Katibu Mtendaji wa APRM, Bibi Rehema Twalib akisisitiza jambo
alipokutana na waandishi wa habari hivi karibuni.
Viongozi wa
Nchi za Kiafrika katika Makao Makuu ya AU.
Jumla ya nchi 34 kati ya 54 wanachama hai wa AU ni wanachama Mpango wa
Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM).
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Wajumbe wa
Bodi na Sekretarieti ya APRM (Tanzania) wakiwa katika picha ya pamoja na Rais
Dkt. Jakaya Kikwete. Kushoto kwa Rais ni Mwenyekiti wa APRM, Prof. Hassa Mlawa
na kulia ni Katibu Mtendaji wa APRM, Bibi Rehema Twalib.
Na Saidi Mkabakuli
Tanzania, kama zilivyo nchi nyingi duniani kwa
miaka mingi imekuwa mfuasi wa dhana ya usawa na haki ili kuwa msingi wa maendeleo ya kijamii na
kiuchumi ili kutimiza matakwa ya demokrasia.
Hali hii imeifanya Serikali kufanya jitihada
nyingi za kuboresha dhana hii licha ya changamoto nyingi zinazokinzana na
juhudi hizi za serikali.
Serikali ya Tanzania kwa kuendeleza ufuasi wake
kwa demokrasia na hasa suala zima la utawala bora, sio tu ilianzisha wizara
maalum kwa ajili ya kusimamia utawala bora pia ilijiunga na Mpango wa Kujipima
kwa kutumia vigezo vya Utawala Bora (APRM) kwa kuwasilisha rasmi maombi ya kujiunga
na mpango huu tarehe 26 Mei, 2004 na kukubaliwa rasmi tarehe 8 Julai 2004,
wakati wa Kikao cha Tano cha Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika.
APRM ni mpango wa hiari, uliobuniwa na viongozi wa
nchi za Umoja wa Afrika, kuziwezesha nchi wanachama wa Umoja wa Afrika,
kujitathmini katika utendaji wa shughuli za serikali na shughuli zao nyingine
kwa ujumla. Aidha mpango huu unalenga kuzipa nchi wanachama, fursa ya kujifunza
kutokana na uzoefu na mafanikio ya nchi zingine za Kiafrika, na hivyo
kuziwezesha nchi husika kuiga sera na mbinu muafaka zilizoleta mafanikio hayo
kwa manufaa ya nchi zao. Kwa ujumla, ombi la kufanyiwa tathmini linapofanywa,
linaashiria nchi husika kukubali kufuata misingi ya utawala bora katika
uendeshaji wa siasa na shughuli za kiuchumi na wakati huohuo, kukubali kufanyiwa
tathmini na Viongozi Wenza wa nchi za Kiafrika.
Hadi sasa nchi 34 kati ya 54 wanachama wa
Umoja wa Afrika zimejiunga na mpango wa APRM. Mpango huo unahusisha uhakiki
katika vipindi mbalimbali (periodic reviews) wa sera, kanuni na taratibu za
utendaji zilizozoeleka (practice) ili kubaini maendeleo yaliyopatikana katika
kutekeleza malengo yaliyokubaliwa katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na utawala
wa pamoja wa kibiashara kama ilivyoainishwa kwenye Tamko la Demokrasia, Siasa,
Uchumi na Utawala wa Pamoja.
Chimbuko la APRM ni Mpango Mpya wa Maendeleo ya
Afrika (New Partnership for Africa’s Development-NEPAD), ambao unalenga
kuliondoa bara la Afrika kutoka kwenye lindi la umaskini, na kuleta maendeleo.
NEPAD imeunganisha mipango ya maendeleo iliyobuniwa chini ya Umoja wa Nchi Huru
za Afrika, (OAU), na kuainisha ukosekanaji wa utawala bora kama mojawapo ya
vikwazo dhidi ya maendeleo yanayolikabili bara la Afrika. Hivyo, ili
kukabiliana na kikwazo hiki, viongozi wa nchi za Umoja wa Afrika (UA) walitoa
Tamko Kuhusu Demokrasia, Siasa, Uchumi na Uongozi Bora katika nyanja za uchumi
na mashirika ya kibiashara. Tamko hilo pia linaainisha mkakati wa kufanikisha
azma hii, kupitia demokrasia na utawala bora.
Lengo la msingi la APRM ni kuhimiza utumiaji wa
sera, viwango na miendeno inayokubalika kitaalamu ili kujenga utengamano wa
kisiasa, ukuaji chanya wa uchumi, maendeleo endelevu na kuharakisha ushirikiano
wa kiuchumi wa kikanda na hatimaye bara zima.
Pia, APRM inatoa fursa ya kuchangia katika
kudumisha utengamano, kuleta maendeleo pamoja na kuimarisha ushirikiano wa
kiuchumi kikanda kwa njia ya kubadilishana uzoefu na kuiga mifano bora ikiwa ni
pamoja na kutambua udhaifu na kutathmini mahitaji ya kuongeza uwezo wa serikali
na nchi.
