Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.
Bila ya shaka mmepata habari kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kuwa siku ya Jumapili ya tarehe 11/06/2016 akiwa kanisani kwake, Mchungaji Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima alitoa kauli za uongo, uchochezi na uchonganishi dhidi ya Chama cha Mapinduzi, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt John Pombe Magufuli, Viongozi wa CCM, Watendaji wa CCM na Serikali ya Awamu ya nne.
Mchungaji Gwajima amedai ati kwamba lipo kundi la wanaCCM wanaozunguka sehemu mbalimbali za nchi wakishawishi wanachama na wakimshawishi Mwenyekiti wa sasa Dkt Jakaya Mrisho Kikwete ili aendelee na Uenyekiti na kuleta hoja ya kutenganisha kofia ya Uenyekiti wa CCM na Urais wa nchi.
Napenda kuwafahamisha wana CCM, wapenzi wa CCM na wananchi kwa jumla kuwa madai hayo ya Mchungaji Gwajima ni uongo mtupu na hayana hata chembe ya ukweli. Ni mambo ya uzushi na hadithi ya kufikirika. Watu hao hawapo kwani kama wangekuwepo habari hizo zingekwishajulikana Chamani kupitia mfumo mahiri wa usalama na maadili wa ndani ya Chama cha Mapinduzi. Chama chenyewe kingekwishawatambua watu hao na kuwachukulia hatua zipasazo za udhibiti na nidhamu.
Kama mambo hayo yangekuwepo viongozi wa Chama wa Mikoa, Wilaya na Matawi waliofuatwa wangekuwa ndiyo wa kwanza kuwafichua. Habari za namna hiyo hazijapokelewa kutoka popote na kutoka kwa kiongozi yeyote wa Chama. Kama kweli Mchungaji Gwajima anawajua watu hao awataje hadharani na aseme walikwenda kumuona nani, wapi na lini kufikisha ujumbe wao huo hasi dhidi ya CCM.
Napenda kusisitiza kuwa habari za namna hiyo hazipo katika Chama cha Mapinduzi. Kwa hakika kinachoendelea sasa Mikoani na Wilayani ni maandalizi ya Mkutano Mkuu Maalum ambapo Mwenyekiti wa CCM wa sasa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete atastaafu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt John Pombe Joseph Magufuli atachaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya. Hakuna jambo lingine.
Nafurahi kuwafahamisha Viongozi na Wanachama wa Chama cha Mapinduzi kwamba kazi ya maandalizi ya Mkutano Mkuu Maalum inakwenda vizuri kabisa. Shughuli hiyo inasimamiwa na Naibu Katibu Mkuu Bara Ndugu Rajabu Luhwavi kwa niaba ya Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM. Kwa mujibu wa hatua iliyofikiwa sasa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa inaweza kukutana siku yoyote kupanga tarehe ya kufanyika kwa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM kwa uhakika.
Sisi katika Chama cha Mapinduzi hatushangazwi ingawaje tunasikitishwa na kauli za uongo, uchochezi na uchonganishi za Mchungaji Gwajima dhidi ya Chama cha Mapinduzi. Ana chuki iliyopitiliza dhidi ya CCM na Mwenyekiti wake. Yeye ni mtu ambae hajawahi kuitakia mema CCM. Hata yeye mwenyewe amekiri kwenye mahubiri yake ya tarehe 11 Juni, 2016 kuwa “alitaka CCM ishindwe katika chaguzi zilizopita na ndivyo anavyotaka iwe hivyo hata sasa, ili Chama chake cha upinzani kishinde.
Mchungaji Gwajima pia hana mapenzi na wala hamtakii mema Rais Dkt John Pombe Magufuli. Kwanza, hakutaka ashinde uchaguzi kwani alimpigania kwa hali na mali mgombea wa UKAWA. Pili, hataki adumu na kufanikiwa katika kazi yake ya Urais, ndiyo maana anatoa ushauri usiokuwa na mashiko na wakihasidi dhidi ya Mheshimiwa Rais. Anamshauri ati kwamba atoke Chama cha Mapinduzi na kuanzisha Chama chake. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais lazima awe mwanachama wa Chama fulani cha siasa.
Hivyo basi, Rais John Pombe Magufuli akitoka CCM anapoteza Urais na Makamu wa Rais anakuwa Rais na CCM inaendelea kuongoza. Yeye atakuwa hana chake. Hivyo Rais wetu atakuwa amepata au atakuwa ameharibikiwa? Huo kweli ni ushauri wa mtu anayedai kuwa na mapenzi mema na Mheshimiwa John Magufuli? La hasha! Huo ni ushauri wa adui yake na wala siyo wa mtu rafiki na mwenye huruma na mapenzi na Rais wetu.
Mchungaji Gwajima anataka kufanya “danganya toto”. Napenda kumhakikishia yeye na genge lake kuwa “CCM hatudanganyiki na Rais Magufuli ndiyo kabisa “hadanganyiki na wala hababaiki”. Mheshimiwa John Pombe Magufuli siyo kama Bwana fulani aliyekubali kudanganywa na Gwajima na kudanganyika. Alitoka CCM akiamini kuwa angeshinda. Aliyomtabiria hayakuwa na sasa yeye na wenzake wanajuta na wengi wameanza kukimbia. Rais wetu mpendwa na Mwenyekiti wetu mtarajiwa hawezi kudanganyika kiurahisi namna hiyo. Mheshimiwa John Pombe Magufuli ni mtu makini na mahiri.
Shabaha ya Mchungaji Gwajima ni kutaka kuleta mfarakano ndani ya Chama cha Mapinduzi kwa kumchonganisha Rais na Mwenyekiti wa CCM. Anachotaka ni kukidhoofisha Chama cha Mapinduzi na kumdhoofisha Rais John Magufuli ili kupalilia Chama chake na mgombea wake washinde uchaguzi ujao.
Napenda kusema kwa kujiamini kuwa hilo halitatokea kamwe. Mwenyekiti Kikwete ni kada aliyelelewa na kupikika vyema na viongozi waasisi wa Chama na Taifa. Anaelewa na kuheshimu mila na desturi nzuri ya CCM kuunganisha kofia ya Urais na Uenyekiti. Hawezi kwenda kinyume. Hakung’ang’ania Urais, hawezi kung’ang’ania Uenyekiti na wala hana mpango huo.
Hali kadhalika, hata ushauri wake wa kutaka Marais Wastaafu waondolewe kinga ili washitakiwe, shabaha yake ni ile ile ya kutaka kuleta mfarakano baina ya Rais John Pombe Magufuli na Marais wastaafu kwa lengo lile lile la kutaka kuleta mfarakano ndani ya CCM na nchini. Matumaini yake ni yale yale ya kudhoofisha CCM na Rais wake ili kunufaisha upinzani. Kamwe Rais wetu hatanasa katika mtego huo.
Kwa kweli inasikitisha kuona Kiongozi wa dini akitumia madhabahu takatifu kusema uongo na kupanga fitina na kupandikiza chuki katika jamii. Hatutegemei Kiongozi wa dini kuwa hivyo. Hatukupenda kujibizana na Kiongozi wa dini lakini kwa vile ameacha ya dini na kuingilia ya upande wetu tumelazimika kusema. Wahenga wamesema “lisilobudi hutendwa”
Nawaomba wanaCCM na Wananchi kupuuza uongo, uzushi na ushauri hasi wa Mchungaji Josephat Gwajima.
Christopher Ole Sendeka.
Msemaji wa Chama Cha Mapinduzi.
No comments:
Post a Comment