Miaka michache nyuma serikali iliona umuhimu wa filamu zetu za kitanzania(bongo movie) na kuamua kurasimisha tasnia hiyo, lengo ambalo lilifurahisha wadau wa tasnia hiyo nchini mimi nikiwa mmojawapo, ila tofauti na wengi nilijiuliza kwa nini sasa hivi?
Nikajiuliza sana, nikapata majibu mawili, la kwanza ni serikali kushtuka kuona msiba wa Steven Kanumba ulivyokuwa mkubwa, la pili kuona ugomvi wa Kanumba na Ray kuhusu magari yao aina ya V8. Hayo ni majibu niliyojipa mimi, kuwa umati na ukubwa wa msiba wa Kanumba uliionesha serikali kuwa kumbe hii tasnia ina wapenzi wengi na kuwa kumbe kuna hela huku.
Pili Ray na Kanumba kugombana kuwa kila mtu anadai gari yake ndio nzuri na gharama serikali ikaona kuwa kumbe huku kuna hela. Kama majibu niliyojipa ni sahihi basi serikali haipo serious na wananchi wake. Mi nadhani serikali inatakiwa kuwa na dhamira madhubuti ya kusaidia wananchi wake hasa vijana ambao ndio asilimia kubwa, kwahiyo ilivyoona vijana wanahangaika na filamu mwanzoni tu ingetupia jicho huko na tena sio kwa kutoa udenda kwa ajili ya kodi bali kwa nia njema ya kuwaokaoa wananchi wake kiajira na kisha kupata kodi, kurasimisha kitu ambacho kimekaa zaidi ya miaka 12 tena kinahusu vijana wa taifa husika na tena ni kitu kinachotazamwa majumbani mwa watu kila siku na magazetini kinaandikwa kila siku na ni chanzo cha ajira nyingi kwa vijana.
Miaka 12 ni muda mrefu mno na ndio chanzo cha mi kujiuliza kwa nini sasa hivi? Au ndio hadithi ya mwenye ng’ombe kumuacha ng’ombe akajitafutie mwenyewe chakula kisha akinenepa amkamue maziwa. Mpaka mwaka 2013 filamu ndio ilikuwa sekta ya pili kwa kutoa ajira nyingi kwa watu nchini Nigeria, ya kwanza ikiwa ni sekta ya kilimo. Hilo sio suala dogo kwa serikali, maana serikali inatakiwa iumize kichwa kwa ajili ya wananchi wake kupata ajira au kwa kifupi shughuli za kuingiza kipato.
Serikali yetu ya Tanzania ilitakiwa kutupia jicho katika filamu tangu 2013 kisha ikatengeneza mazingira mazuri ya kazi na biashara katika sekta hii ili baadaye ianze kupata kipato kupitia sekta hiyo na sio kuingia tu na kodi bila hata kujali mazingira ya kazi ya wahusika wa sekta hiyo(ng’ombe anapewa chakula ndio anakamuliwa sio anakamuliwa halafu ndio apewe chakula)
Kilichonisukuma kuandika makala hii ni baada ya juzi Mkuu wa Mkoa wa Dare es Salaam alipoongelea suala la kuongeza kodi kwenye filamu na muziki wa kutoka nje ya nchi ili filamu na muziki wa ndani upate soko kubwa(kulinda vya nyumbani).
Kauli ya mkuu wa mkoa inafanana na ile ya TRA kuhusu kodi kwa filamu za nje, namnukuu mkuu wa mkoa, ‘tunataka kuongeza kodi kwa filamu au muziki ambao unatoka nje kuja ndani,’ hiyo kauli inaonesha kabisa viongozi wanaongeaga kauli ambazo nia yao ni kutufanya wadau wa sekta hizi tujisikie vizuri na kudhani wanatujali wakati sio kweli.
Nasema hivyo kwa uhakika kwani kauli hizo zinaonesha viongozi na hata TRA huwa hawana taarifa ya biashara ya filamu Tanzania na duniani, yaani wanaongea vitu ambavyo hawavijui. Natoa ufafanuzi kidogo ili nieleweke kwa nini nasema hawajui chochote kuhusiana na filamu na kuwa wanaongea kudanganya toto wananchi wao. Filamu zinazozungumziwa za nje hapa asilimia 80 ni za Hollywood.
