Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.
Tino aliamka akiwa na
furaha kubwa ya ndoto yake ya muda mrefu kutimia. Ndoto hiyo si nyingine bali
ni kupanda cheo kipya jeshini. Hakuwa akidhani katika umri mdogo kama wake
angeweza kufikia cheo cha Ukapteni.
Hiyo haikuwa ni kazi nyepesi, ni baada ya
kujibidiisha katika mafunzo mbalimbali ya kozi za kijeshi alizofaulu vizuri
akiwa nchini Urusi, Uingereza na China.
Hiyo ilimfanya hata Jenerali Martin kuutambua uwezo
wake na kumpandisha vyeo haraka akinzia ngazi ya ukoplo.
Akavaa magwanda yake vizuri aliyoandaliwa na mpenzi
wake, Jackline na kufungua kinywa kisha akatoka himahima na kwenda kuwasha gari
yake aina ya Toyota Noah na kuipasha moto injini wakati akimsubiri mama yake
mzazi na mchumba wake Jackline waingie.
Kama kawaida waliingia taratibu lakini ilikuwa ngumu
kidogo simba kukubali kubaki peke yake pale nyumbani.
“simba kaa chini!” ilikuwa ni sauti kali ya Tino
ikimuamrisha mbwa wake mtiifu simba kubaki pale nyumbani, naye akakaa kimya uso
wake ukionesha huzuni mkubwa.
Ndani ya dakika mbili tayari walikuwa safarini
kuelekea makao makuu ya Jeshi Upanga.
Walifika na kupaki gari kisha wakashuka huku
Tino akiwaelekeza wakakae sehemu walizoandaliwa wageni watakaohudhuria
sherehe hizo kwa siku hiyo.
Tinonko naye aliambatana na wenzake waliokuwa ndani
ya magwanda yao, wakajipanga na kukaa siti za peke yao wakisuburi shughuli
ianze.
Wakati huo wote bendi ya jeshi ya matarumbeta
maarufu kama Brass Band ilikuwa ikitumbuiza nyimbo kadhaa za kizalendo.
Ilisemekana kuwa rais mwenyewe atakuwepo hapo siku
hiyo, hivyo kila mtu alikuwa bize kuhakikisha hakiharibiki kitu.
Muda
wote huo wageni waliokuja kushuhudia ndugu zao wakipanda vyeo walikuwa
wakishangaa jinsi wanajeshi walivyokuwa wakifanya mambo yao kwa ukakamavu kweli.
Na hii ilimshangaza
hata Jackline mwenyewe ambaye aliona kwa mara ya kwanza, mtu mzima sana
akimnyenyekea kijana mdogo kiumri. Hapo ndiyo mama yake Tino ambaye kidogo
alikuwa na uelewa wa masuala ya kijeshi kupitia mwanaye, akamfafanulia Jackline
kuwa heshima hiyo ilitokana na alama ya vyeo vyao walivyovibeba mabegani mwao.
Ndani ya muda mchache
walianza kukaribishwa kwenye shamrashamra na baadaye rais wa Serikali ya
Muungano wa Tanzania, alifika na kupita juu ya zuria jekundu kisha akaenda
kuketi kwenye jukwaa.
Shughuli ikapamba moto
kwa kupitia vipengele kadhaa vinavyoboa ikiwemo kusoma risala ndefu yenye
maneno kibao ya misamiati.
Jackline na mama yake
Tino wakajikuta wakipokezana kupiga miayo hadi mwishowe wakasinzia.
Walishtushwa na
vigeregere na vifijo kutoka kwa watu waliowazunguka walipoamka waligundua
ilikuwa ni zamu ya rais kutoa vyeo kwa wanajeshi hao na tayari alikuwa ameanza.
Walisubiri majina
mengi yakipita na hatimaye ilifika zamu ya mwanaye, Tino akasikia anatajwa;
Tinonko Marato. Mwenyewe akasimama kwa ukakamavu kutoka pale kwenye kiti chake,
akatembea hatua za kijeshi kufuata lile zuria jekundu kisha akapiga kwata na
kusogea mbele ya rais aliyekuwa amesimama katikati ya viongozi wengine wa
kijeshi.
Akawekewa nyota
mabegani na kurudi kwa mwendo uleule hadi kwenye kiti chake. Hii ilikuwa ni
furaha kubwa kwa mama Tino na Jackline; walikula na kunywa kisha sherehe
ikahamia nyumbani kwao.
“Mwanangu baba yako
angekuwepo angefurahi sana hata mimi nimefurahi sana, lakini nataka
unifurahishe zaidi, muoe huyu binti ili mniletee wajukuu, sitaki muishi hivi
tu,” alizungumza mama yake Tino akimwambia mwanaye wakati huo Jackline akiwa
bize kuandaa Juisi ya mapasheni huko jikoni.
“Mama
hata mimi mwenyewe nimelifikiria hilo, hamna tatizo, tuanze na kutangaza ndoa
ili mambo yaende vizuri. Kama unavyoniona nina kila kitu, sasa sioni sababu ya
kunizuia kuoa,” alizungumza Tino kiasi cha kumfanya mama yake atabasamu.
Usiku ulipoanza kuliteka
anga la dunia, Mama Tino alijikuta akizidiwa na usingizi uliotokana na uchovu
mkubwa, akaingia chumbani kwake na kulala.
Tino wakati huo
alitoka kwenye ua wa nyumba yake na kuketi huku akinywa juisi na kufurahia
mafanikio yake. Simba hakuwa mbali bali alizungukazunguka karibu ya bosi wake
na kutikisa mkia.
Mara kidogo alifika
Jackline, Tino akaona ni muda sahihi wa kumwambia alichoongea na mama yake;
Jackline alionekana kufurahia sana wazo hilo la kufunga ndoa.
Siku zilienda huku
taratibu za ndoa nazo zikishamiri hasa kwanza kwa kuzikutanisha familia zote
mbili kwa ajili ya hatua za awali.
Kila kitu kilienda
sawa na wakawa wamebakiza mwezi mmoja tu kabla ya ndoa yao. Michango ilikuwa
ikimiminika kila kona huku ndoa hiyo ikikaridiwa kuhudhuriwa na viongozi
wakubwa wa serikali waliopewa mualiko.
Mahari ilitolewa kwa
mujibu wa mila za Kichaga yaani upande wa bibi harusi mtarajiwa Jackline, kila
gharama iliyotakiwa kulipwa kwa wakati huo, Tino alikuwa tayari ameshalipa.
Lakini kadri siku
zilivyozidi kukaribia ndipo Tino alishangaa kuona mkewe mtarajiwa akizidi
kunenepa kiasi kwamba lile shela alilomnunulia siku chache nyuma likianza
kumbana.
Alishangaa pia kumuona
mchumba wake huyo akibadilika kila siku kitabia na kuanza wivu uliokithiri,
hakujua ni nini.
Maudhi yalivyozidi
alitamani hata ndoa hiyo aiharishe na kumtimua Jackline nyumbani kwake, lakini
aliamua kumshirikisha mama yake kwanza.
Mama huyo mtu mzima
aliyejua mambo mengi ya duniani alicheka na kumnong’oneza Tino; “nenda mkapime
inawezekana amenasa ujauzito.”
Kweli walivyopima
Jackline alionekana ana ujauzito wa wiki mbili. Wote wakajikuta wakifurahia na
kumshukuru Mungu kwa kuwabariki zaidi.
ITAENDELEA JUMANNE




No comments:
Post a Comment