Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.

Mjadala uliopo katika jamii kwa sasa ni
kufananisha ufuasi mkubwa anaopata Edward Lowassa baada ya kujiengua CCM na
kujiunga na Chadema na alioupata Augustine Mrema alipojiunga na NCCR-Mageuzi
mwaka 1995 akitokea CCM.
Wanajadili kuwa alipoangukia Mrema, ndipo atatumbukia Lowassa huku
wakilinganisha umati wa watu unaomfuata Lowassa na ilivyokuwa enzi za Mrema;
walivyopokewa na upinzani, vijana wanavyoonekana kuhamasika na kushindwa kuvunja
mtandao wa CCM.
Ukweli ni kwamba kuna tofauti kubwa kati Mrema na Lowassa kama
inavyoelezwa hapa chini:
Tofauti zao
Tofauti ya kwanza ni taswira yao katika jamii, kwamba Mrema
alijijenga yeye binafsi ili aonekane kuwa nyota serikalini na katika jamii hasa
aliposuluhisha masuala ya ndoa. Lakini Lowassa amekuwa kama taasisi iliyojengwa
na wanasiasa na wafanyabiashara.
Mrema alijiondoa CCM ili asifukuzwe kwa utovu wa nidhamu
aliouonyesha baada ya kutoa bungeni siri za Baraza la Mawaziri kuhusu
kufisidiwa kwa mabilioni ya shilingi yaliyotolewa kwa ajili ya kufufua mkonge
na alitumia hoja hiyo katika kampeni wakati wananchi walikuwa hawaamini.
Lowassa amejiondoa baada ya jina lake kukatwa na vikao vya CCM bila kutoa
sababu hivyo ikatafsiriwa kuwa ameonewa na amebeba ajenda tatu kubwa; kupiga
vita umaskini, kutafuta ajira kwa vijana na kuimarisha elimu.
Mrema hakuwa na mawazo ya urais kabla ya kujiondoa CCM hivyo
alipojiunga NCCR hakuwa na mikakati wala muda wa kujijenga kwa wananchi
isipokuwa alitegemea umaarufu aliojijengea alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.
Lowassa alianza kutamani urais mwaka 1995, aliposhindwa alisimamia mtandao
uliomwingiza Ikulu swahiba wake Jakaya Kikwete na aliendelea kuutumia mtandao
huo kujijenga akiwa na matumaini kuwa ndiye ataungwa mkono kumrithi Kikwete
kwenye urais.
Mrema alijiunga na upinzani wakati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Nyerere alikuwa na nguvu na japokuwa alichangia kurejeshwa kwa mfumo wa vyama
vingi, hakutaka CCM ife akiwa hai, hivyo aliwaaminisha wananchi, kwa wakati
ule, kwamba CCM ilikuwa bado chaguo bora. Lowassa amejiunga na upinzani wakati
ambao Rais Kikwete anaonekana kukata tamaa hata kuitabiria kifo CCM na kwamba
ikipona mwaka huu basi itakwenda na maji mwaka 2020.
Mwaka 1995 Mrema alipojiunga na NCCR ilikuwa takriban miaka mitatu
tangu mfumo wa vyama vingi uruhusiwe hivyo vingi vilionekana kutokuwa na katiba
nzuri, sera, taratibu wala mfumo mzuri wa uongozi na kukosa wafuasi wengi.
Lowassa anajiunga wakati vyama vina ukomavu wa miaka 23; vina katiba, kanuni,
sera, mfumo mzuri, viongozi madhubuti na wanachama wengi.
Alipokuwa CCM Mrema alipandikiza chuki dhidi ya upinzani akidai
kuwa unaleta vita na chuki na haufai hivyo alipohamia upinzani alishindwa
kubadili fikra hizo kwani CCM walitumia mikanda ya video iliyoonyesha vita
katika nchi jirani ya Rwanda kuwatisha wananchi wasiwachague wapinzani. Lowassa
hakukomoa upinzani ila alijenga ngome imara usiweze kupenya Monduli na
amejiunga kipindi ambacho, wananchi wana uelewa mkubwa na wanajua vita
husababishwa na viongozi au vyama tawala vinavyong’ang’ania madaraka hata
vinapokuwa vimeshindwa.
Mrema alijiunga na upinzani wakati Watanzania hawakuwa wanajua
faida na hasara zake, hivyo walikuwa wanaogopa, lakini Lowassa amejiunga na
upinzani wakati jamii ina mwamko na hamasa kubwa baada ya kuona kazi
iliyofanywa na wapinzani wachache bungeni na katika mabaraza ya madiwani, hivyo
wengi sasa ni wanachama na mashabiki wa vyama vya upinzani na kwamba “iwe mvua
au jua” wanataka mabadiliko.
