Katika miongo kadhaa iliyopita, uvaaji wa
wigi umekuwa fasheni katika sekta ya urembo na hutumika hususan na wanawake.
Ingawa uvaaji wa wigi huwafanya wanawake hao kuonekana mithili ya mtu aliyevaa
kofia ngumu (helmet), lakini yaonekana ni mapendeleo ya wengi.
Wanaume wengi hujiuliza , "Ni kwanini
kinamama hupendelea kuvaa wigi na kusuka nywele za bandia?, wakati hupendeza na
kuwa warembo zaidi wakiwa na nywele zao za asili"
Wigi huvaliwa zaidi na kinamama wenye asili
ya Afrika au Wamarekani wa asili ya Afrika. Lakini tukiangalia moja ya chimbuko
hasa la uvaaji wigi ni ubaguzi uliokuwepo wakati wa utumwa ambapo wale wenye
ngozi nyeupe na nywele shombeshombe walipewa kazi za ndani na wale wasio na
ngozi nyeupe na nywele zisizo shombeshombe walifanyishwa kazi ngumu za
mashambani. Watumwa waliopelekwa barani Amerika hawakuweza kuzihudumia nywele
zao kutokana na hali ngumu, na mabwenyenye waliwashusha hadhi na kuwavunja moyo
kwa kuwaambia hawakuwa na nywele bali ni "manyoya".
Lakini sababu nyingine inayodhaniwa
kuwaathiri wanawake wa asili ya Afrika ni fikra kuwa mwanamke mwenye nywele
ndefu pengine hadi mgongoni ni mrembo zaidi. Pia siku hizi warembo na
wanaoshiriki katika mashindano ya urembo hujaribu kurefusha nywele zao
ili kuwa na viwango na aina za mitindo ya ughaibuni.
Pamoja na kuwa wanawake wanajaribu kuwa
warembo kwa uvaaji wa wigi, zifuatazo ni baadhi ya hasara au madhara kiafya ya uvaaji
wigi na usukaji wa nywele za bandia.
Uvaaji wa wigi au nywele za bandia waweza
kukusababishia mzio(allergy), endapo malighafi au kemikali zilizotumika
kutengeneza wigi hiyo zitasisimua mfumo wa kinga ya mwili wa mvaaji.
Kupata
mba ni tatizo jingine kutokana na uvaaji wigi, hii hutokana na kukosekana kwa hewa ya kutosha ya Oksijeni katika ngozi ya
kichwa(scalp hypoxia)
na katika
tishu za shina la nywele. Kwa hiyo kama utaamua kuvaa wigi uhakikishe
imetengenezwa kwa viwango vya ubora unaotakiwa na inapitisha hewa ya
kutosha ya
Oksijeni.
Pia waweza kunyonyoka nywele hata kama una nywele nzuri zenye afya, na kama utachagua
kuvaa wigi na unataka kuepuka madhara hakikisha kuwa nywele zako ni safi, usilazimishe
kuvaa wigi iliyo ndogo na yenye kubana sana, hakikisha unapata muda wa kupata
hewa na nywele zako zinapakwa mafuta kuepuka ukavu wa ngozi ya kichwa na nywele kukatika .
Maumivu ya kichwa ni tatizo ambalo laweza
kusababishwa na uvaaji wigi au usukaji wa nywele bandia. Wigi iliyo ndogo
husababisha mkandamizo kichwani na kusababisha maumivu ya kichwa ya mara kwa
mara.
Upotevu wa muda na fedha ni dhahiri kwa kuwa
ufumaji wa nywele za bandia waweza kuchukua muda mrefu, itamlazimu mvaaji wigi
kubadili kwa kununua mpya kila baada ya muda fulani au kuwa na wigi nyingi kwa
ajili kubadili kulingana na fasheni.
Harufu mbaya huweza kujitokeza endapo
mba na jasho vitachanganyikana na hupelekea uwepo wa bakteria au fangasi
na kusababisha muwasho mkali, hii yaweza kumkosesha raha mvaaji wigi na
mwenye kufuma nywele za bandia hasa pale anapokuwa katika majumuiko ya
kijamii.Kama utachagua kuvaa wigi hakikisha nywele zako zinasafishwa na shampoo au sabuni, zinakaushwa vizuri na kupakwa mafuta.
Endapo mwanamama atachagua kuvaa
wigi,asisahau kuwa nywele zake za asili zinahitaji matunzo,na azingatie
wakati wa kununua wigi au nywele za bandia, ahakikishe ananunua yenye
ubora
unaotakiwa ili kuepuka madhara ya kiafya anayoweza pata kutokana na
uvaaji wigi au anapofuma nywele za bandia.
No comments:
Post a Comment