HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» »Unlabelled » MAWAZIRI, VIGOGO WAFANYA KUFURU

 
Waziri wa Ujenzi, John Magufuli akisisitiza jambo fulani siku za hivi karibuni, yeye ndiye  mwenye dhamana na nyumba za Serikali. Picha na Maktaba 
Dar es Salaam . Viongozi wa Serikali wakiwamo mawaziri, wameingia kwenye kashfa inayowaweka katika wakati mgumu, baada ya kubadili matumizi ya nyumba za Serikali walizonunua, kinyume na mikataba inavyoeleza.
Nyumba hizo ambazo zilianza kuuzwa mwaka 2002 enzi ya utawala wa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ziliuzwa kwa mawaziri, makatibu wakuu na watumishi wengine wa ngazi mbalimbali za umma.
Mikataba ya kisheria ya ununuzi wa nyumba za Serikali inaeleza kuwa, mfanyakazi wa Serikali anaponunua au kukopeshwa nyumba, hatakiwi kubadili matumizi au kuuza hadi baada ya miaka 25 kupita.
 ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Kwa mujibu wa mkataba wa mauziano kifungu Na 9 na 10, mtumishi aliyeuziwa nyumba au mrithi wake haruhusiwi kuiuza nyumba hiyo mpaka hapo itakapotimia miaka ishirini na mitano (25), kuanzia tarehe ya hatimiliki.
Gazeti hili lilimtafuta Waziri wa Ujenzi, John Magufuli mwenye dhamana na nyumba za Serikali kwa muda wa miezi miwili kutoa ufafanuzi wa suala hilo bila mafanikio, huku akitoa sababu mbalimbali kwa mwandishi kukwepa kuzungumzia suala hilo.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Injinia Gerson Lwenge alisema kuwa anahitaji kupata ripoti kamili kutoka kwa Wakala wa Nyumba za Serikali (TBA), ili ajionee mikataba na afahamu ni wapi ilipovunjwa.
“Serikali ina nia nzuri kabisa kuwauzia watumishi wake nyumba, lakini kama kuna mikataba inakiukwa, basi TBA inafahamu kwa kina ni kwa vipi watu hao wachukuliwe hatua,” alisema.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa, viongozi wengi ambao nyumba zao zipo katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Mwanza wamezibadili matumizi na kuwa za biashara.
Kwa Jiji la Dar es Salaam baadhi ya nyumba zilizouzwa kwa vigogo hao wa Serikali na kubadilishwa matumizi zipo katika maeneo ya Oysterbay.
Gazeti hili lilishuhudia baadhi ya nyumba hizo zikiwa zimebadilishwa matumizi na kuwa klabu za starehe, kupangishwa taasisi au balozi, huku nyingine zikiwa tayari zimeuzwa.
Moja ya nyumba hizo ni ya aliyewahi kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Muungano, Mohamed Seif Khatib, iliyopo Oysterbay, Mtaa wa Bongoyo katika Barabara ya Hillpark. Nyumba hiyo kwa sasa imevunjwa na kujengwa klabu na baa iitwayo Ocasa.
Alipoulizwa kuhusu nyumba hiyo na mkataba wake unavyosema, Khatib alisema kwamba hajavunja sheria yoyote kwa sababu hajauza nyumba hiyo.

Alifafanua kuwa yeye amebadili matumizi sehemu ndogo ya nyumba hiyo huku akimtaka mwandishi aandike tu kuhusu sehemu kubwa na siyo mabadiliko aliyodai ni madogo.
“Nyie waandishi ndivyo mlivyo, kwa nini msiandike mazuri yetu. Mnapenda kuandika mambo mabaya tu, mnataka tuishi kimaskini. Nyumba imejengwa tangu enzi za ukoloni, mnataka mpaka leo ibaki hivyohivyo?” alihoji.
Eneo la Kinondoni, palipokuwa na nyumba ya aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Afya katika Serikali ya Rais Kikwete, nayo kwa sasa imevunjwa na kujengwa ghorofa, huku kibao cha mkandarasi kikionyesha kuwa ujenzi wa jengo la biashara unaendelea.
Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili umeonyesha kuwa nyumba nyingine za viongozi wa Serikali zilizobadilishwa matumizi zipo eneo la Msasani na Masaki.
Nyumba nyingine iliyobadilishwa matumizi inamilikiwa na waziri mmoja eneo la Barabara ya Hindu, Kinondoni mkabala na Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, ambayo imebadilishwa na kujengwa nyumba za kupangisha watu.
Mjini Arusha baadhi ya nyumba za Serikali zilizouzwa na kubadilishwa matumizi zipo eneo la Uzunguni.
Moja ya nyumba hizo ipo karibu na Ikulu ndogo mjini humo, ambayo hivi sasa imebadilishwa na kuwa baa. Nyumba hiyo ipo Mtaa wa Haile Selassie.
Katika Jiji la Mwanza, nyumba zilizobadilishwa matumizi zipo katika eneo la Isamilo na Kapiripointi.
Historia ya nyumba za Serikali
Nyumba za watumishi wa Serikali zilianza kujengwa na watawala wa Kijerumani na Waingereza. Nyumba hizo ambazo sasa idadi yake inakadiriwa kufikia 10,000 ni za daraja la tatu, pili na la kwanza, kulingana na nyadhifa za watumishi wa Serikali.
Sababu za kuuza nyumba hizo hazikuwekwa bayana, lakini maelezo mengine yanaonyesha kuwa hatua hiyo imefikiwa ili kuwasaidia watumishi wa Serikali kuwa na nyumba. Hata hivyo, maelezo mengine yanaonyesha kwamba nyumba hizo ziliuzwa kwa kuwa ni mzigo kwa Serikali.
Hadi kufikia mwaka 2012, nyumba za Serikali zilizouzwa kwa watumishi wa umma ni 6,000.

