Ndugu wasomaji wetu
tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili
tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba
+255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.
HISTORIA
inaonyesha kwamba tumbaku ilivumbuliwa na mabaharia wa Kihispania kwenye fukwe
za Marekani mwaka 1500 (BK). Kuanzia hapo, wafanyabiashara wa Kizungu
waliichukua tumbaku hiyo kutoka Marekani na kuisambaza sehemu mbalimbali
duniani walikokuwa wakifanya biashara zao.
Iliaminika kwamba
tumbaku ni zawadi kutoka kwa Mungu. Moshi wa tumbaku uliotolewa nje baada ya
kuvuta, ulidaiwa kuwa na uwezo wa kubeba mawazo/matakwa ya mvutaji pamoja na
sala kwenda mbinguni. Aidha, tumbaku ilitumiwa kama dawa ya masikio, meno na
mafua yatokanayo na baridi.
Aina za Tumbaku
Kwa sasa inaaminika
kuwepo kwa aina sita za tumbaku.
1. BIDIS: Hizi ni aina ndogo ya sigara
zilizotengenezwa kwa mkono, na hutumiwa sana katika nchi za Bara la Asia. Mtu
anapovuta aina hii ya sigara hupata lami, nikotini na kaboni monoksidi nyingi
zaidi kuliko sigara za kawaida.
2. BIRI: Hii ni aina ya sigara inayosokotwa kwa
majani ya tumbaku au kwa kutumia karatasi iliyotengenezwa kwa tumbaku. Kwa
kulinganisha na asidi ya tumbaku iliyo kwenye sigara, tumbaku iliyo kwenye biri
hufanya nikotini iingie kupitia mdomo hata ikiwa biri haijawashwa.
3. KRETEKS. Hii ni sigara inayotengenezwa kwa
mchanganyiko wa tumbaku na karafuu. Kwa kawaida asilimia 60 inakuwa ni tumbaku
na asilimia 40 inakuwa ni karafuu. Mtu anapovuta aina hii ya tumbaku hupata
lami, nikotini na kaboni monoksidi nyingi zaidi kuliko sigara za kawaida.
4. VIKO: Hii ni tumbaku aina ya kiko. Tumbaku
husagwa na kuwekwa kwenye kiko kinachotengenezwa maalum kwa ajili ya kuvuta
tumbaku na mara nyingi hupendelewa kutumiwa na watu wenye umri mkubwa na ina
athari zilezile za sigara za kawaida.
ENDELEA KUSOMA MAKALA HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
5. UGORO. Hii ni tumbaku inayotumiwa moja kwa
moja bila kutoa moshi. Aina hii hutumika kwa ama kwa kutafuna au kwa kunusa.
Kwa hiyo nikotini yake huingia kwenye damu kupitia mdomoni. Ni hatari kutumia
tumbaku hizo zisizokuwa na moshi kama tu tumbaku nyingine.
6. SHISHA. Hii ni tumbaku inayovutwa kupitia
mvuke wa maji maji. Moshi wa Shisha unaovutwa, hupitishwa kwenye maji kabla ya
kuvutwa. Hata hivyo, mbinu hiyo haipunguzi kiasi cha nikotini kilichomo ndani
ya tumbaku na zaidi huweza kusababisha kansa mapafu.
Shirika la Afya
Ulimwenguni (WHO), linazungumzia matumizi ya tumbaku kwa kusema: "Tumbaku
inatumiwa katika njia nyingi tofauti-tofauti. Tumbaku huuzwa katika maduka
yanayouza dawa na bidhaa za vyakula vya kuboresha afya. Hata hivyo, tumbaku ni
hatari hata itumiwe kwa njia yoyote ya gani."
Uvutaji wa tumbaku una
kemikali za sumu, kama vile nikotini, lami (tar), kaboni monoksidi, arsenic,
benzopyrene na nyinginezo. Mvutaji anameza sumu hizi angalau kwa kiwango kidogo.
Madhara yake yanajumuisha kufika wakati ambapo athari yake ni kuua kidogo
kidogo viungo vya mwanadamu na nyama nyama (tissues) za mwanadamu. Mtu anaweza
kufa kutokana na magonjwa yanayosababishwa na tumbaku kama vile kansa na
magonjwa ya moyo.
Kwa mujibu wa ripoti
za WHO, kwa kila sekunde nane, mtu mmoja hufariki dunia ulimwenguni kutokana na
matumizi ya tumbaku. Inaaminika pia kwamba watu saba kati ya wavutaji tumbaku
10, huanza matumizi hayo wakiwa watoto.
Ripoti za shirika hilo
zinasema kadri mtu anavyoendelea kuvuta tumbaku kwa muda mrefu, hufupisha urefu
wa maisha yake kwa takruban miaka 20 hadi 25. Hiyo inatokana na sababu kwamba
tumbaku ina aina za kemikali zipatazo 4,000 ambazo zina uwezo wa kudhuru afya
ya binadamu. Uchunguzi unaonyesha kwamba zaidi ya asilimia 80 ya chembe za
moshi unaovutwa hubakia mwilini.
Inaelezwa kwamba katika karne moja tu iliyopita, watu milioni zaidi ya milioni 100 walifariki dunia kutokana na uvutaji wa sigara.
Inaelezwa kwamba katika karne moja tu iliyopita, watu milioni zaidi ya milioni 100 walifariki dunia kutokana na uvutaji wa sigara.
Aidha, takwimu
zilizopo zinaonyesha kwamba watu zaidi ya milioni sita hufariki dunia kila
mwaka kwa sababu ya kuvuta sigara.
Wataalamu wanaonya kwamba ikiwa mambo hayatobadilika, kufikia mwaka 2030, uvutaji wa sigara utasababisha vifo vya watu zaidi ya milioni nane kila mwaka. Aidha, wanatabiri kwamba uvutaji wa sigara utasababisha vifo vya watu bilioni moja hivi kufikia mwisho mwa karne ya 21.
Wataalamu wanaonya kwamba ikiwa mambo hayatobadilika, kufikia mwaka 2030, uvutaji wa sigara utasababisha vifo vya watu zaidi ya milioni nane kila mwaka. Aidha, wanatabiri kwamba uvutaji wa sigara utasababisha vifo vya watu bilioni moja hivi kufikia mwisho mwa karne ya 21.
Athari za tumbaku
zinaanzia kwa mkulima wa zao hilo, familia yake na hatimaye mvutaji na watu
wanaokaa karibu na wavutaji nao. Upo ushahidi wa kutosha wa kisayansi kwamba
moshi wa sigara usiokuwa wa moja kwa moja, husababisha magonjwa sawa kama
sigara inayovutwa moja kwa moja, ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa moyo na mishipa,
mapafu na upumuaji (COPD).
Kutokana na hali hiyo,
maelfu ya watu wasiovuta sigara nao hufariki dunia kila mwaka kutokana na
kuishi au kukaa karibu na watumiaji wa tumbaku. Ndiyo maana WHO wanasema:
"Moshi wa sigara unaweza kumdhuru mtu asiyevuta bila kujali kiwango cha
moshi anachopumua."
Hivi sasa, hatari za
kiafya za moshi wa tumbaku ni suala la makubaliano ya kisayansi, na hatari hizo
zimekuwa moja ya motisha kubwa kwa ajili ya kupiga marufuku sigara katika
maeneo ya kazi na ndani ya maeneo ya umma, ikiwa ni pamoja na mikahawa, baa na
klabu za usiku.
Kwa mujibu wa utafiti
uliofanywa na Chama cha Wazuiaji Tumbaku Tanzania (CTCA), hakuna mkulima wa zao
la tumbaku ambaye amenufaika na kilimo hicho. Badala yake, utafiti huo
unabainisha kwamba wakulima wengi wa zao hilo wamechoka kiafya kutokana na
maradhi ya ngozi, kansa na magonjwa ya kifua kikuu.
CTCA wanaamini kwamba
kuendelea kuwepo kwa matangazo, promosheni na ufadhili wa bidhaa za tumbaku
nchini kumesababisha ongezeko kubwa la matumizi ya tumbaku miongoni mwa vijana.
