Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.

Ali Hassan Mwinyi alizaliwa tarehe 8 mwezi wa tano (Mei) mwaka 1923 katika
kijiji cha Kivure, wilayani Kisarawe ,mkoa wa Pwani, Tanzania Bara. Kama wengi wa
viongozi wetu, Mwinyi naye alizaliwa katika iliyokuwa Tanganyika. Akiwa bado
mwenye umri mdogo sana familia yake ilihamia Zanzibar. Kwa maana hiyo Mwinyi ni
mzaliwa wa bara aliyekulia na kuendelea kuishi visiwani Zanzibar.
Alianza safari yake kielimu
huko visiwani Zanzibar katika shule ya msingi Mangapwani kuanzia mwaka 1933
hadi 1936 kabla ya kujiunga na shule ya sekondari Dole kwa ajili ya elimu ya
sekondari kuanzia mwaka 1937 mpaka mwaka 1942. Baada ya hapo alijiunga na Chuo
Cha Ualimu Zanzibar kusomea ualimu kuanzia mwaka 1943 mpaka 1944.
Kuanzia mwaka 1945 mpaka mwaka 1950 alirejea tena katika shule ya Mangapwani,shule aliyosomea,safari hii akiwa sio mwanafunzi tena bali Mwalimu.Kuanzia mwaka 1950 mpaka 1954 alikuwa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo wakati huo huo alikuwa akiongeza elimu yake kwa njia ya posta ambapo alijipatia General Certificate in Education (GCE) na pia alikuwa amejiunga na Durban University Institute of Education, United Kingdom (kwa njia ya posta tena) kusomea stashahada ya ualimu. Baada ya hapo alijiunga tena na Chuo Cha Ualimu Zanzibar kama mkufunzi kuanzia mwaka 1956 mpaka mwaka 1961 huku pia akiendelea kujisomea kwa njia ya posta kutoka Regent Institute kilichopo London nchini Uingereza ambapo alijipatia cheti cha ufundishaji lugha ya kiingereza.
Kuanzia mwaka 1961 mpaka 1962 alijiunga na Hall University, Uingereza katika Tutors’ Attachment Course. Mzee Mwinyi pia ana cheti ya lugha ya kiarabu alichokipatia Cairo nchini Misri kati ya mwaka 1972 na 1974.

Mwinyi (wa pili kutoka kushoto) akishuhudia mchezo wa bao kati ya hayati Mwalimu Nyerere (wa pili kutoka kulia) na mzee mmoja wa Butiama(jina halijulikani).Wengine wanaoshuhudia ni Mama Maria Nyerere(kulia) na kaka yake Nyerere,Chief Burito(wa tatu kutoka kulia).Picha ilipigwa Butiama.
Safari yake ya kisiasa aliianza rasmi mwaka 1964 alipojiunga na Afro Shiraz Party (ASP) huko Zanzibar ambapo alikitumikia chama katika ngazi na nafasi mbalimbali. Kati ya mwaka 1964 na 1965 alikuwa ni Katibu Mkuu wa muda katika wizara ya elimu Zanzibar kabla hajateuliwa kuwa Naibu Mkurugenzi katika iliyokuwa Zanzibar State Trading Corporation (ZSTC). Hiyo ilikuwa ni kati ya mwaka 1965 na mwaka 1970. Pia katika miaka hiyo hiyo, kuanzia mwaka 1966 mpaka 1970, Mwinyi alikuwa mweka hazina msaidizi katika tawi la ASP la Makadara,Zanzibar. Wakati huo huo pia kati ya mwaka 1964 mpaka 1977 alikuwa ni mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA)
Majukumu mengine aliyokuwa nayo miaka hiyo ni pamoja na uenyekiti wa Zanzibar Censorship Board (1964-1965), Mjumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam na pia mwenyekiti wa Baraza la Chakula na Lishe.
Kuanzia mwaka 1972 mpaka 1975, Mwinyi alikuwa ni Waziri wa Afya wa Tanzania kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kuanzia 1975 mpaka 1977. Mwaka 1977 aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Misri cheo alichokitumikia mpaka mwaka 1982 aliporejea nyumbani na kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii cheo ambacho alikutumia kwa muda mfupi tu kwani mwaka 1983 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi katika ofisi ya Makamu wa Raisi.
Mwaka 1984, kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Raisi wa Zanzibar wakati huo,Alhaj Aboud Jumbe, Mwinyi alichaguliwa kuwa Raisi wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar na wakati huo huo Makamu wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuanzia mwezi August mwaka huo huo wa 1984 Mwinyi alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi cheo alichoendelea nacho mpaka mwaka 1990 baada ya kung’atuka kwa Hayati Mwalimu Nyerere kutoka katika kukiongoza Chama Cha Mapinduzi(CCM)

Mwalimu
Nyerere aliamua kung'atuka kwa hiari yake na kumuachia kwa njia ya kidemokrasia
madaraka ya urais Alhaji Ali Hassan Mwinyi. Hiyo ilikuwa mnamo 1985.
Alipoingia madarakani kumpokea
aliyekuwa Raisi wa Awamu ya kwanza, Mwalimu Julius Nyerere mnamo tarehe 5
Novemba mwaka 1985, watanzania wachache sana (kama wapo) waliweza kutabiri
kwamba miaka kumi baadaye na zaidi baada ya kustaafu rasmi, ataibuka kuwa
mmojawapo wa maraisi wa Tanzania ambao watabakia kupendwa na kuheshimika kwa
namna ya kipekee kabisa.
Tunadiriki kusema “namna ya kipekee” kwa sababu ukweli
unabakia kwamba inapofanyika tathmini ya uongozi wake, bado mtu au watu
mbalimbali wanakuwa na maoni yao tofauti tofauti kuhusiana na suala hilo.
Utoaji huo wa tathmini ni suala ambalo haliwezi kukoma leo wala kesho, ni tukio
linaloendea na litakaloendelea, vizazi mpaka vizazi.
Mwinyi katika picha rasmi ya wakati wa utawala wake.
Huo ndio uzuri au ubaya wa
historia na muda (history and time),huwa vina jinsi ya kipekee katika kutoa hukumu
zao.
Mpaka anakabidhi madaraka
yake ya uraisi kwa raisi wa awamu ya tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa
mnamo tarehe 23 November mwaka 1995, jina ambalo wengi tulipenda kulitumia ni
“Mzee Rukhsa” ingawa kamwe hatukuwahi kusahau kwamba jina lake kamili ni Ali
Hassan Mwinyi, Raisi wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Rais Msaafu wa awamu ya pili Mh. Ali Hassan Mwinyi ni mtaalamu wa lugha ya
Kiswahili na pia hupenda michezo hususani jogging. Mwinyi ameoa wake wawili
(Sitti Mwinyi na Khadija Mwinyi), ana watoto na wajukuu. Anaishi Msasani jijini
Dar-es-salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Marais wastaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Dkt Jakaya Mrisho Kikwete na Mhe. Benjamin William Mkapa mara baada ya kulihutubia bunge kwa mara ya kwanza toka awe rais,





No comments:
Post a Comment