TAMKO LA JESHI LA POLISI MKOA WA DODOMA KUHUSIANA NA MAANDAMANO YA CHADEMA YATAKAYOFANYIKA KESHO

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishina Msaidizi wa Polisi EMMANUEL G. LUKULA (ACP) akiongea na Waandishi wa Habari ofisini kwake leo.

Na. Sylvester Onesmo wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma.
Jeshi la Polisi mkoani Dodoma limetoa tamko la kuzuia maandamano ya Chama cha CHADEMA hapo tarehe 18/09/2014 na kuwataka wananchi kuyapuuza.

Akiongea na waandishi wa habari, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishina Msaidizi wa Polisi EMMANUEL G. LUKULA (ACP) alisema kuwa; Kufuatia Viongozi wa CHADEMA kutaka kufanya maandamano kuelekea viwanja vya Ofisi za Bunge Mkoani Dodoma kwa ajili ya kupinga Bunge la Katiba siku ya tarehe 18/09/2014 linaloendelea, kuwa maandamano hayo ni batili na akiwataka wananchi wakazi wa Dodoma kuyapuuza kwa kuwa yanakiuka Sheria iliyoliweka Bunge hilo.

Kamanda LUKULA – ACP alitaja sababu za msingi za kuzuia maandamano hayo kuwa ni:-

Siku ya maandamano ya tarehe 18/09/2014 ni siku ya kazi ikiwa ni pamoja na muda wa maandamano hayo ni masaa ya kazi saa 04:00 asubuhi hadi saa 06:00 mchana yataathili ufanisi wa watu waliopo makazini/maofisini.

ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI


Bunge maalumu la Katiba linaloendelea kwa sasa lipo Kisheria na hakuna tamko lolote lililotolewa na Mahakama yoyote kulisitisha, hivyo moja ya kazi ya Jeshi la Polisi ni kulinda Sheria na wale wanaofuata sheria. Hivyo kufanya maandamano yanayopinga Bunge la Katiba ni kukiuka Sheria iliyoliweka Bunge hilo.

Kuna kesi Mahakamani ya kupinga Bunge hilo kuendelea, hadi sasa shauri hilo linaendelea Mahakamani. Hivyo kwa CHADEMA kuandamana ni kuingilia Uhuru wa Mahakama.

Baadhi ya Wilaya barua za kufanya maandamano zimechelewa kufika kwa Wakuu wa Polisi Wilaya kabla ya saa 24 kisheria.

Aidha Kamanda LUKULA – ACP alisisitiza kuwa kwa sababu hizo alitoa wito kwa wananchi wa Dodoma kupuuza maandamano yoyote ya kupinga uwepo wa Bunge la Katiba kwani ni batili. Aidha aliwashauri viongozi wa CHADEMA Mkoa na Wilaya za Dodoma wayasitishe maandamano hayo na wasipo ridhika, wakate rufaa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwa maelekezo zaidi.

No comments

Powered by Blogger.