Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Winifrida Rutahindurwa akitoa hotuba ya Ufunguzi kwa makatibu wasaidizi wa TSC ngazi ya wilaya (hawapo pichani). Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Ajira na Maendeleo ya Watumishi TSC, Mectildis Kapinga, Pembeni (kushoto) ni Afisa Utumishi TSC, Bw. George Ndatta akifuatiwa na Mratibu wa Equip Tanzania, Bibi Phoebe Okeyo.
Mratibu wa Equip Mkoa wa Singida, Bibi Phoebe Okeyo akizungumza mbele ya makatibu wasaidizi TSC (hawapo pichani) ngazi ya wilaya. Pembeni yake (mwenye miwani) ni Katibu wa TSC, Winifrida Rutahindurwa, akifuatiwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Ajira na Maendeleo ya Watumishi TSC, Mectildis Kapinga na Pembeni (kushoto) ni Afisa Utumishi TSC, Bw. George Ndatta.
Afisa Utumishi mwandamizi kutoka TSC, Bibi Apsa Ally akiwasilisha mada juu ya masuala ya ajira katika mafunzo ya makatibu wasaidizi ngazi ya wilaya.
Washiriki wa mafunzo (makatibu wasaidizi) wakichukua dondoo muhimu katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wa utendaji kazi katika maeneo yao.
Makatibu wasaidizi wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo wa utendaji kazi katika maeneo yao.
Makatibu wasaidizi wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo wa utendaji kazi katika maeneo yao.
Katibu wa TSC, Bibi Winifrida Rutahindurwa (wa pili kutoka kushoto kwa waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Makatibu Wasaidizi ngazi ya wilaya. Wa kuwanza kushoto (waliokaa) ni Mkurugenzi Msaidizi wa Ajira na Maendeleo ya Watumishi TSC, Bibi Mectildis Kapinga, wa tatu (kutoka kushoto) ni Mratibu wa Equip Mkoa wa Singida, Bibi Phoebe Okeyo na pembeni ni Afisa Utumishi TSC, Bw. George Ndatta.
Na Adili Mhina
Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) imeendesha mafunzo ya siku mbili kwa lengo la kuwajengea uwezo makatibu wasaidizi wa TSC ngazi ya wilaya ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na kupunguza malalamiko na mashauri ya nidhamu ya Walimu.
Akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki mjini Singida, Katibu wa TSC, Winifrida Rutahindurwa alisema kuwa kila mtendaji wa TSC anapaswa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria katika kushughulikia masuala ya walimu ili kufanyaa maamuzi ya haki.
Alieleza kuwa TSC ilifanya tathmini ya utendaji kazi wa makatibu wasaidizi ngazi ya wilaya na kubaini kuwa zipo changamoto za uelewa katika masuala ya sheria, utawala na ajira ambayo yamekuwa yakiathiri ufanisi katika kutoa huduma stahiki kwa walimu.
“Mafunzo haya yamekuja baada ya zoezi lilofanyika Mkoani Iringa ambapo baadhi ya makatibu wasaidizi (wawakilishi) walishiriki na kubainisha maeneo ambayo mnahitaji kujengewa uwezo ili kuweza kutekeleza majukumu yenu,” alisema.
Alisisitiza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia watendaji kuzingatia kanuni, taratibu na sheria hususani katika kuandaa hati ya mashitaka kwa walimu pale inapohitajika. Eneo hilo limekuwa na dosari za mara kwa mara na kusababisha mashauri ya walimu kuchukua muda merefu bila kutolewa maamuzi.
Aidha, Katibu huyo aliagiza kuwa watendaji wanaoshiriki mafunzo hayo wanapaswa kuwafundisha wenzao ambao hawakuhudhuria ili kujenga uelewa wa pamoja katika kutekeleza majukumu ya Tume kwa mujibu wa sheria.
“Nipende kuwakumbusha kwamba, kwa kuwa hatujaweza kumshirikisha kila mmoja wenu, ninyi ni wawakilishi wa wenzenu ambao hawapo hapa, hivyo mnatakiwa kwenda kuwafundisha wenzenu mliowaacha maofisini kile mnachojifunza hapa”, aliagiza.
Mafunzo hayo yaliyotolewa na TSC kwa kushirikiana na programu ya Equip -Tanzania yalishirikisha makatibu wasaidizi kutoka wilaya za Ilala, Tabora, Hanang, Ludewa, Kibaha, Sengerema, Muleba, Kisarawe, Geita, Mpanda, Moshi, Arumeru, Singida, Chamwino na Namtumbo.
Naye Mratibu wa Equip Mkoa wa Singida, Phoebe Okeyo alieleza kuwa Taasisi yake imeamua kugharamia mafunzo hayo ikiwa ni hatua ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha TSC inafanya kazi kwa weledi katika kutekeleza majukumu yake.
Alieleza kuwa licha ya kufadhili mafunzo hayo, Equip imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na wadau mbalimbali wa elimu na kumekuwa na ushirikiano katika kutatua changamoto zinazorudisha nyuma maendeleo ya elimu nchini.
Akitoa mifano ya mipango ya taasisi yake katika kuimarisha sekta ya elimu nchini, Okeyo alieleza kuwa Equip Tanzania imedhamiria kugagawa vishkwambi (tablets) kwa waalimu wakuu na pikipiki kwa waratibu wa elimu kata katika mikoa tisa (9) hapa nchini.
Alitaja mikoa itakayonufaika na mpango huo kuwa ni Shinyanga, Tabora, Katavi, Lindi, Simiyu, Mara, Dododoma, Singida na Kigoma. Pikipiki hizo tayari zipo bandarini na mchakato wa kuzitoa na kuzigawanya kwa wahusika unaendelea kufanyika kulingana na utaratibu uliowekwa.
No comments:
Post a Comment