Kwa mfano, utafiti uliofanywa mwaka 2008 na taasisi binafsi ya Global Youth
Tobacco Survey, ulionyesha kuwa asilimia 1.06 ya wanafunzi mashuleni na vyuoni
wanatumia bidhaa zinazotokana na tumbaku.
Baadhi ya athari za tumbaku katika mwili wa
binadamu ambazo zimethibitishwa na wanasayansi ulimwenguni:-
Nywele – Uvutaji wa sigara hudhoofisha kinga ya mwili na kisha kudhuru mizizi ya nywele mapema.
Akili – Uvutaji sigara
una madhara kwa akili ya mwanadamu na namna ya kuwasilisha hoja zake. Mtu
ambaye ameathirika na sigara anapitia vipindi vibaya vya kuhitaji kuvuta sigara
kila wakati na kumfanya kuwa mgumu wa kufikiri, kuwa makini, kusuluhisha tatizo
au kufanya jambo lolote muhimu hadi avute sigara. Pale mtu anapovuta sigara,
misuli yake inajiachia na anapata kipindi cha mapumziko mafupi ya kutokwa na akili
yanayogubika tatizo lililomkumba, lakini baada ya hapo mvutaji anaweza kupatwa
na maumivu ya kichwa na kizunguzungu.
Aidha, tumbaku
husababisha uraibu (addiction). Kemikali aina ya nikotini katika tumbaku
husisimua na vile vile hutuliza hisia. Wanasayansi wamegundua kwamba nikotini
hiyo huongeza kiwango cha homoni za mkazo. Lakini pia, kemikali hiyo humfanya
mvutaji ajisikie vizuri wakati anavuta sigara, na zaidi humpa mvutaji msongo wa
mawazo na kushuka moyo pindi anapomaliza kuvuta sigara.
Kuvuta sigara hupeleka
nikotini haraka kwenye ubongo tena na tena. Inaelezwa kwamba pafu (mvuto) moja
la sigara, ni sawa na dozi moja, hivyo mvutaji wa kawaida anaweza kuvuta dozi
200 kwa siku, ambacho ni kiwango cha juu kuliko dawa yoyote ile. Ndiyo maana
nikotini husababisha uraibu mkubwa zaidi. Mtu aliyezoea kuvuta sigara hujihisi
vibaya anapokawia kuvuta.
Macho – Wavutaji wa
sigara hupata magonjwa ya macho mara nyingi kuliko wasiovuta. Sehemu ya macho
inayopitisha mwangaza inaweza kufichwa kama vile wingu linavyoficha jua na
kusababisha upofu. Ugonjwa huu husababishwa kwa njia mbili. Kwanza moshi wa
sigara huwasha macho, na pili; kemikali zilizo ndani ya sigara hupita kwenye
mishipa ya damu na hatimaye kudhuru macho. Sigara pia husababisha kudhoofika
kwa sehemu ya kati ya macho (retina) na hivyo kupunguza uwezo wa macho kuona
vizuri na hata kutofautisha rangi (macular degeneration).
Ngozi – Uvutaji
tumbaku husababisha kukauka kwa ngozi, kubadilika rangi ya ngozi na kuwa njano
pamoja na kukunjamana kwa ngozi. Sigara huleta magonjwa mengi ya ngozi kama
vile uvimbe, kuwashwawashwa na kudhoofisha hali ya ungaavu wa ngozi. Kemikali
zinazopatikana ndani ya sigara hupunguza uwezo wa ngozi kujirekebisha, hivyo
ngozi huzeeka haraka na kupoteza uwezo wa kulainika. Mvutaji wa sigara
huonekana mzee zaidi kuliko umri wake.
Aidha, harufu mbaya ya
moshi huganda katika ngozi. Uvutaji sigara unasababisha saratani ya ngozi.
Kemikali za sigara husababisha vidonda kwenye ngozi na ambavyo haviponi kwa
urahisi, ma wakati mwingine huweza kugeuka na kuwa saratani.
Masikio – Uvutaji
sigara huweza kusababisha magonjwa ya masikio. Sababu ni kwamba uvutaji wa
sigara husababisha uchafu kuganda kwenye mishipa ya damu, na hivyo kupunguza
mwendo wa damu hadi kwenye sehemu za ndani za masikio. Moshi na kemikali za
tumbaku pia hujeruhi sehemu za ndani za masikio na majeraha hayo yanaweza
kuambukiza hata ubongo (meningitis) na hatimaye kusababisha uziwi.
Kinywa – Tumbaku
hutatiza mdomo na kuongeza uchafu unaoganda kwenye meno, hivyo kusababisha
kuoza kwa meno na harufu mbaya mdomoni. Tumbaku huathiri chembechembe za kinywa
zinazotumika kuonja ladha ya chakula, hali inayowasababishia watumiaji wa
tumbaku kushindwa kufurahia vizuri ladha ya vyakula.
Aidha, tumbaku
husababisha fizi za kinywa kutokwa na damu, na wakati mwingine husababisha
kushindwa kupona kwa vidonda mdomoni, hasa baada ya kung'olewa kwa jino.
Saratani za mdomo, ulimi na koo zinapatikana zaidi kwa wavutaji sigara na
watumiaji wa tumbaku za aina nyingine.
Mapavu – Wavutaji
wa tumbaku hupata taabu ya kupumua kwa kuwa uvutaji huharibu mapafu. Uvutaji
husababisha kukohoa na kutoa malenda-lenda pamoja na magonjwa ya mapafu
(emphysema & chronic bronchitis). Endapo mvutaji ana ugonjwa wa pumu,
anaweza kuongeza hatari zaidi ya kubanwa kifua na kuishiwa pumzi.
Uvutaji wa sigara
ndiyo sababu kubwa zaidi ya saratani ya mapafu, na pia husababisha kupasuka kwa
vibifu vya hewa safi na kutoa harufu mbaya mwilini. Wavutaji pia hupata
saratani ya koromeo na kuziba njia ya hewa, na hivyo inabidi kutobolewa kwa kishimo
kwenye shingo ili kuwezesha mgonjwa kupumua.
Nyama za mwili na
mifupa – Tumbaku husababisha mzunguko wa damu na hewa safi, kwa maana ya
oksijeni kupungua kwenye nyama za mwili na hivyo kusababisha maumivu ya nyama
na viungo pale mvutaji anapofanya mazoezi au anapokuwa michezoni.
Sigara inasababisha mifupa kuwa mnyepesi na kupunguza nguvu. Sababu ni kwamba kemikali zilizoko ndani ya sigara, hupunguza uwezo wa mwili kujenga mifupa iliyo na nguvu. Mifupa kama hii huvunjika kwa urahisi na kuchukua muda mrefu kupona, hivyo kusababisha magonjwa ya mifupa kama vile ‘Rhematoid Arthritis.’
Sigara inasababisha mifupa kuwa mnyepesi na kupunguza nguvu. Sababu ni kwamba kemikali zilizoko ndani ya sigara, hupunguza uwezo wa mwili kujenga mifupa iliyo na nguvu. Mifupa kama hii huvunjika kwa urahisi na kuchukua muda mrefu kupona, hivyo kusababisha magonjwa ya mifupa kama vile ‘Rhematoid Arthritis.’
Moyo – Tumbaku ni
chanzo kikuu cha magonjwa ya moyo. Uvutaji wa tumbaku huharibu mishipa ya damu,
hufanya mishipa kuvimba na kufanya upenyo wa damu kuwa mdogo. Hali hii husababisha
moyo kusukuma damu kwa nguvu na kasi kubwa kuliko kawaida na hivyo kusababisha
shinikizo la damu kupanda (High Blood Pressure). Hata kwa wale wanaovuta sigara
chini ya tano kwa siku, wako katika hatarini pia kupata magonjwa ya moyo.
Aidha, uvutaji tumbaku
husababisha damu kuganda kwenye mishipa ya damu na kuzuia mzunguko wa damu hadi
kupelekea mshtuko wa moyo(Heart attack) tatizo linaloweza sababisha kifo cha
ghafla. Moja kati ya kila vifo vitatu ulimwenguni hutokana na magonjwa ya moyo
na huua zaidi ya watu milioni moja kwenye nchi za Afrika.
