HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

NBAA YATOA MAFUNZO KWA NJIA YA MTANDAO



Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (​NBAA) imeendesha warsha kwa njia ya mtandao kwa wanafunzi wanaotegemea kufanya mitihani ya Bodi ili kuongeza ufanisi kipindi wanapokwenda kufanya mitihani hiyo.

Akizungumza wakati wa kufungua warsha hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Pius A. Maneno amesema wamefanya warsha hiyo kwa njia ya mtandao na kuwakutanisha wanafunzi wa ngazi mbalimbali wanaotegemea kufanya mitihani ya Bodi katika ngazi mbalimbali ikiwa na lengo la kuwanoa kwenye mbinu mbalimbali za mitihani hasa kwenye maeneo yanayokuwa na changamoto kwa watahiniwa wa Bodi.

CPA Maneno amesema yapo Masomo yanaleta changamoto na kiwango cha ufaulu unakuwa mdogo hivyo tumewaletea walimu wa Masomo hayo kutoka vyuo na Taasisi mbalimbali ili waweze kuwapa uzoefu na mbinu mbalimbali za kuweza kujiandaa na kufanya mitihani ya Bodi.

"Tumewasisitiza sana namna ya kujiandaa wasijiandae kiholelaholela bali waweke muda wa kutosha kwenye kujifunza kwasababu mitihani ya mwezi Novemba itatumia mtaala mpya " alisema CPA Maneno

Pia amesema lengo kubwa la NBAA ni kuona wanapandisha kiwango cha ufaulu kwa mitihani mbalimbali pamoja na kuongeza kiwango cha uelewa ili kipindi wanapomaliza mitihani yao waweze kuwa wabobezi kwenye masuala ya Uhasibu na Ukaguzi.

Naye Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Elimu na Mafunzo NBAA, Peter Lyimo anasema Bodi hiyo imejipanga vizuri ili kuhakikisha kila mtahiniwa anafanya mitihani vizuri na kuhakikisha wanaondoa changamoto zote zinazowakabili, pia aliwashukuru waliohudhuria mafunzo hayo muhimu .

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Pius A. Maneno akizungumza kwa njia ya mtandao na wanafunzi wanaotegemea kufanya mitihani ya Bodi wakati wa kufungua mafunzo hayo.
Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, CPA Dkt. Emmanuel Christopher akitoa elimu kuhusu namna ya kujiandaa na kufanya masomo ya B1 na C3 kwa wanafunzi wanaotegemea kufanya mitihani ya Bodi waliokuwa wanafuatilia kwa njia mtandao.

Mkufunzi CPA Rashid Mganwa akitoa elimu kuhusu namna ya kujiandaa na kufanya masomo ya B2 na C1 kwa wanafunzi wanaotegemea kufanya mitihani ya Bodi waliokuwa wanafuatilia kwa njia mtandao.
Mkufunzi CPA Ansbert Kishamba akitoa elimu kuhusu namna ya kujiandaa na kufanya somo la B5 kwa wanafunzi wanaotegemea kufanya mitihani ya Bodi.


Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Elimu na Mafunzo NBAA, Peter Lyimo akijibu maswali pamoja na kufunga warsha kwa njia ya mtandaoni kwa wanafunzi wanaotegemea kufanya mitihani ya Bodi.
Baadhi ya Sekretarieti ya Warsha kwa njia ya Mtandao wa NBAA wakiwa kwenye picha ya pamoja na wakufunzi wa warsha kwa njia ya mtandaoni kwa wanafunzi wanaotegemea kufanya mitihani ya Bodi.

WALIOISHIA VETA SASA WANAWEZA KUSOMA ELIMU YA JUU

Mkurugenzi wa Ufundi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Standi nchini,Dk Noel Mbonde akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mtaala Unganishi katika Chuo cha Ufundi Arusha(ATC)jijini Arusha ni Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ufundi(ATC),Dk Erick Mgaya.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Standi nchini,Dk Noel Mbonde akizinduzi wa Mtaala Unganishi unaowawezesha wahitimu wa Veta kuendelea na elimu ya juu ya ufundi,kushoto ni Mshauri wa Ufundi kutoka Canada,Dk Allan Copeland na kulia ni Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ufundi(ATC),Dk Erick Mgaya 
Mkurugenzi wa Ufundi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Standi nchini,Dk Noel Mbonde akionesha Mtaala Unganishi uliozinduliwa katika Chuo cha Ufundi Arusha(ATC) jijini Arusha,kushoto ni Mshauri wa Ufundi kutoka Canada,Dk Allan Copeland na kulia ni Kaimu Mkuu wa Chuo cha ATC,Dk Erick Mgaya


