Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, akitazama taarifa ya makadirio ya gharama za ujenzi wa sehemu ya barabara ya Mboga kuelekea kiwanda cha Matunda cha Sayona, wilayani Bagamoyo, leo. Kulia ni Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Pwani Eng. Rehana Yahya.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, akielekeza jambo kwa Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Bw. Magid Mwanga kuhusu makadirio ya gharama za ujenzi wa sehemu ya barabara ya Mboga kuelekea kiwanda cha Matunda cha Sayona, wilayani Bagamoyo, leo.
Mkandarasi wa kampuni ya Motsum Builders, Bw. Kante Bay akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, kuhusu sehemu ya barabara ya Mboga inayoelekea katika kiwanda cha Matunda cha Sayona, wilayani Bagamoyo, leo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (katikati), akitazama ramani ya mji inayoonesha maingilio ya barabara katika kiwanda cha Matunda cha Sayona, wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani leo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (katikati), akifafanua jambo kwa Meneja Mradi wa Kiwanda cha Marumaru na Masinki cha Twyford Ceramics Bw. Howard Li, kilichopo Chalinze mara baada ya kukagua kiwanda hicho, mkoani Pwani leo.
Serikali imesema kuwa itashirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo katika kutoa wataalam, kuandaa michoro na kusimamia ujenzi wa barabara zote zinazoingia katika viwanda vinavyojengwa mkoani Pwani.
Akizungumza leo mkoani humo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, amesema kuwa hatua hiyo imefikiwa mara baada ya uongozi wa Halmashauri ya wilaya hiyo kuandika barua kwa Wizara hiyo kuomba msaada wa kujengewa barabara ya Km 1 inayoingia kwenye kiwanda kipya cha Matunda cha Sayona kutoka kwenye barabara kuu ya Chalinze - Arusha na ile iliyopo katika kiwanda cha kutengeneza marumaru na masinki cha Twyford.
"Barabara hii ni ya kwenu Halmashauri, angalieni namna ya kukaa na mwenye kiwanda kuona namna ya kusaidia miundombinu yake, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Pwani, itasaidia huduma za kitaalamu na usimamizi”, amesema Naibu Waziri.
Aidha, Naibu Waziri huyo ameutaka uongozi wa Halmashauri hiyo kutumia fedha za Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), kuona namna ya kujenga barabara hizo na kuhakikisha ubora wa barabara hizo unaendana na thamani ya fedha zinazotolewa.
Kuhusu ujenzi wa barabara inayoingia kwenye kiwanda cha kutengeneza marumaru na masinki kilichopo wilayani hapo, Naibu Waziri Ngonyani, ameuagiza uongozi wa TANROADS mkoani humo kupima na kufanya tathmini ya gharama za ujenzi wa barabara hiyo ili kupata taarifa sahihi.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Bw. Magid Mwanga, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kufanya kazi kwa vitendo kwa kuchukua hatua za haraka za kutembelea maeneo hayo na kuboresha miundombinu ya barabara katika viwanda ili kuhamasisha na kuchochea wawekezaji wa viwanda nchini.
Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kujenga miundombinu bora kwa wananchi wake na Taifa kwa ujumla ili kuhamasisha uwekezaji wa viwanda na huduma za usafirishaji ili kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment