Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akizungumza na wananchi na viongozi wakati wa uzinduzi
wa Daraja la Kigamboni Jijini Dar es Salaam leo. (PICHA ZOTE NA KHAMISI
MUSSA)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akikata utepe huku viongozi wengine wakiushikilia kuashiria uzinduzi rasmi wa Daraja la Kigamboni katika wilaya mpya ya Kigamboni jijini Dar es salaam leo Aprili 19, 2016.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akiwapungia mimkono wananchi wakati alipokuwa akiondoka eneo la Daraja mara baada ya kulizindua
Wananchi wakimpungia mikono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli wakati alipokua akiondoka mara baada ya Uzinduzi wa Daraja hilo
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe
19 Aprili, 2016 amefungua rasmi Daraja la Kigamboni linalounganisha
usafiri wa barabara kati Kigamboni na Kurasini Jiji la Dar es salaam na
amependekeza Daraja hilo liitwe Daraja la Nyerere (Nyerere Bridge).
Sherehe
za ufunguzi wa daraja hilo kubwa na la kipekee kwa Afrika Mashariki na
Kati zimefanyika kando ya daraja hilo upande wa Kigamboni na kuhudhuriwa
na viongozi na wageni mbalimbali wakiwemo Mke wa Rais Mama Janeth
Magufuli, Balozi wa China nchini Tanzania Dkt. Lu Youqing, Naibu Waziri
wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Mhandisi Edwin Ngonyani, Naibu Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu) Mheshimiwa Antony Mavunde, Wabunge na Mameya wa Jiji na Dar es salaam.
Ujenzi
wa daraja hilo umehusisha nguzo mbili za pembezoni na mihimili miwili
inayoshikilia nyaya 36, na daraja zima lina urefu wa meta 680, upana wa
mita 32, njia sita za magari, njia mbili za watembea kwa miguu na
barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 2.5.
Daraja
hilo limejengwa kwa fedha za ndani na kugharimu jumla ya shilingi
Bilioni 254.12 ambapo kati ya fedha hizo asilimia 60 zimetolewa na
Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), na asilimia 40 zimetolewa na
Serikali ya Tanzania.
Kujengwa
kwa Daraja hili kutaondoa kero ya msongamano wa magari na usafiri kwa
wakazi wa Kigamboni na wakazi wa katikati ya Jiji la Dar es salaam ambao
walilazimika kutumia kivuko (Ferry) ili kukatiza eneo la mkondo wa
bahari ya Hindi ama kutumia barabara ya kuzunguka kupitia Kongowe lenye
urefu wa kilometa 52.
Daraja
hilo limefanyiwa majaribio kwa kutumia Malori 44 yenye uzito wa tani 30
na limethibitika kuwa na uwezo wa kubeba jumla ya tani 1,320 na hivyo
linatarajiwa kusaidia usafirishaji wa mizigo ya kutoka na kuingia katika
bandari ya Dar es salaam.
Akizungumza
katika sherehe hizo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli ameagiza vyombo husika vianze mchakato wa daraja hilo
kupewa jina la "Daraja la Nyerere" (Nyerere
Bridge) ikiwa ni kuuenzi mchango mkubwa wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere aliyefanya kazi kubwa ya kuijenga Tanzania.
Aidha,
Rais Magufuli amewapongeza wadau wote waliohusika kufanikisha ujenzi wa
Daraja hilo likiwemo Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Wizara ya
Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi na wakandalasi kutoka China, na ametaka
watanzania wajivunie daraja hilo kubwa na lililojenga heshima kubwa kwa
nchi.
Pia
Dkt. John Pombe Magufuli ametoa wito kwa vyombo vya habari vya Tanzania
kuitangaza vyema Tanzania na kuwa na uzalendo wa kweli kwa nchi yao
badala ya kubeza kazi nzuri zinazofanywa ndani ya nchi kwa manufaa ya
watanzania.
Katika hatua nyingine Rais
Magufuli amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam Bw.
Wilson Kabwe na kuagiza vyombo vinavyohusika kufanya uchunguzi dhidi ya
tuhuma zinazomkabili za kusaini mikataba iliyosababisha serikali
kupoteza mapato.
Dkt.
Magufuli ametangaza uamuzi huo wakati akitoa hotuba ya ufunguzi wa
daraja la Kigamboni, baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Bw. Paul
Makonda kumueleza kuwa amebaini upotevu wa shilingi Bilioni 3 uliotokana
na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam Bw. Wilson Kabwe kusaini
mikataba ya ukusanyaji mapato ya Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo kwa
kutumia sheria iliyopitwa na wakati, na pia ukusanyaji wa tozo za
uegeshaji wa magari ndani ya Jiji.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
19 Aprili, 2016
No comments:
Post a Comment