Na Filbert Rweyemamu
Arusha.Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) imethibitisha matumizi ya mtaala unganishi wa masomo ya ufundi nchini utakaowawezesha wahitimu wa vyuo vya Mafunzo ya Ufundi Stadi(Veta) kuendelea na elimu ya juu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mtaala huo,Mkurugenzi wa Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini,Dk Noel Mbonde amesema utasaidia kuwapa fursa vijana wengi waliotamani kuendelea na masomo ya ufundi ya juu kunufaika.

Amesema serikali inathamini maboresho hayo yanayotoa nafasi ya kuwanoa wataalamu wa kutosha inayoenda sambamba na sera ya serikali ya awamu ya tano ya kufikia uchumi wa viwanda.

"Kulikua na tatizo la wanafunzi wetu wanaohitimu Veta kuendelea na kozi za juu za ufundi na sababu kubwa ilikua ni kukosekana kwa sifa za kuwawezesha kujiunga na kozi za ufundi katika ngazi ya Stashahada na kuendelea mtaala unganishi umekua jibu,"alisema Dk Mbonde

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha(ATC),Dk Erick Mgaya amesema mtaala huo ni matokeo ya mahitaji ya wahitimu wengi wa vyuo vya Veta nchini  kuwa na shauku ya kuendelea na masomo ya juu ya ufundi.

Amesema kwa ushirikiano wa wataalamu wa Chuo Kikuu cha Sault nchini Canada walikamilisha mtaala huo unawapa sifa wanaotaka kuendelea na masomo kwa kuhudhuria kozi maalumu kwa muda mwa miezi mitatu.

Naye Mratibu wa NACTE Kanda ya Kaskazini,Godfrey Komba amesema mtaala huo umekuja kwa wakati muafaka ambao serikali inahimiza matumizi ya teknolojia katika kusukuma ajenda ya uchumi wa viwanda nchini.

Aliwataka vijana kuchangamkia fursa hiyo ya kupata elimu unganishi inayowapa nafasi ya kuendelea na elimu ya juu ya ufundi itakayofungua milango zaidi kwa kutoa nafasi ya kupata ajira kwenye makampuni makubwa na kujiajiri wenyewe.

Kwa upande wake Mshauri wa Elimu ya Ufundi kutoka nchini Canada,Dk Allan Copeland  amesema jumla ya wanafunzi 72 wameanza kozi unganishi katika Chuo cha Ufundi Arusha kutoka mikoa mbalimbali ambao ni wahitimu wa vyuo vya Veta.

PROFFESA MSAMBICHAKA ASISITIZA NIDHAMU KWA WANAFUNZI NA WALIMU ILI KUINUA ELIMU WAKATI AKIZINDUA KAMPENI YA 3D


 WALIMU, Wanafunzi na Wafanyakazi katika shule mbalimbali wametakiwa kuzingatia nidhamu shuleni ili kuweza kuchochea maendeleo ya ufaulu kwenye shule zao.Wito ulitolewa jana na Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya John Baptist iliyopo Boko Basihaya jijini Dar es Salaam, Aspiter Kibona wakati wa mahafali ya 10 ya kidato cha nne ya shule hiyo yaliyoenda sambamba na uzinduzi wa kampeni ya '3D' yenye maana ya !Nidhamu, Nidhamu, Nidhamu!.
Kibona alisema wameamua kuzindua kampeni hiyo ikiwa ni kauli mbio yao kwa wanafunzi wa shule hiyo pamoja na walimu na wafanyakazi wengine kuzingatia nidhamu muda wote ambayo itaendelea kuchochea maendeleo ya ufaulu kwa wanafunzi wa shule hiyo.
"Nidhamu si kwa wanafunzi pekee bali inatakiwa kuanzia hata kwangu mimi mkuu wa shule pamoja na walimu na wafanyakazi wengine katika shule yetu hii, hivyo tumezindua kampeni hii ikiwa ni kauli mbio yetu ya kuendelea kuhamasisha nidhamu katika shule yetu kwa nia kuendelea kuchochea maendeleo ya wanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao darasani, " alisema Kibona.
Alisema nidhamu inapoanzia kwa viongozi wa juu, walimu na wafanyakazi wengine inasaidia nidhamu hiyo hiyo kuingia hadi kwa wanafunzi ambayo inawachochea kufanya vizuri katika masomo yao darasani.
Naye Mkurugenzi wa shule hiyo, Jalia Mayanja aliwataka wahimu 53 wa kidato cha nne kuzingatia nidhamu mahali popote watakapokuwa mara baada ya kutoka shuleni hapo kwa faida yao ya huko waendako.
Mayanja alisema nidhamu ndiyo siri ya mafanikio ya shule hiyo katika ufaulu kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Alisema ni vema wahitimu hao wa kidato cha nne wakaendeleza nidhamu waliyokuwa wakiionyesha shuleni hapo huko wanapokwenda ili iweze kuwasaidia katika maisha yao ya baadae.
Aliongeza kwa kuwataka wazazi wanaopeleka watoto wao katika shule hiyo kukaa kwa amani kutokana na kwamba wapo katika mikono salama.