Kiharusi/Kupooza(Stroke) kinaweza tokea endapo damu itaganda kwenye mishipa ya
damu ya kichwa na kuzuiia mzunguko wa damu kichwani au pale mishipa inapozidiwa
na kupasuka.
Tumbo – Sigara
hupunguza uwezo wa mwili kujikinga dhidi ya viini vinavyosababisha vidonda
tumboni. Pia hupunguza uwezo wa tumbo kustahimili nguvu ya asidi baada ya kula.
Vidonda vya mvutaji huwa ni vigumu kutibu na mara nyingi hutokea tena baada ya
kupona.
Vifole na Kucha
– Tumbaku husababisha kutu inayokusanyika na kuganda kwenye kucha na
vidole vya mvutaji, na hivyo kusababisha kubadilika kwa rangi ya vidole na
kucha kuwa manjano au maji ya kunde. Ngozi ya vidole pia hukauka na kuwa ngumu
kwa sababu ya joto na kemikali za sigara.
Mishipa ya Damu –
Uvutaji tumbaku husababisha ugonjwa ambao kitaalam unajulikana kama ‘Buerger's
Disease.’ Huu ni ugonjwa wa uvimbe kwenye mishipa ya damu ya miguuni na
mikononi. Mishipa hii huzibwa na kuzuia mwendo wa damu kwenye sehemu
zilizoathirika. Isipotibiwa kwa haraka, mvutaji anaweza kukatwa miguu au
mikono.
Afya ya uzazi kwa
mwanamke – Uvutaji tumbaku hupunguza nafasi za mwanamke kushika mimba na
kuharibu DNA kwenye shahawa za mwanaume. Ni vigumu zaidi kwa mwanamke mvutaji
sigara kutunga mimba na ni rahisi sana kwake kumpoteza mtoto wakati wa kulea
mimba (Miscarriage). Uvutaji wa sigara pia hufanya mwanamke kuzaa mtoto iyekufa
(Stillbirth) au aliye na kasoro kama uzito usiotimia wa kawaida. Watoto hawa
huwa na afya duni baadaye kwa sababu ya kemikali za sigara ambazo hupunguza
mwendo wa mtoto kukua akiwa angali mimbani.
Aidha, sigara
husababisha ugumba (menopause) kabla ya wakati wake. Sigara inaweza kumfanya
mwanamke kuwa tasa. Na pia sigara huongeza hatari ya kupata saratani ya fuko la
uzazi (Cancer of the uterus).
Afya ya uzazi kwa
mwanaume – Uvutaji wa tumbaku unapunguza msukumo wa damu kwenye sehemu za
uume. Sigara pia huharibu mbegu za kiume, na kwa hiyo watoto wanaozalishwa huwa
na uwezekano mkubwa wa kuwa na kasoro za maumbile na kupata magonjwa ya
saratani. Sigara pia huweza kuwasababishia wanaume wawe tasa.
Saratani – Zaidi ya
kemikali 40 zinazopatikana kwenye tumbaku zimethibitishwa kusababisha magonjwa
ya saratani kwa mvutaji, ikilinganishwa na asiyevuta sigara. Utafiti uliofanywa
na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road mwaka 2010/2011, umebainisha kwamba zaidi
ya asilimia 30 ya saratani zote, zinahusishwa moja kwa moja na matumizi ya
tumbaku na hivyo kuigharimu Serikali zaidi ya dola za Marekani milioni 40
kuhudumia wagonjwa wa saratani.
Kisukari
– Uvutaji sigara husababisha aina ya pili ya kisukari (Type 2 Diabetes
Mellitus), na hufanya kuwa vigumu kudhibitiwa. Hatari ya kupata kisukari ni
asilimia 30-40 kwa wavutaji, ikilinganishwa na wasiovuta. Endapo mvutaji ana ugonjwa
wa kisukari, anaongeza mara mbili hadi tatu hatari ya kupata ugonjwa wa figo.
Pia wavutaji wenye kisukari wana hatari zaidi ya magonjwa ya moyo, macho na
mfumo wa fahamu.
No comments:
Post a Comment