Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.
Hakimu Mwakalinga siku alipohukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa mauaji ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe. Leo amehukumiwa tena kunyongwa mpaka kufa katika mauaji ya mlemavu wa ngozi Henry Mwakajila.
Na
Daniel Mbega
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Mbeya leo hii imewahukumu kunyongwa
mpaka kufa watu wanne kati ya watano waliomuua Henry Mwakajila (17) ambaye ni mlemavu
wa ngozi (albino).
Waliohukumiwa kunyongwa mpaka kufa ni Asangalwisye Kayuni
maarufu kama Katiti au Mwakatoga na Gerard Korosso Kalonge (wakazi wa Kijiji
cha Mbembati wilayani Ileje), na Leonard Msalage Mwakisole na Hakimu Mselem
Mwakalinga (wakazi wa Kiwira wilayani Rungwe).
Mshtakiwa wa nne, Mawazo Philemon Figomole, ameachiliwa huru
na mahakama hiyo baada ya ushahidi wa upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha
pasi na shaka kwamba alihusika katika mauaji hayo.
Akisoma hukumu ya kesi hiyo ya mauaji yenye kumbukumbu Namb.
KIW/IR/49/2008 na PI 5/2013, Jaji wa Mahakama Kuu Dk. Revila, amesema mahakama
imejiridhisha pasi na shaka na ushahidi wa upande wa mashtaka kwamba washtakiwa
hao wanne walitenda kosa hilo na hivyo wanastahili adhabu hiyo.
Hii ni kesi ya saba ya mauaji ya albino kutolewa hukumu
ambapo mpaka sasa jumla ya watuhumiwa 15 wamehukumiwa kunyongwa mpaka kufa.
Ililezwa mahakamani hapo kwamba, mnamo Februari 5, 2008
majira ya saa 12:00 na saa 1:00 jioni huko katika Kijiji cha Ilolo, Kata ya Kiwira,
tarafa ya Ukukwe, wilayani Rungwe katika Mkoa wa Mbeya, washtakiwa hao
walimteka nyara kijana Henry Mwakajila, ambaye ni mlemavu wa ngozi aliyekuwa
akisoma kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Ukukwe na kisha kumuua.
Wakati wa mwenendo wa kesi, ilielezwa na mashahidi wa upande
wa mashtaka kwamba mshtakiwa wa kwanza Asangalwisye Kayuni maarufu kama Katiti
au Mwakatoga ambaye ni mganga wa jadi, mkazi wa Kijiji cha Mbembati, Wilaya ya
Ileje, alikutwa na utumbo unaodhaniwa kuwa wa binadamu na ulipopelekwa kwa
Mkemia Mkuu wa Serikali ukathibitika kwamba ni utumbo wa marehemu Henry.
Mshtakiwa wa pili, Gerard Korosso Kalonge wa Kijiji cha
Mbembati wilayani Ileje alikutwa na vidole vinne na mifupa kumi (10) vyote
vinavyodhaniwa kuwa vya binadamu na baada ya uchunguzi wa Mkemia Mkuu wa
Serikali ilibainika kwamba ni viungo vya marehemu Henry Mwakajila.
Ilielezwa pia kwamba, washtakiwa Leonard Msalage Mwakisole,
Mawazo Philemon Figomole na Hakimu Mselem Mwakalinga ndio waliodaiwa kumteka
nyara mtoto huyo na kumuua, kisha kupeleka viungo kwa mganga wa kienyeji
Asangalwisye Kayuni.
Mshtakiwa wa tano, Hakimu Mselem Mwakalinga, tayari
alikwishahukumiwa kunyongwa katika kesi nyingine ya mauaji ya Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, John Mwankenja, ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi
nyumbani kwake.
Hukumu ya kesi hiyo namba 131/2012 ilitolewa Novemba 13,
2013 ambapo inaelezwa kwamba watuhumiwa walitenda kosa hilo Mei 19, 2011 katika
kijiji cha Mpandapanda, Kata ya Kiwira Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya.
Ingawa watuhumiwa walikuwa wanne, lakini Mahakama Kuu Kanda
ya Mbeya chini ya Jaji Samwel Karua iliwahukumu kunyongwa mpaka kufa mshtakiwa
wa kwanza Hakimu Mwakalinga na mshtakiwa wa pili Daudi Mwasipasa kwa maelezo
kwamba walihusika moja kwa moja na mauaji hayo ya kukusudia.
Mshtakiwa namba tatu Obote Mwanyingili yeye alitiwa hatiani
kutokana na kosa la kumhifadhi mtuhumiwa namba moja baada ya kutoka kufanya
mauaji wakati mshtakiwa namba nne Kelvin Myovela alitiwa hatiani kutokana na
kuhifadhi silaha iliyotumika katika mauaji hayo ingawa hakusika na kitendo
hicho moja kwa moja, hivyo wote wawili walihukumiwa kifungo cha miaka saba jela.
Hata hivyo, Myovela tayari alikwishahukumiwa kifungo cha
miaka 20 jela kwa kukutwa na silaha kinyume cha sheria.
Inadaiwa kwamba, chanzo cha mauaji hayo ya John Mwankenja,
ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Rungwe,
kilitokana na kiongozi huyo kufahamu kwamba hao ndio waliomuua mlemavu wa ngozi
Henry Mwakajila, hivyo aliuawa ili kupoteza ushahidi.
Imeandaliwa
na mtandao wa www.brotherdanny.com
No comments:
Post a Comment