chama kumueleza nia yake kukata rufaa Baraza Kuu la Chama kupinga hatua
iliyochukuliwa na Kamati Kuu dhidi yake kumvua nyadhifa zake ndani ya
Chama.
Kuna sababu mbili za msingi za kukata rufaa;
1. Utaratibu wa kuchukua hatua za nidhamu ulikiukwa.
2. Sababu za kuchukuliwa hatua hizo sio sahihi.
Utaratibu ambao unatakiwa kufuatwa kabla ya kumchukulia hatua za
kinidhamu kiongozi kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Uendeshaji ni kama
ifuatavyo;
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Kanuni ya Uendeshaji 6.5.6 inasema;
Kiongozi yeyote hatachukuliwa hatua za kinidhamu bila kwanza kupewa
mashitaka yake kwa maandishi na mamlaka husika na kupewa nafasi ya
kujibu mashitaka kwa maandishi.
Pia tunapenda ijulikane kwamba Kanuni ya Uendeshaji 6.5.2 (a), (b), © na (d) kama ilivyorekebiswa Januari 2013 inasema; Kwa
mujibu wa ibara ya 5.4.3 na 5.4.4 ya Katiba mwanachama yeyote
hatachukuliwa hatua za kinidhamu ama kuonywa ama kuachishwa ama
kufukuzwa uanachama bila kwanza;
a) Kujulishwa makosa yake kwa maandishi na kutakiwa kutoa majibu katika muda usiopungua wiki mbili.
b) Kupewa nafasi ya kujitetea mbele ya kikao kinachohusika.
c) Mwanachama atajulishwa kwa maandishi uamuzi wa kikao mnamo wiki mbili baada ya kusikilizwa.
d) Kamati Kuu inaweza kuchukua hatua za dharura bila kuzingatia
utaratibu (b), © hapo juu kama itaona maslahi ya Chama kwa ujumla
yanaweza kuathiriwa isipokuwa mwanachama au kiongozi anayelalamikiwa
atalazimika kuitwa kwenye kikao husika.
Naomba nichukue fursa hii kufafanua kuwa uongozi wa chama ulifanya
mkutano na waandishi mnamo tarehe 26/11/2013 na kusema kwamba
marekebisho haya ya Kanuni ya mwaka 2013 ambayo nimewawekea hapo juu,
ndiyo utaratibu waliofuata.
Pia walieleza kuwa sikuwa naifahamu na nilidanganywa kwani Kanuni ilishabadilishwa.
Mabadiliko haya ambayo ni katika kipengele (d) kuhusu hatua ya dharura
iliyochukuliwa na Kamati Kuu haikugusa kipengele (a) cha Kanuni. Yaani
ni kuwa hata kama Kamati kuu itachukua hatua ya dharura kwa mujibu wa
kipengele (d), bado kipengele (a) ni lazima ifuatwe na inatamka wazi
sharti la kiongozi kupewa mashtaka kwa maandishi na kupewa nafasi ya
kujibu kwa maandishi. Hii ni haki ya msingi kwa kila utawala au uongozi.
Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe hakupewa mashtaka yake aliyakuta ndani ya
kikao baada ya kupewa taarifa kwa ujumbe wa simu (text message au sms).
Kwa uzito wa makosa hayo yaliyosababisha kuvuliwa uongozi na kwa
kuangalia athari zake kwake yeye binafsi na chama kwa ujumla, Kamati Kuu
ilitakiwa kujiridhisha kwamba Kanuni za Uendeshaji na Katiba
zinafuatwa.
Hili linaendana na utaratibu uliotumika kwa Samson Mwigamba kuvuliwa
nyadhifa yake ya uenyekiti wa mkoa. Yeye hakuitwa kabisa kwenye kikao
hicho na ni ukiukwaji wa Kanuni ya Uendeshaji 6.5.6(d) niliyoisoma hapo
juu kwamba lazima kiongozi huyo aitwe kwenye kikao.