Tofauti yao nyingine ni juu ya umuhimu wa ushirikiano. Mrema
alipojiunga upinzani alikataa kuunganisha nguvu ili vyama vya upinzani vifanye
kazi kwa ushirikiano na vimuunge mkono mgombea urais wa chama hicho, akidai
NCCR ingesimama na kushinda uchaguzi peke yake. Lowassa amejiunga na Chadema
wakati chama hicho kimekamilisha kujenga ushirikiano madhubuti na vyama vingine
chini ya Ukawa na amesifu mikakati hiyo akisema ndiyo njia pekee ya kupambana
na chama chenye mizizi mirefu kama CCM.
Kisiasa Mrema alikuwa maarufu kama kada lakini hakuwa na mizizi
ndani ya chama ndiyo maana alipojivua uanachama na kujiunga NCCR hakuondoka na
vigogo wala wanachama mashuhuri ili wamsaidie kuchukua nchi. Kwa upande wake,
Lowassa ameonyesha nguvu zake; amewashawishi makada wengi kuhama CCM na
kujiunga na Chadema kuanzia vijijini wakiwamo madiwani, wabunge na wenyeviti wa
mikoa.
Tatizo jingine lililomkumba Mrema alipojiunga na upinzani ni hofu
waliyokuwa nayo makada wa CCM juu ya uwezo wake kuongoza nchi na chama na
kwamba alimudu alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kwa matamko yake au amri zake
za kuwataka wanaomiliki silaha za moto isivyo halali nchini, wazisalimishe
katika muda wa siku saba lakini alipwaya alipohamishiwa Wizara ya Kazi na
Ajira. Lowassa amemudu wizara zote alizoteuliwa kuziongoza na kuonyesha kipaji
cha uongozi kiasi cha kuelekea kumfunika hata bosi wake, Rais Kikwete katika
kipindi cha miaka miwili ya uwaziri mkuu.
Kwa kuwa aliupa upinzani picha mbaya, alipohamia alipigwa mabomu ya
machozi ili kumzuia na kuvuruga mikutano yake, kumfungulia kesi na kutisha
wananchi waamini upinzani ni vurugu na ni vita. Lakini Lowassa anaingia
upinzani wakati mazingira ya uhasama kati ya “ngunguri” na “ngangari” umepungua
kiasi ndiyo maana Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe amewasifu wapinzani
walivyoandamana kumsindikiza mgombea huyo wa urais kwenda NEC kuchukua fomu
huku wakisindikizwa na polisi.
Baada ya uchaguzi mkuu wa viongozi wa Bakwata kusuasua kwa muda
mrefu, Mrema aliingilia na kuhakikisha unafanyika, pia alipenda kuvaa
baraghashia ili ionekane hayuko mbali na watu wa dini zote. Lowassa
alichafuliwa na sakata la Richmond hivyo alijiuzulu akarudi kwa wananchi
kujisafisha kwa kushirikiana nao katika harambee za kuchangia vikundi vya
kiuchumi (kama vicoba), madawati, ujenzi wa makanisa na misikiti matukio
yaliyomjenga na hata kuwasahaulisha sakata la Richmond.
Mrema ameacha alama hadi leo; ujenzi wa vituo vidogo vya polisi
karibu na makazi ya watu ili kupunguza uhalifu ingawa aligonga mwamba
alipokwenda uwanja wa ndege wa Kimataifa kukamata dhahabu iliyokuwa inatoroshwa
kimagendo, na kumzuia Oscar Kambona kurejea nchini. Lowassa husoma mazingira na
sheria ndiyo maana aliweza kuzuia kubinafsishwa eneo la Mnazi Mmoja, Dar es
Salaam; na alihakikisha inafutwa sheria ya kikoloni iliyotumiwa na Misri kuzuia
Tanzania kutumia maji ya Ziwa Victoria, aliifurusha kampuni ya City Water
kutokana na ubabaishaji, na shule za kata ambazo Serikali ya Awamu ya Nne
inajivunia.
Mrema alipoingia upinzani aliwatisha sana watendaji wa serikalini
kwamba NCCR-Mageuzi wakiingia madarakani makamanda kadhaa wa Jeshi la Polisi,
viongozi serikali wangetiwa ndani. Lowassa amewaondoa hofu wote kwamba hana ugomvi,
chuki wala kinyongo na akishinda hatalipiza kisasi.
Mwaka 1995 vijana wengi walijitokeza kumshabikia Mrema na kusukuma
tu gari lake wakati wengi hawakuwa wamejiandikisha kupiga kura na
waliojiandikisha hawakupiga kura. Lowassa amejiunga na upinzani wakati vijana
wengi wamehamasika kujiandikisha kupiga kura na mijadala inayoendelea huenda
wengi wakapiga kura ili kukamilisha kile wanachodai wanataka mabadiliko.
*Mwandishi wa Makala hii ni Mhariri wa Uchunguzi na anapatikana kwa
baruapepe mwangulj@gmail.com na simu 0658383979.



No comments:
Post a Comment