SHULE YA GENIUS KINGS YAJIPANGA KUWA SHULE BORA KITAALUMA TANZANIA

 Wanafunzi wa shule ya Genius Kings Nursery and Primary School iliyopo Tabata jijini Dar es Salaam, wakifundishwa somo la kompyuta.
Wanafunzi wa darasa la tano wakimsikiliza kwa makini mwalimu wa taaluma.
 Wanafunzi wa darasa la sita na la saba katika wa shule ya Genius Kings wakiwa katika chumba cha maabara wakijifunza somo la sayansi kwa vitendo.
Wanafunzi wa darasa la sita na la saba katika wa shule ya Genius Kings wakiwa katika chumba cha maabara wakijifunza somo la sayansi kwa vitendo wakitoa maelezo kwa Mkurugenzi wa Shule hiyo Bw. Machage Kisyeri.
Mkurugenzi wa Shule hiyo Bw. Machage Kisyeri akiwa ofisini kwake.

Shule ya awali na ya msingi ya Genius Kings iliyopo Tabata-Segerea jijini Dar es Salaam imejizatiti kuhakikisha inakuwa shule bora na ya mfano kitaaluma ikiwa ni mwendelezo wa mafanikio ambayo imeyapata katika kipindi cha miaka 10 tangia kuanzishwa kwake.

Akiongea jijini Dar es Salaam kuhusiana na maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwake ambayo yameanza kusherehekewa mapema wiki na kutarajia kumalizika mapema mwezi Desemba mwaka huu,Mkuu wa shule hiyo,Bw.Aloyce Siame,alisema licha ya kwamba mwanzo huwa ni mgumu kwa mradi wowote ule, shule imeweza kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo katika sekta ya elimu na kuweza kuchomoza kuwa miongoni mwa shule zinazofanya vizuri mkoani Dar es Salaam na kwa ngazi ya kitaifa.

Bw.Siame alisema kuwa katika kipindi cha miaka 10 shule imeweza kushikilia rekodi ya kufanya vizuri kwa kufaulisha wanafunzi wa darasa la saba na la nne kwa kiwango cha juu na kuingia katika shule tano bora wilayani Ilala na shule bora 20 mkoani Dar es Salaam mfululizo hali ambayo imewajengea hari ya kuzidi kufanya vizuri kwa mwaka huu na miaka ijayo.

“Moja ya mtazamo wa shule hii ni kuifanya kuwa shule bora ya mfano inayotoa elimu bora nchini kuanzia shule ya awali na shule ya msingi.Tumejipanga kuhakikisha lengo hili linatimia na tunatoa shukrani kwa serikali,wazazi na wadau wote ambao wameonyesha kutuunga mkono katika kipindi hiki cha awamu ya kwanza ya mwanzo ya miaka 10 na kuwezesha mafanikio haya kupatikana”.Alisema.

