Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imetoa mafunzo maalumu kwa watumishi 101 wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) kwa lengo la kuimarisha ujuzi wa kitaaluma, kuongeza ufanisi katika utendaji kazi pamoja na kuendana na mabadiliko ya kimataifa katika Taaluma ya Uhasibu na Ukaguzi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Prof. Siasa Issa Mzenzi ameishukuru NAOT kwa kuendelea kushirikiana na NBAA katika kuwawezesha Wahasibu na Wakaguzi kupitia mafunzo mbalimbali ya kitaaluma, hususan mafunzo maalumu yaliyoandaliwa kwa watumishi wa ofisi hiyo.
Prof. Mzenzi amesema tangu alipoanza rasmi majukumu yake tarehe 30 Machi mwaka huu, amepokea salamu nyingi za pongezi kutoka kwa wadau mbalimbali wa Taaluma ya Uhasibu na Ukaguzi, jambo ambalo limempa hamasa ya kuendelea kuisukuma mbele Taaluma hiyo kupitia kaulimbiu ya “Moving the Profession Forward”.
Aidha, amempongeza aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius A. Maneno, kwa mchango wake mkubwa wa zaidi ya miaka 20 katika kuimarisha Taaluma ya Uhasibu na Ukaguzi nchini. Amesema mafanikio mengi yanayoonekana leo katika Taaluma hiyo yametokana na uongozi na juhudi zake katika kipindi chote cha utumishi wake.
Katika hatua nyingine, Prof. Mzenzi amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya NBAA na NAOT katika maeneo mbalimbali ikiwemo mafunzo, utawala bora pamoja na matumizi ya Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu wa Sekta ya Umma (IPSAS).
Amesema Tanzania imeendelea kuwa mfano bora barani Afrika katika utekelezaji wa viwango vya IPSAS, huku nchi nyingi za Afrika zikiiangalia Tanzania kama kitovu cha kujifunza uzoefu na mafanikio katika utekelezaji wa viwango hivyo. Ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na juhudi kubwa zinazofanywa na NAOT katika kuhakikisha Taasisi za umma zinaandaa taarifa za fedha zinazokidhi viwango vya kimataifa.
Sambamba na hilo, amewataka Wahasibu na Wakaguzi kujiandaa na mabadiliko mapya ya Taaluma, hususan katika eneo la Sustainability Reporting, akisema kuwa mfumo huo sasa ni sehemu muhimu ya taarifa za kifedha duniani. Ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha tayari imeanza kutoa mwongozo na ramani ya utekelezaji wa mfumo huo nchini.
Naye mwakilishi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles E. Kichere, amesema faida kubwa ya mafunzo hayo ni ushirikiano uliopo kati ya NBAA na NAOT katika kuandaa muundo wa mafunzo unaoendana na hali halisi pamoja na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu ya Ukaguzi wa hesabu za Serikali.
“Tumekuwa na muundo maalumu wa ratiba ya mafunzo haya ili kuhakikisha yanakuwa yenye tija na yanakidhi mahitaji halisi ya washiriki. Kabla ya kuanza rasmi kwa mafunzo, tulipata fursa ya kushirikiana kwa karibu katika kuandaa mada mbalimbali, jambo lililowezesha kuwepo kwa majadiliano yanayoakisi mazingira halisi ya kazi pamoja na changamoto zinazokabili Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali,” amesema.
Aidha, amesema ushirikiano huo umewezesha NBAA kutoa nafasi kwa wakufunzi wa ndani pamoja na wakufunzi kutoka NAOT kushiriki katika kuendesha mafunzo hayo, hatua ambayo imeongeza ubora wa mafunzo na kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma kati ya Taasisi hizo mbili.
Vilevile, amewapongeza watumishi wa NAOT kwa ushiriki wao mzuri katika mafunzo hayo, akieleza kuwa ushiriki huo ni ishara ya dhamira ya kuendelea kujifunza na kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza ujuzi wa kitaaluma kwa washiriki na kuimarisha uwezo wao katika kutekeleza majukumu ya Ukaguzi na usimamizi wa fedha za umma kwa ufanisi zaidi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Prof. Siasa Issa Mzenzi akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) alipokuwa anafungua mafunzo ya siku mbili yaliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya APC, Bunju jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Huduma za Utafiti, Viwango na Uhasibu wa NBAA, CPA Angyelile Tende akizungumza kuhusu namna wanavyoshirikiana na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) katika utoaji wa Mafunzo kwa watumishi wao wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Siku mbili yaliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya APC, Bunju jijini Dar es Salaam.
Mkufunzi wa Mafunzo hayo, CPA. Dkt. Neema Kiure Mssusa akiendelea kutoa mada kwa watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT)
Watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Prof. Siasa Issa Mzenzi wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Siku mbili kwa watumishi hao.
Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Prof. Siasa Issa Mzenzi akiwa kwenye picha ya pamoja na Watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT), watoa mada pamoja na baadhi ya watumishi wa NBAA.


No comments:
Post a Comment