Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi la Polisi mkoani Arusha limeweza kudhibiti matukio ya uhalifu kwa 17.9% mwaka jana 2017 tofauti na mwaka 2016 ambapo kulikuwa na matukio 2,817 wakati mwaka 2017 kulikuwa na matukio 1,963 pungufu ya matukio 854, huku matukio ya uvunjaji yakipungua toka 604 hadi 294 ikiwa ni zaidi ya mara mbili ya mwaka 2016.
Akitoa taarifa hiyo Kamanda Polisi wa mkoa wa Arusha, Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo alisema kwamba, matukio hayo ya uhalifu yamezidi kupungua mwaka hadi mwaka ambapo mwaka 2016 matukio yalipungua kwa 6.8% ikilinganishwa na mwaka juzi 2015, na kuongeza kwamba hayo yote yanatokana na ushirikiano mzuri kati ya wananchi na Jeshi hilo.
Makosa mengine ambayo yamepungua ni pamoja na Unyang’anyi wa kutumia nguvu ambayo mwaka 2016 yalikuwa 86 na mwaka jana 2017 yameshuka hadi 40 huku makosa ya kutupa watoto yalikuwa 38 lakini mwaka 2017 yameshuka hadi kufikia 13.
“Matukio ya Mauaji nayo yalipungua kutoka 65 hadi 58 kwa mwaka 2017, wizi wa Watoto yalikuwa 20 na yamepungua hadi matukio mawili, na yalioongezeka ni Ubakaji na Ulawiti ambapo mwaka 2016 matukio ya Ubakaji yalikuwa 144 na mwaka jana yameongezeka matukio matano wakati makosa ya Kulawiti yalikuwa 58 yameongeza kufikia 62”. Alisema Kamanda Mkumbo.
Aidha katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya Jeshi hilo liliweza kukamata Cocaine gramu 480, Bhangi kilogramu 211 na gramu 760 na Mirungi kilogramu 317 na gramu 710 pamoja na watuhumiwa 554.
Kwa upande wa Usalama Barabarani Jeshi hilo limeweza kukusanya jumla ya shilingi 3,825,180,000 kutokana na makosa mbalimbali ambapo kwa mwaka 2016 Jeshi hilo lilikusanya jumla ya shilingi 4,708,680,000 kutokana na makosa hayo.
Hata hivyo Kamanda Mkumbo alisema kwamba kushuka kwa makosa ya Usalama Barabrani kumetokana na watumiaji wengi wa barabara hususani madereva wa vyombo vya usafiri kufuata vyema sheria za Usalama Barabarani hali hiyo imetokana na elimu iliyokuwa inatolewa na Jeshi hilo kitengo Usalama Barabarani kupitia Radio mbalimbali za hapa jijini Arusha, elimu kwa wanafunzi lakini pia elimu ya kituo hadi kituo kwa wadereva wa Pikipiki za abiria.
Pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kupunguza uhalifu, Kamanda Mkumbo ameendelea kutoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Arusha kuendelea kushirikiana na Jeshi hilo katika kutoa taarifa za uhalifu na wao kuzifanyia kazi mara moja lakini pia ametoa onyo kwa yoyote atakayedhubutu kushiriki kutenda uhalifu, atakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
No comments:
Post a Comment