Nilipofikiria kuandika makala kuhusu uwezo wa kushawishi watu wengine wakubaliane na mawazo yetu niliingiwa na shaka kuwa huenda baadhi ya watu wasione umuhimu wa mtu kuwa na stadi kama hizo. Iwapo wewe ni miongoni mwa watu wenye fikra hizi, jiulize kama unaweza kuishi bila kuongea na watu, Je, huwa haitokei ukamweleza mtu au watu mawazo ambayo ungependelea wayaelewe na kuafikiana na wewe.
Katika maisha yetu ya kila siku tunatoa maelezo mbalimbali ili kueleza maoni, fikra ama hisia zetu. Mara nyingine wale tunaoongea nao huwa na mawazo tofauti na yetu. Hakika hufurahi sana tunapofanikiwa kuwashawishi hadi wakaafikiana na mawazo yetu. Kuna matukio ambayo hutufanya tuone ni muhimu sana kuweza kushawisha watu wakubaliane na mawazo yetu. Matukio hayo ni kama tunapokwenda kwenye ofisi mbalimbali tukiwa na mahitaji kama vile kiwanja cha kujenga nyumba, nafasi za watoto shuleni, kuunganisha huduma ya maji au umeme katika nyumba, kuomba mkopo au kazi na maombi mengine .
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Ushawishi huweza kuwa muhimu zaidi tunapowaeleza watoto wafuate maadili, tunapomweleza bosi uzito wa kazi na nakuomba nyongeza ya mshahara, tunapotoa maelezo katika mashauri mahakama au tunapowapatanisha ndugu au jamaa waliohitilafiana na kukosana. Kuna watu wasiyo na uwezo kabisa wa kushawishi. Hivyo, badala ya kunasihi, wao hutumia mbinu ya kukaripia au kufoka. Ushawishi wa namna hii huwa siyo wa hiari wala kudumu. Watu wenye uwezo mkubwa wa kushawishi huwa na haiba kubwa katika maisha. Lakini kila mmoja wetu unaweza kujifunza jinsi ya kushawishi. Wanafalsafa wamefanya utafiti na kugundua kuwa uwezo wa kushawishi huweza kujengeka kwa kuzingatia mbinu sita zifuatazo:-
Kutumia ushawishi katika sehemu uliyozoea
Watu wenye uhodari wa kushawishi huweza kufanya shughuli hiyo katika mazingira waliyoyazoea. Kanuni hii hutumika katika utawala. Mameneja hufanya vikao na watendaji wao katika ofisi zao. Kama unaongea na mtu au kundi ambalo lina sehemu yake na kama haiwezekani kuzungumzia katika sehemu yako ni vyema zaidi kukutana katika sehemu isiyo yenu wote.
Kuonekana nadhifu
Kuna watu wanao amini kuwa tunapomsikiliza mtu akiongea huwa tunavutiwa zaidi na kile anachosema kuliko anavyoonekana. Jambo hili siyo kweli. Utafiti umeonyesha kuwa watu huvutiwa zaidi na muonekano wa msemaji kuliko maneno anayosema. Hii ndiyo maana hata mavazi wanayovaa viongozi wa dini huwasaidia kuongeza ushawishi wa maneno wanayosema kwa waumini wao. Tunaposhawishi inafaa tuwe nadhifu.
Kujinasibisha na wale tunaowashawishi
Imebainika kuwa unapokuwa ukijaribu kumshawishi mtu huna budi kumfanya akuone wewe siyo tofauti na yeye na kwamba unamthamini yeye na mawazo yake. Ni vyema ujenge hoja yako kuanzia kwenye fikra au mawazo yake.
Kuzingatia uelewa na uzoefu wa unayemshawishi
Watu wenye uzoefu wa kushawishi huzingatia welewa na uzoefu wa mtu au watu anaokusudia kuwashawishi. Huna budi kuelewa upeo wa welewa wa mtu unayekusudia kumshawishi ili uweze kumshawishi vizuri zaidi. Huna budi kuanzia hoja yako kwenye kiwango cha unayemshawishi na kumchukua taratibu hadi kwenye mawazo yako.
Ni vyema kukumbuka kuwa usipoweza kumweleza mtu au watu kwa kuzingatia upeo wa welewa wake utakuwa umefanya kazi bure. Fikiri jinsi wazazi wanavyopata shida ya kuwaeleza watoto wadogo mahali watoto wanakotoka.
Kila mara wamezoea kusema watoto wananunuliwa sokoni au wanaokotwa porini. Nakumbuka kuna mtoto mdogo alimuuliza mama yake mbona tumbo la shangazi limekuwa kubwa, kwa sababu mama alijua shangazi akijifungua ataonekana ana mtoto, akamjibu mtoto
“Katika tumbo la shangazi yako kuna katoto kazuri” Yule mtoto akamuuliza mama yake “Kama ni katoto kazuri kwa nini shangazi alikameza.” Hizi zote ni jitihada za kuweza kupata maelezo yatakayolingana na uwezo wa kuelewa wa mtoto
Tumia hoja za maarifa badala ya hoja ya fikira au mawazo yako
Unapotaka kumshawishi mtu akubaliane na wazo lako huna budi kutumia maarifa ya kweli badala kutoa hoja zinazoonekana kama hisia au mawazo yako tu.
Daima hakikisha unatumia maelezo yenye ushahidi unakubalika. Maprofesa hutumia ushahidi wa maarifa yaliyoandikwa katika vitabu na wataalamu waliobobea katika fani mbalimbali. Viongozi wa dini nao hutumia maneno yaliyoandikwa katika misahafu ya dini. Maneno yanayonukuliwa kutoka kwa wabobezi na katika vitabu vitukufu hutumika kama hoja zenye nguvu zinazosaidia kushawishi.
Tumia hadithi au mifano ya matukio halisi
Hakuna kitu chenye nguvu ya kushawishi kama hadithi au mifano ya matukio ya kweli. Vitu hivi huwa na nguvu ya kushawishi zaidi kuliko maelezo yanayofafanua maarifa au dhana fulani. Hebu fikiria watu wawili waliokuwa wakiuza magari yao walivyotofautiana katika kuyatangaza. Mmoja alielezea ubora wa gari yake kwa kutumia maelezo ya yaliyowekwa na watengenezaji kwenye kitabu cha gari.
Maelezo hayo yalikuwa kama vile jinsi gari linavyotumia mafuta kidogo, jinsi linavyokwenda kasi na kutulia barabarani bila kuyumba. Mwingine alieleza ubora wa gari yake kwa kusema alijaza mafuta kwenye tanki akaenda hadi Tanga na kurudi bila kuongeza mengine.
Alieleza kwamba alitumia saa chache kwa sababu gari lake lilikuwa linakwenda haraka kuliko magari mengine mengi. Pia kwa kuwa gari lake haliyumbi hata kwenye kona nyingi aliweza kwenda kasi bila kuyumba hivyo alitumia muda mfupi sana.
Huyu wa pili anaweza kuuza kwa urahisi kwa sababu anatoa mifano halisi ya jinsi gari inavyoweza kutumika.
Haya niliyoyataja ni baadhi ya mambo ambayo mtu aliyatumia yatamsaidia kuhamasisha watu wengine waafikiane na mawazo yake. Zamani watu waliamini kuwa mtu hawezi kujifunza jinsi ya kushawishi watu kwa sababu ni kipaji anachozaliwa nacho mtu. Lakini utafiti umedhihirisha kuwa uwezo wa kushawishi unatokana na baadhi ya stadi za mawasiliano ambazo mtu anaweza kujifunza mwenyewe kama nilivyoeleza katika makala hii.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment