Na
Tiganya Vincent
SERIKALI Mkoani Tabora imeagiza kukamatwa mara moja wazazi au walezi ambao hadi kufikia Jumatatu ijayo (15, January 2018) watakuwa wameshindwa kuhakikisha kuwa watoto wao waliochaguliwa kujiunga Kidato cha kwanza mwaka huu watakuwa hajaripoti katika Shule walizopangiwa.
Agizo hilo limetolewa jana mjini Sikonge na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri baada ya kupata taarifa kutoka kwa Afisa Elimu Mkoa iliyoakuwa ikionyesha kuwa idadi kubwa ya wanafunzi walichaguliwa kujiunga na Kidato cha kwanza mwaka 2018 bado wengi wao hawajaripoti katika Shule walizopangiwa.
Alisema kuwa kufikia Jumatatu ijayo anataka kupata taarifa na majina ya wanafunzi wote waliochangiwa ambao hawako shuleni ikiwa na majina ya wazazi wao ili hatua za kisheria dhidi yao ziweze kuchukuliwa kwa kosa la kumkoshesha watoto haki ya kupata elimu.
Mwanri aliongeza kuwa viongozi wa kuanzia mitaa, vitongoji, vijiji , Kata na Wilaya ni vema wahakikishe wanawatafuta watoto wote waliochaguliwa ambao hawako shuleni ili kujua walipo na wanafanya nini kwa kuwa inawezekana wapo ambao tayari wameshaozeshwa.
Alisisitiza kuwa wakikuta mtoto yupo nyumbani na mzazi wake hataki kumpeleka Shule wamukamate mzazi wake ili hawawezi kuwajibika kwa uzembe wake.
“Hapa tutakwenda kwa Sera ya mbanano…kama kiongozi lazima umbane mzazi ambaye hadi hivi sasa hajampeleka mtoto shule wakati wenzake wameshaanza masomo na ikibidi mfikisheni katika vyombo vya Sheria ili ajibu mashitaka yake ya kunyima mtoto haki yake ya elima”alisema Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora
Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora wakati wa ziara ya kukagua zoezi la upandaji miti kwa ngazi ya Shule za Msingi na Sekondari ,Katibu Tawala Msaidizi (Elimu) Suzan Nussu alisema kuwa hali ya watoto kuripoti katika Shule za Sekondari kwa wanafunzi walichaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka huu bado sio nzuri kwa baadhi yao hawajafika shuleni hadi hivi sasa.
Alisema kuwa katika Shule ya Sekondari ya Ngulu iliyopo Sikonge walichaguliwa watoto 130 lakini hadi hivi sasa wamejiunga 44, Shule ya Sekondari Usisya iliyopo Urambo wamechaguliwa 130 lakini waliripoti ni 54 na Shule ya Sekondari Nanga Sekondari iliyopo Igunga waliochaguliwa ni 160 lakini walioripoti ni 7 hadi kufikia sasa.
Nussu alisema kuwa kuchelewa kuripoti kwa wanafunzi hao sio tu kunarudisha nyuma maendeleo ya watoto hao kwa sababu ya kuachwa na wenzao bali pia kunasababisha usumbufu kwa walimu kuanza upya kuwafundisha wanafunzi waliochelewa ili waweze kwenda na kasi ya wenzao.
Alitoa wito kwa wazazi kuhakikisha ifikapo mapema wiki ijayo watoto wote wawe wamefika Shule kwani tayari Serikali ilishafuta ada na hivyo hakuna kisingizio ambacho kinaweza kumsababisha mtoto kushindwa kuanza masomo yake kwa ajili ya faida yake na Taifa kwa ujumla.
Nussu alisema kuwa michango mingine inapangwa na wazazi wa watoto wa Shule husika kwa kukubaliana na Kamati za Shule na hivyo hakiwezi kuwa kikwazo kwa watoto kushindwa kuhudhuria masomo yao.
Kwa upande wa Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Ngulu Israel Mwambikwa alisema kuwa amekuwa akipata tatizo kutoka kwa baadhi ya wazazi kushindwa kutoa hata michango waliokubaliana katika vikao vyao ya kutoa kilo 10 za mahindi ,kilo mbili za maharage na shilingi 17,000/- ambazo wazazi walikubaliana kama mahitaji ya chakula cha kila mtoto kwa mwezi.
No comments:
Post a Comment