Sababu zilizotumika ingawaje hajapokea taarifa rasmi ya maandishi kwa
mujibu wa Kanuni za Uendeshaji ni kwamba yeye ameshirki kwenye kuandaa
na kusambaza waraka ambao unasemekana ni mkakati wa ushindi wenye lengo
la kupindua uongozi uliopo.
Waraka huo haukumtaja Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe kama muandaaji au msambazaji. Waliouandaa hawajaukana na badala yake wamesema waziwazi kabisa kwa maneno na maandishi kwamba Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe HAHUSIKI.
Sio sawa kumuadhibu Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe kwa hisia au tu kwa sababu ya urafiki wake na watu fulani. Haya
ni mapungufu ambayo kwa bahati nzuri Katiba na Kanuni za Uendeshaji
zinatoa nafasi ya kurekebishwa kwa kutoa nafasi ya kukata rufaa. Na
utaratibu ni huu hapa;
Kwa ufupi, Ibara 6.3.6(d) ya Katiba ya Chama;
“Kiongozi aliyechukuliwa hatua za kinidhamu na mamlaka yake ya nidhamu
anayo haki ya kukata rufaa ngazi ya juu ya ile mamlaka yake ya nidhamu
na uamuzi wa ngazi hiyo utakuwa wa mwisho”.
Ibara 6.3.6(e) ya Katiba ya Chama;
“Rufaa yoyote lazima ifanyike katika muda wa siku thelathini tangu
tarehe ya kupokea rasmi kwa maandishi maamuzi ya mamlaka iliyotoa
adhabu”.
Kanuni za Uendeshaji zinatoa UTARATIBU ambao unatakiwa ufuatwe ili
kiongozi aliyeadhibiwa aweze kutumia HAKI yake ya kukata rufani kwa
maneno haya;
Kanuni ya 6.5.8 ya Kanuni za Uendeshaji;
“Kiongozi aliyeadhibiwa atapewa taarifa ya msingi wa maamuzi ya mamlaka ya nidhamu ili kumuwezesha kuamua kukata rufani au la”
Kanuni ya 6.5.9 ya Kanuni za Uendeshaji;
“Mwadhibiwa atakayeamua kukata
rufani atatakiwa kufanya hivyo katika muda wa siku thelathini baada ya
kuarifiwa uamuzi wa adhabu”
Kanuni ya 6.5.10 ya Kanuni za Uendeshaji;
“Baada ya kutoa uamuzi kikao husika kinalazimika kuandaa taarifa kamili
ya mwenendo wa shauri na kuwasilisha ngazi ya juu. Taarifa hiyo lazima
ifike katika muda wa siku kumi na nne baada ya kikao cha mamuzi”
Mpaka hivi sasa hatujapokea taarifa kamili ya mwenendo wa shauri tokea kikao cha Kamati Kuu cha tarehe 20-21/11/2013
Huo ndio utaratibu ambao Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe ameamua kufuata
kwa kuheshimu maamuzi ya Kamati Kuu lakini kukatia rufaa maamuzi hayo.
Kuheshimu maamuzi sio kuyakubali uhalali wake.
Kumekuwa na matukio ya kusikitisha
ambayo mengine yamefikia mahali kuwa fujo na vurugu ikiwa ni pamoja na
kurushiwa mawe Katibu Mkuu wa Chama. Vurugu hizo baadhi zimehusishwa na
Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe na baadhi ya watu.
Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe hahusiki kwa njia yoyote na hayo
yanayoendelea na anayakemea na kuwashauriwanachama wote kuwa watulivu
na kuendelea kuwaheshimuviongozi wa kitaifa. Hatua zimeshachukuliwa
kukata rufaa na niimani yake kwamba Baraza Kuu la Chama litatenda haki
kwakupitia rufaa yake na kutoa uamuzi.
Nawashukuru wote.
ALBERT MSANDO,
Mwanasheria
No comments:
Post a Comment