Hollywood filamu zao zimegawanyika mara mbili (1)indie films au independent films hizi kwa kifupi ni filamu zinazotengezwa kwa fedha za watu binafsi na huwa hazina gharama kubwa na kwa asilimia kubwa hazioneshwi sinema bali zinaenda moja kwa moja kwenye DVD(direct to DVD) (2) Studio films au blockbuster hizi ni filamu zinagharamiwa na studios, kuna major studios na minor studios. Filamu hizi hutengenezwa kwa gharama kubwa sana na huwa zinaenda kwanza sinema na huwekwa kwenye DVD baada ya siku 90.
Katika kipindi ambacho filamu zinaooneshwa sinema wachina huingia sinema na camera ambazo zina nguvu na kurekodi filamu nzima ambazo wao huzidurufu na ndio hizi zinauzwa madukani hapa Tanzania na sehemu kubwa ya Afrika. Kwahiyo ieleweke kuwa filamu zote tunazoona zinauzwa hapa nchini ni za wizi Hollywood hawazitambui.
South Africa kuna makampuni mawili STER KINEKOR na NU METRO hizi ni kampuni zilizoingia mkataba na kupewa mamlaka kuwa msambazaji wa filamu za Hollywood South Africa na nchi za jirani yake. Tanzania hakuna kampuni kama hiyo ya kusambaza,sasa jiulize TRA wanapata wapi ujasili wa kusema waweke kodi tena kwa kuweka stika katika DVD hizo. Je hawayajui hayo niliyoelezea hapo juu au wanayajua wanajifanya viburi? Jibu lolote watakalotoa litaonesha wao sio wazuri katika wanachofanya.
Na je mkuu wa mkoa alifanya research ya alichokuwa anakisema au ndio yale yale kutaka kuonesha wanajali wananchi wakati ukweli hawajui hata wanachokiahidi. Ushauri wangu kwa serikali ni kwamba iwe inasaidia kwanza pindi inapoona vijana wamebuni kitu chochote au shughuli yoyote ya kiuchumi iwafuate iwaandalie mazingira mazuri ya shughuli. Ifanye research katika jambo hilo,iwe tayari kupeleka hata watu wakapate utaalamu katika nchi zilizofanikiwa katika suala hilo.
Baada ya kuwawekea mazingira mazuri kwa muda mrefu wahusika, ndio ianze kutoka udenda wa kodi, maana hata stika ambazo TRA wanaweka kwenye DVD na CD za bongo movie wajue hata Kariakoo zinauzwa. TRA walidhani stika zinamtisha mwizi wa kazi za sanaa ukweli ni kwamba zile stika hazina shoti ya umeme kana kwamba ni kuweka na kuacha tu. Wanatakiwa wafuatilie la sivyo hapatakuwa na biashara ya filamu hapa nchini maana wanatakiwa kushangaa kwa nini wameanza kuweka stika na filamu ndio zimekufa kabisa!
Kingine serikali iweke watu TRA wenye ujuzi mbalimbali tofauti ili waweze kumudu shughuli zao, mfano kitengo cha filamu kiwe na watu wenye kujua filamu kiundani na hata kuzipenda pia hivyo vigezo vitasaidia utendaji kiufanisi. Maana wao hawajui filamu wanajua kodi tu ndio mana wanaanza kutuambia mambo ya kutoza kodi filamu za nje badala ya kuzifungilia mbali maana serikali ikichukua kodi kwenye kitu cha wizi basi na yenyewe imeshiriki katika wizi huo. Na nikisema wapende filamu namaanisha wakipenda filamu watakuwa na kauchungu kidogo kwa hiyo hawatalaghaiwa na visenti wanavyoweza kupewa na wafanyabiashara haramu.
Kwa mfano majuzi juzi Kariakoo ilichafuka polisi na TRA wakifunga maduka ya filamu za kizungu kwa makufuli yao. Wageni wa mambo haya waliokuepo Kariakoo wakasema duu serikali sasa inafanya kazi. Sisi ambao tunajua kuwa ile ni mikwara ya mara kwa mara tukawa tunacheka. Siku 6 zilizofuatia maduka yalikuwa wazi na hakukuwa na dalili za makufuli kuvunjwa kwa hiyo walipewa funguo. Na kama unavyojua wakati wakufunga maduka waandishi wa habari walijaa Kariakoo wakati wakufungua hakuwepo hata mmoja.
Kwenye filamu huwa nawaambia waigizaji ‘usinambie, nioneshe’ kama umechukia usiseme umechukia onesha,na serikali tumechoka kuwa mnatuambia tuonesheni. Kabla hamjarasimisha filamu zilishamiri mmerasimisha zimedoda, jiulizeni.
Imeandikwa na SEKABOYI 0753 666 444
No comments:
Post a Comment