Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imeendesha warsha kwa njia ya mtandao sambamba na mafunzo ya ana kwa ana kwa wakufunzi wa vituo vya kufundishia wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya Bodi, ikiwa na lengo la kuwaongezea ujuzi na kuimarisha mbinu za ufundishaji.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Elimu ya Taaluma na Mafunzo wa NBAA, Peter Lyimo, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Prof. Siasa Mzenzi, amesema mafunzo hayo yameandaliwa kwa ajili ya kuwakumbusha wakufunzi majukumu yao pamoja na kuhakikisha wanaendana na mitaala na mahitaji ya Bodi.
Amesema NBAA imeona mafanikio makubwa katika vituo vya kufundishia, ikiwemo kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaofanya mitihani ya Bodi mwaka hadi mwaka.
“Tumeona mafanikio makubwa kwenye vituo vya kufundishia wanafunzi, ambapo idadi ya wanafunzi wanaofanya mitihani ya Bodi imeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka. Mwaka jana wanafunzi waliofanya mitihani walikuwa zaidi ya 8,000 na hivi sasa tunaelekea kufikia 10,000,” amesema Lyimo.
Amesema lengo la NBAA ni kuongeza kiwango cha ufaulu katika mitihani mbalimbali ya Bodi na kuhakikisha wanafunzi wanapata uelewa mpana wa masuala ya Uhasibu na Ukaguzi wa hesabu, ili wanapohitimu wawe wataalamu wenye weledi na uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kufanya jitihada zaidi katika kuboresha huduma zinazotolewa na vituo vya kufundishia, ili wanafunzi waone thamani ya kwenda kusoma katika vituo hivyo na kuwepo kwa utofauti wa kitaaluma kati ya mwanafunzi anayepitia mafunzo katika vituo hivyo na yule anayejisomea bila kupata mafunzo hayo.
Amesema NBAA itaendelea kushirikiana na vituo vya kufundishia pamoja na wakufunzi kuhakikisha wanafunzi wanapata maandalizi bora kuelekea mitihani ya Bodi na hatimaye kujenga wataalamu wenye uwezo wa kuchangia maendeleo ya Taaluma ya Uhasibu na Ukaguzi wa hesabu nchini.
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Elimu ya Taaluma na Mafunzo wa NBAA, Peter Lyimo akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wakufunzi waliofika katika warsha ya ana kwa ana na kwa njia ya mtandao kwa Wakufunzi wa Vituo vya Kufundishia wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya Bodi.
Mkurugenzi wa Huduma za Shirika kutoka NBAA CPA Kulwa Malendeja akizungumza na wakufunzi waliofika katika warsha ya ana kwa ana na kwa njia ya mtandao kwa Wakufunzi wa Vituo vya Kufundishia wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya Bodi.
Mkuu wa Sehemu ya Elimu na Mafunzo NBAA, Sawa Ngendabanka akiwakaribisha wakufunzi wa vituo vya Kufundishia watahiniwa wanaotarajia kufanya mitihani ya Bodi ambao walikuwa wakifuatilia Warsha hiyo na kwa ana na kwa njia ya mtandao.
Mdhibiti Ubora Mwandamizi kutoka NACTVET Dkt. Bonaventure Ackles akitoa mada kuhusu "ufundishaji na uwezeshaji wenye ufanisi kwa wanafunzi" iliyotolewa kwa wakufunzi waliofika katika warsha ya ana kwa ana na kwa njia ya mtandao kwa Wakufunzi wa Vituo vya Kufundishia wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya Bodi.
Mkufunzi CPA Simon Mangesho akitoa mada kuhusu mbinu bora za kufundisha na kufundisha kikamilifu maudhui ya mitaala ya kitaaluma kwa kutumia mfano wa B2 na C1 kwa wakufunzi waliofika katika warsha ya ana kwa ana na kwa njia ya mtandao.
Mkufunzi CPA Rashid Mganwa akitoa elimu kuhusu maboresho ya B4, C4 pamoja na IFRS 18 kwa wakufunzi waliofika katika warsha ya ana kwa ana na kwa njia ya mtandao kwa Wakufunzi wa Vituo vya Kufundishia wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya Bodi.
Baadhi ya Wafanyakazi wa NBAA na Wakufunzi wa Vituo vya Kufundishia Wanafunzi 'Tuition Providers' wanaotarajia kufanya mitihani ya Bodi wakifuatilia mada pamoja na wale wanaofuatilia ana kwa ana na kwa njia ya mtandao kwa Wakufunzi wa Vituo vya Kufundishia wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya Bodi.

Picha ya pamoja ya wafanyakazi wa NBAA na wakufunzi wa vituo vya kufundishia watahiniwa wa Bodi 'Tuition Providers'














No comments:
Post a Comment