Wakala wa Majengo
Mkurugenzi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Elius Mwakalinga alisema kuwa kuna masharti ya nyumba za Serikali ambayo miongoni mwake ni kutobadili matumizi na kutohamisha mali hiyo hadi baada ya miaka 25.
Mwakalinga alisema pia kwamba mfanyakazi wa umma hatatakiwa kuhamisha mali hiyo wala hatimiliki kwa mtu wa tatu na iwapo atahitaji kufanya ukarabati, basi atatakiwa kuomba kibali.
“Kama kweli kuna watu wanaofanya ujanja katika hilo, hata kama ni viongozi, watashughulikiwa kulingana na sheria,” alisema Mwakalinga.
Waziri Lwenge
Akizungumzia zaidi suala hilo, Naibu Waziri Lwenge alihoji maswali kadhaa, ikiwamo sababu za watumishi kubadili nyumba hizo na kuzifanya klabu au maeneo ya biashara na wakapewa ruhusa na mamlaka ya mipango miji. Hata hivyo, alisisitiza kuwa hajaifahamu kwa kina mikataba hiyo inasema nini.
Lwenge alisema kwamba wizara yake itaketi na wanasheria wake na kuangalia upya mikataba hiyo, ili iwapo kuna vipengele vyenye upungufu virekebishwe.
“Inawezekana kuna vitu vinakosekana kwenye mikataba hiyo, au havijafafanuliwa na ndiyo maana watumishi wa Serikali wanavitumia vibaya kuvunja masharti ya mikataba yenyewe,” alisema.
Lwenge pia alisema kwamba kuna mambo mengi kwenye mikataba hiyo anayodhani yanatatiza na kuhitaji kutupiwa jicho.
Alitaja mfano wa mtumishi aliyestaafu na kuiachia nyumba hiyo familia yake, ambayo haifahamu masharti ya mikataba.
“Nia yetu ni kusaidia wafanyakazi. Ni hilo tu, hatuna jingine, lakini kama kuna upungufu kama huo ni lazima uangaliwe. Ila nashukuru kwa kuwa waandishi mnafanya kazi ya kubaini vitu kama hivi,” alisema.
Manispaa Kinondoni
Msemaji wa Manispaa ya Kinondoni, Sebastian Kaiohela alisema kuwa TBA wana kazi yao na nyumba zao na wanaifahamu mikataba ya wateja wao.
“Sina uhakika kama TBA ina nyumba maeneo ya Oysterbay, ila kwa upande wa nyumba za Serikali zinazosimamiwa na manispaa, tuna orodha ya mikataba na waliobadili matumizi,” alisema.
Ushawishi kutoka kwa wawekezaji
Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwa baadhi ya viongozi na watumishi wengine wa Serikali wamepangisha nyumba hizo kwa kampuni binafsi, baadhi kujenga maduka ya biashara na ofisi nje ya uzio wa nyumba hizo.
Ilibainika kuwa, viongozi wengi wanaomiliki nyumba hizo huingiwa tamaa ya kuziuza au kubadili matumizi kwa sababu ya ushawishi wa wawekezaji wa nje, ambao huahidi kuwalipa kiasi kikubwa cha fedha na kuzirudisha nyumba hizo baada ya miaka 20.
Septemba mwaka jana, nyumba ya Serikali iliyoko eneo la Mafiati, mjini Mbeya, yenye namba 162, Block ilipigwa mnada na Kampuni ya Udalali ya J.A Kandonga.
Nyumba hiyo inadaiwa kuuzwa kwa mfanyabiashara wa jijini Dar es Salaam kwa Sh250 milioni kutoka kwa mfanyakazi wa Serikali, Simboleo Gibson.
Mohamed Seif Khatib
Akizungumzia zaidi kuhusu nyumba aliyoinunua serikalini Khatibu ambaye pia ni Katibu wa NEC Oganaizesheni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema kwamba sehemu kubwa ya nyumba yake ameibadilisha kuwa nyumba ya kuishi na kuwa ghorofa yenye vyumba kadhaa ili iwe katika hadhi nzuri, huku pia akikiri mabadiliko katika eneo ilipo baa ya Osaka.
“Sehemu kubwa nimebadilisha kuwa makazi ya kuishi vilevile sasa kwa nini nyinyi mnataka kukuza hili jambo katika sehemu ndogo tu? Haya andika utakavyo, andika nimebadili matumizi kama unavyotaka,” alifoka Khatib.
Rais Kikwete
Rais Jakaya Kikwete, aliwahi kusema kuwa Serikali yake imefikia uamuzi wa kuzirejesha baadhi ya nyumba za Serikali zilizouzwa kwa watumishi wa umma, baada ya kubaini kwamba zilijengwa katika mazingira nyeti.
 Kikwete aliyasema hayo Ikulu Dar es Salaam alipokuwa akijibu maswali ya wahariri wakuu wa vyombo mbalimbali vya habari aliokutana nao chini ya kivuli cha utaratibu aliojipangia wa kuzungumza na wananchi kila mwishoni mwa mwezi.
“Hatukusudii kuzichukua nyumba zote…kwa mfano kuna OCD kauziwa nyumba ya OCD iliyo katika eneo la polisi, na yule OCD aliyeuziwa kahamishwa kutoka Mtwara kwenda Mafia…au kastaafu na nyumba kapangisha.Kwa kweli kuna maeneo ambayo lazima tufanye marekebisho,” alisema Kikwete.
MWANANCHI

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: