Kiongozi wa kimila wa jamii ya kifugaji wa kimasai, Laigwanani Salae Shinini akizungumza baada ya kuwasimika vijana kuwa wazee kwenye kitongoji cha Nomunyi Kijiji cha Loiborsiret Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Miundombinu ya shule ya sekondari ya Kata ya Loiborsiret Wilayani
Simanjiro Mkoani Manyara, imezidi kuimarishwa baada ya kumalizika
vyumba viwili vya madarasa na nyumba sita za walimu.
Diwani wa kata ya Loiborsiret Ezekiel Lesenga (Mardadi) aliyasema hayo
wakati akizungumza kwenye sherehe ya kuvuka rika kwa vijana wa
irkiponi na kuwa wazee iliyofanyika kitongoji cha Ndepes.
Mardadi alisema wamemaliza kujenga madarasa hayo mawili, vyoo vyenye
matundu nane na nyumba sita kubwa zilizo pamoja zenye vyoo na bafu
ambazo zitaishi familia sita za walimu wa shule hiyo.
Alisema wanasubiri serikali kukabidhi majengo hayo ambayo yamekamilika
na bado wanaendelea kujenga mabweni ya wavulana kwa wanafunzi wa shule
hiyo ambayo hivi sasa yapo kwenye msingi.
“Baada ya awali mimi binafsi kukabidhi madawati 100 kwenye shule hii
ya sekondari Loiborsiret, naishukuru serikali ya wilaya iliyoongeza
madawati 28 mengine na hivi sasa yameshafika,” alisema Mardadi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Loiborsiret Martin Noongululu alitoa wito kwa
vijana waliovuka rika kuwa wazee, waendelee kuchangia shughuli za
maendeleo ikiwemo elimu kwani maendeleo hayajastaafu.
Noongululu alisema baada ya vijana hao kutumia miaka 20 ya ujana wao
kwa kushiriki shughuli za maendeleo, wanapaswa kuendelea kufanikisha
maendeleo ya eneo hilo ili eneo hilo lizidi kupiga hatua.
“Kipindi hiki cha miaka miwili niliyooongoza kijiji hichi nimepata
ushirikiano mkubwa wa maendeleo nikiwa na vijana hawa waliovuka rika
hivyo waendeleze ushirikiano walionipa,” alisema Noongululu.
Mzee wa mila wa eneo hilo Alais Koina alisema jamii ya wafugaji wa
kimasai inawategemea wazee kwenye kutoa maamuzi yao ya kila siku hivyo
anatarajia vijana hao waliovuka rika watatimiza jambo hilo.
“Kupitia nafasi waliyoipata hawa hivi sasa wamekuwa wazee na jamii
yetu ya kifugaji inatarajia maamuzi makubwa kutoka kwa wazee na vijana
kazi yao itakuwa ni kutekeleza maamuzi hayo,” alisema Koina.
No comments:
Post a Comment