Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, jana aliomba radhi Bunge baada ya kutoa
kauli, iliyoonesha ubaguzi kwa wabunge kutoka Zanzibar.
Kabla
ya kuomba radhi, kauli hiyo ilisababisha wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF),
kutoka nje ya Bunge kuonesha kukerwa na kauli hiyo.
Muda
mfupi baadae, wabunge hao waliungwa mkono na wabunge kutoka Bara, ambao
wanatoka Chadema na NCCR Mageuzi, ambao nao walitoka na kuwaacha wabunge
wa CCM na mbunge wa UDP, John Cheyo.
Awali
kabla ya kutoka nje, Mbunge wa Ole, Rajabu Mbarouk (CUF), aliomba muongozo wa
Spika akilalamikia kauli ya Werema wakati akimjibu Mbunge wa Mkanyageni, Habibu
Mnyaa (CUF).
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Werema
alimwambia Mnyaa kuwa mambo mengine akaulize Zanzibar na sio katika Bunge la
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuwa sio kila kitu kitaulizwa ndani ya
bunge hilo.
Hoja
ilianzia kwa Mnyaa, wakati akiomba Kamati ya Matumizi ya Bunge iliyokaa
kupitisha vifungu vya hotuba Waziri wa Katiba na Sheria kuhusu makadirio ya
mapato na matumizi ya mwaka 2014/15.
Mbunge
huyo aliituhumu Wizara ya Katiba na Sheria kuwa ni moja ya Wizara muhimu lakini
imekuwa ikivunja sheria na haki za binadamu.
Baada
ya hoja hiyo, Werema alijibu: “Alichokizungumza Mnyaa ni sahihi lakini hapa sio
mahali pake, namshauri kuwa akaulize huko Zanzibar kwenye vikao vyao hapa sisi
hatuna majibu.”
Mara
baada ya bunge kurejea, Mbunge wa Ole, Rajabu Mbarouk (CUF), aliomba mwongozo
wa Spika akitaka ufafanuzi wa kauli hiyo kwamba ilikuwa ya ubaguzi.
“Mheshimiwa
Spika, wakati wa majadiliano na wakati ambapo Mheshimiwa Mnyaa anaongea na
kutaka ufafanuzi wa haki za binadamu, huu ni ubaguzi na haupaswi kufanywa na
mtu msomi kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” alisema Mbarouk.
Hata
hivyo Spika alipinga na kusema; “hakuna mwongozo wowote kwa kuwa hata wewe
umevunja sheria kwani hata nilipokuambia kaa chini, umeendelea kuzungumza,
tunaendelea Katibu.”
Baada
ya kauli ya spika, wabunge wa Zanzibar walihamasishana na kuamua kutoka nje
wote kwa wakati mmoja na kuwaacha wabunge wenzao wa upinzani wakiendelea
kuitana na kutafakari cha kufanya.
Spika
alifafanua kuwa Mbarouk alikosea kumshutumua Spika hadharani, kwa kuwa kanuni
zinaelekeza kama amekosea, malalamiko yapelekwe katika Kamati ya Kanuni.
No comments:
Post a Comment