Kwa kutambua
umuhimu wa utawala bora, Mipango na mikakati mingi ya kimaendeleo na ile ya
kupambana na umaskini imekuwa ikijumuisha kipengele cha utawala bora kama moja
ya misingi ya kufikia malengo. Kwa mfano, moja ya misingi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo (TDV) 2025, kati ya misingi
minne ya utekelezaji, unahimiza uimarishaji wa utawala bora na uongozi wa haki na kisheria
ikiwa ni pamoja na jamii kukataa rushwa, kuimarisha mifumo ya uongozi na
utawala ili kuweza kufikia malengo makuu ya Dira hiyo.
Pia, kwa upande wa Mkakati wa Kukuza
Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA) I&II, sifa na
misingi yake ni pamoja na Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini wa Mapato;
Kuboresha maisha ya watu na Ustawi wa Jamii; na Utawala bora na uwajibikaji.
Suala kuu la msingi linalojitokeza katika kila Mkakati
ni Utawala bora na uwajibikaji. Dhana hii ni msingi madhubuti katika kutekeleza
mikakati hii yenye mkondo wa kiuchumi na mingine mingi inayotekelezwa na
Serikali. Hivyo basi, umuhimu wa APRM katika mustakabali wa ustawi wa jamii ni
chanya, kwa kuwa nchi inapata faida ya kujitathmini pale inapokosea. Hivi karibuni Katibu Mtendaji wa Mpango huu
(APRM) nchini Tanzania, Bibi Rehema Twalib alitoa taarifa kuwa Tanzania ni moja
ya nchi zinazofanya vizuri katika utawala bora Barani Afrika.
Akizungumzia umuhimu wa APRM katika kufikia lengo
la msingi la mikakati hii, Bibi Twalib anasema kuwa ni muhimu kudumisha
utengamano, ili kuleta maendeleo pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi
kikanda kama njia ya kubadilishana uzoefu ili kuiga mifano mizuri kutoka nchi
zilizopiga hatua kiuchumi.
Kwa mujibu wa Bibi Twalib, Tanzania imepata
mafanikio katika maeneo ya Usimamizi wa Uchumi, Maendeleo ya Uchumi-Jamii
Demokrasia na Utawala Bora, Siasa, Uendeshaji wa Kampuni na Masuala Mtambuka
kama Afya.
Bibi Twalib alisema kuwa Tanzania kupitia APRM,
imefanya tathmini yake katika maeneo hayo na kuwasilisha ripoti yake mbele ya
wakuu wa nchi wanachama na kujadiliwa. Akizungumzia mikakati iliyopo katika
kuhakikisha kuwa malengo ya APRM yanakuwa chachu ya kukuza uchumi wa nchi na
kuleta maendeleo kwa jamii ya Kitanzania.
Bibi Twalib aliongeza kuwa APRM kupitia Serikali
ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania inaendelea kuendesha
tathmini ya utendaji wake na vyombo vyake kwa uwazi, ukweli na umakini,
kulingana na vigezo vilivyowekwa kwenye Mpango wa Kujipima kwa kutumia Vigezo
vya Utawala Bora.
“Kwa kutambua umuhimu katika kuimarisha utawala bora, Sekretarieti inaendelea
kutekeleza Mpango kazi wa kitaifa wa kujitathmini katika masuala ya utawala
bora (African Peer Review Mechanism - National Plan of Action, APRM-NPoA),”
aliongeza Bibi Twalib.
Kwa mujibu
wa APRM-NpoA, moja kati ya manufaa ya ya
utekelezaji wa Mpango huu ni kubaini mambo mazuri juu ya utawala bora nchini
Tanzania hali inayoongezea imani (confidence) wawekezaji toka nje ya nchi na
wabia wa maendeleo. Hili moja ya mafanikio ya APRM, maana kwa mujibu wa takwimu
kutoka Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) mpaka kufikia mwezi Desemba, 2013
kilifanikiwa kusajili miradi 9,442.
Hatahivyo, suala la kushirikisha wananchi ni suala
lisiloepukika, ambapo, Bibi Twalib anahimiza suala la nafasi ya wananchi katika
Mchakato huu. Bibi Twalib anasema kuwa, kwa kuwa APRM ina njema ya kupanua wigo
wa demokrasia, na kuwapa wananchi kauli katika maamuzi yanayohusu mustakabali
ya nchi yao.
“APRM Tanzania inategemea kuwa wananchi watatumia
kikamilifu, nafasi inayotolewa ili kutoa tathmini yao ya kweli, kuhusu yale
wanayoyaona kuwa ni mapungufu ya utendaji serikalini na mapungufu ya utawala
bora nchini kwa ujumla, ili kuiwezesha serikali nayo kuyabaini mapungufu hayo
na kuyachukulia hatua muafaka” anasihi Bibi Twalib.
Anaongeza
kuwa ikiwa wananchi watatumia vyema fursa hizi vizuri, ndipo malengo ya
kuanzishwa kwa Mchakato huu yatakapotekelezwa na kuwezesha kutimia malengo na
misingi ya mikakati ya Serikali ya kuivusha Tanzania kutoka dimbwi la umaskini.
No comments:
Post a Comment