Upande wa mashtaka umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa watabadilisha hati ya mashtaka katika kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili Rais wa Simba, Evans Aveva na makamu wake kwa kumuongeza mshtakiwa mwingine.
Mbali ya Aveva ambaye amefikishwa mahakamani hapo baada ya kulazwa Hospital ya Taifa Muhimbili kwa muda mrefu, mshtakiwa mwingine ni Godfrey Nyan’ge ‘Kaburu‘.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba, wakili wa TAKUKURU, Leornad Swai amedai kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali baada ya upelelezi kukamilika.
Hata hivyo, wakili Swai ameiomba mahakama ahirisho fupi kwa kuwa wanatarajia kufanyia mabadiliko ya hati ya mashtaka kwa kutaka kumuongeza mshtakiwa mmoja.
Kufuatia ombi hilo, Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi April 12, 2018 kwa ajili ya upande wa mashtaka kufanya mabadiliko hayo na washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.
Kwa pamoja washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi ikiwamo ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na utakatishaji wa fedha ambazo ni Dola za Marekani (USD) 300,000.
No comments:
Post a Comment