Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema anamsamehe Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema kwa maneno aliyosema kwenye mitandao ya kijamii kwa kuwa hajui atendalo.
Spika Ndugai amesema amesononeshwa na maneno yanayosemwa kuhusu Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kupigwa risasi.
Akizungumza baada ya kutambulisha wageni bungeni leo Alhamisi, Spika Ndugai amesema wabunge wenyewe ndio waliamua suala la matukio ya watu kushambuliwa kwa risasi liende wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.
Spika amesema Lema anamtuhumu kwa kumpeka mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge lakini wao ndio waliamua suala la watu kushambuliwa kwa risasi lijadiliwe na kamati ya ulinzi.
“Anasema maneno barabarani ayaseme huko kwa wabunge wenzake,” amesema Spika.
Kiongozi huyo wa Bunge amehoji ni kwa nini wanasubiri awaite kwenye kamati wakati wanaweza kwenda badala ya kupotosha wananchi.
Spika amesema hata yeye hajui kinachoendelea ila anasubiri kamati iwasilishe taarifa bungeni kesho.
Amesema si vizuri kutumia tukio hilo kuwashutumu wabunge wengine kama mashetani.
Spika amefafanua shutuma zilizotolewa na Lema kwenye mtandao akisema suala la Kubenea linahusisha mapenzi, Bunge kutogharamia matibabu na wabunge kuchangia badala ya Bunge kulipia.
Mbunge wa Singida Mashariki, Lissu alishambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi Alhamisi Septemba 7 akiwa nyumbani kwake Area D mjini Dodoma na sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Aga Khan iliyopo Nairobi, Kenya.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment