Spika wa Bunge, Job Ndugai ametoa wiki moja kwa Bodi ya Benki Kuu Tanzania (BoT) na menejimenti yake kufika mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kujieleza kuhusu matumizi ya bima binafsi ya matibabu.
Spika Ndugai ametoa agizo hilo lejana bungeni Juni 4, 2018 mara baada ya Mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga kusema BoT kuna ufisadi mkubwa wa watumishi wake kuendelea kutibiwa nje ya nchi.
Mlinga alisema wakati usalama wa Taifa, Bunge na taasisi nyingine zikitumia Bima ya Taifa ya Afya (NHIF), BoT ndiyo inayotumia fedha nyingi kuliko taasisi yoyote.
“BoT ukiumwa mafua unakwenda Uingereza. Matumizi yao yamepanda kutoka Sh1 bilioni wanatumia Sh12 bilioni kwa sababu watu wana maslahi binafsi,” alisema Mlinga.
Mlinga alisema hataunga mkono hoja ya Waziri Mpango (Philip) hadi atakapokuja na majibu ya maswali hayo.
Mara baada ya kumaliza kuchangia, Spika Ndugai aliagiza PAC, kuiita bodi ya BoT na menejimenti yake na wajieleze kwa nini wanafanya matumizi hayo na baada ya wiki moja waripoti kwake.
“Muwe mmekaa na Mlinga na mkae na NHIF, halafu sasa mnawaita hawa BoT, baada ya kufanya haraka sana mnipe na nimwandikie Rais ili aingilie kati,” alisema.
No comments:
Post a Comment