Aliongeza kuwa mbali na kufundisha masomo ya darasani kwa nadharia na vitendo na ujuzi wa kutumia kompyuta kupata maarifa ya kielimu shule inatoa mafunzo ya kuwajengea wanafunzi uwezo wa kuwa wabunifu,Sanaa,michezo mbalimbali,kuwajengea uwezo wa kujiamini kuongea mbele ya hadhara na kufanya mijadala ya kuchambua masuala yanayohusiana na elimu na nyanja nyinginezo hususani masuala yanayoendelea hapa nchini na nje ya nchi bila kusahau kuibua na kukuza vipaji vya wanafunzi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa shule hiyo,Bw.Machage Kisyeri,alisema anajivunia kwa mafanikio yaliyopatikana ndani ya kipindi cha miaka 10 na kuahidi kuwa uongozi umejipanga kuhakikisha kitaalamu shule inazidi kupanda zaidi na kuimarisha mafunzo ya shule ya awali kwa ajili ya kuwaandaa wanafunzi wadogo kupata elimu bora zaidi kwa kutumia nyenzo mbalimbali za kisasa,kuimarisha miundombinu na kuongeza walimu wenye ujuzi mkubwa wa kufundisha madarasa ya chini ya watoto wadogo kwa kuwa msingi mzuri kielimu ndio unawezesha watoto kuendelea kufanya vizuri katika masomo yao.

Kuhusiana na changamoto wanazokabiliana nazo alisema kuwa zipo changamoto za kawaida kinachotakiwa ni ushirikiano baina ya wazazi,walimu,na wadau wanaosimamia elimu ili kuhakikisha mafanikio yanapatikana na elimu ya Tanzania inazidi kupanda “Walimu wakiwezeshwa vizuri na kupewa ushirikiano wa kutosha naamini shule nyingi za Tanzania zitatoa elimu bora kwa kuwa tunao walimu wengi wazuri ambao wakitumiwa ipasavyo tutasonga mbele”.Alisema.

Akiongea kwa niaba ya wanafunzi wenzake,Mwanafunzi John Magongo anayesoma darasa la saba shuleni hapa alisema kuwa wanawezeshwa kupatiwa elimu ya kuwajengea uwezo wa kufanya vizuri kitaaluma ,nidhamu, kujiamini na kujituma kiasi kwamba popote watakapokwenda wanaamini watazidi kung’ara kutokana na elimu inayotolewa shuleni hapo.

Shule ya Genius Kings ilianzishwa mnamo mwaka 2008 na vijana wa kitanzania wenye taaluma mbalimbali ambapo waliweza kupata walimu wazuri ambao kwa kipindi chote hiki wamewezesha kupatikana mafanikio ya shule kuwanoa wanafunzi vizuri kitaaluma na kuwa miongoni mwa shule bora mkoani Dar es Salaam ,pia uwekezaji wa shule hii umewezesha kupunguza tatizo la ajira kwa kuwa mbali na kuajiri walimu imeajiri wafanyakazi katika vitengo vyake mbalimbali vya uendeshaji.


CHUO CHA UFUNDI ARUSHA CHAZINDUA MTAALA MPYA WA GESI NA MAFUTA

Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Arusha,Hagnery Chitukulo akizungumza wakati wa ufunguzi wa kozi ya ufundi bomba,mafuta na gesi katika chuo cha Ufundi Arusha(ATC) jijini Arusha,kushoto ni Mkuu wa Chuo cha Camosun nchini Canada, Sherri Bell na kulia ni Mkuu wa Chuo cha ATC,Dk Richard Masika.
Afisa wa kitengo cha biashara katika ubalozi wa Canada nchini,Anita Kundy akisoma hotuba yake,kushoto ni Mshauri wa ufundi kutoka nchini Canada,Dk Alan Copeland. 
Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Arusha,Hagnery Chitukulo akionesha nakala ya mtaala mpya wa kozi ya ufundi bomba,mafuta na gesi uliozinduliwa katika chuo cha Ufundi Arusha(ATC).
Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi nchini(TVET)Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia,Mhandisi Thomas Katebalirwe akizungumza jambo katika hafla ya uzinduzi huo. 
Baadhi ya wanafunzi wa mwanzo wa kozi ya ufundi bomba na utaalamu wa gesi na mafuta katika Chuo cha ufundi Arusha 
Mgeni rasmi Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Arusha,Hagnery Chitukulo(wa tatu kushoto)akiwa katika picha ya pamoja na wageni kutoka Chuo cha Camosun,Victoria nchini Canada na Chuo cha ATC. 

Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Arusha,Hagnery Chitukulo amekipongeza Chuo cha Ufundi Arusha(ATC) kwa uamuzi wake wa kushirikiana na Chuo cha Camosun cha nchini Canada kuandaa mtaala wa ufundi bomba,gesi na mafuta katika ngazi ya Diploma.

Akizindua mtaala huo ambao ni kwanza na aina yake nchini alisema utaisadia serikali kuwapata vijana wengi wenye utaalamu wa sekta ya mafuta na gesi nchini katika ngazi hiyo ambayo imenekana kuna pengo kubwa nchini.

"Mafunzo haya yatasaidia sana kuwapata wataalamu wetu na itaipunguzia serikali mzigo wa kuwaajili wataalamu wa kigeni ambao ulipwa fedha nyingi za kigeni,"alisema

Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha,Dk Richard Masika amesema baada ya kutambua mahitaji makubwa ya wataalamu wa fani hiyo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita walikua wakiaanda mtaala kwa ushirikiano na Chuo cha Camosun na mafanikio yamepatikana.

Alisema kozi hiyo ni nyumbufu itakayowawezesha wanafunzi kufanya kazi baada ya kumaliza mwaka wa kwanza na baadaye kuendelea na masomo jambo ambalo litakua likiwapa maarifa kwa vitendo zaidi badala ya nadharia pekee.

Mmoja wa wanafunzi wanaosoma kozi hiyo ambayo imegharamiwa na serikali ya Tanzania,Latifa Mkombo amesema wanaishukuru serikali kwa kutoa ufadhili huo na kuahidi kusoma kwa bidii kwaajili kuingia katika ajira za gesi na mafuta.

Hizi ndizo Sifa 10 zilizotajwa na HESLB kwa wanafunzi wanaoomba mikopo kwa mwaka wa masomo wa 2017/18

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imetangaza mwongozo na vigezo vya utoaji mikopo na ruzuku kwa mwaka wa masomo 2017/2018 na imeanza kupokea maombi ya mikopo kuanzia tarehe 6 Agosti 2017 hadi tarehe 4 Septemba, 2017.
Waombaji wote wa mikopo watarajiwa wanasisitizwa kusoma mwongozo wa utoaji mikopo na ruzuku kwa mwaka wa masomo 2017/2018 pamoja na taratibu nyingine za uombaji mkopo kabla ya kujaza fomu za maombi ya mkopo zinazopatikana kwenye mtandao wa https://www.heslb.go.tz/

Aliyeipaisha Tusiime kitaifa atamani PhD

Mwanafunzi bora nafasi ya tatu kitaifa katika masomo ya biashara wa shule ya Tusiime, Rashid  Abdalah aliyevaa flana, akifurahia na kupongezwa na wanafunzi wa kidato cha tano wa shule hiyo alipokwenda kuwatembelea na kuwadokeza siri ya magfanikio yake.


MWANAFUNZI wa shule ya Sekondari ya Tusiime, Rashid Abdalah, aliyeshika nafasi ya tatu kitaifa kwa masomo ya biashara amesema nia yake ni kusoma hadi ngazi ya Shahada ya Uzamivu (PhD).

Akizungumza leo shuleni hapo Rashid amesema ndoto yake ya miaka mingi ni kuwa mkaguzi wa hesabu hivyo amenuia kusoma kwa bidii hadi afikie ngazi hiyo.

“Naamini nitafikia malengo yangu kwa kuwa najua siri ya kufika huko ni juhudi, kujitambua  na kuwasikiliza walimu, hakuna kingine zaidi ya kuwa makini na masomo na kuwa makini,” alisema Rashid ambaye alianzia kidato cha pili shuleni hapo mwaka 2012.

Amesema juhudi za walimu katika kufuatilia maendeleo ya wanafunzi na mazingira mazuri ya shule, ushirikiano mzuri na wanafunzi wenzake ni baadhi ya mambo ambayo yamekuwa chachu ya mafanikio yake.

Aidha amewaasa wanafunzi waliobaki shuleni hapo kujitambua wamefuata nini shuleni na kufuatilia kila wanachofundishwa na walimu wao ili mwisho wa siku wapate mafanikio kama yake.

“Kufaulu haiwezi kuwa muujiza ni juhudi tu na kusikiliza mafundisho na maelekezo ya walimu, lazima mtambue kuwa walimu wanataka mfaulu hivyo mkiwasikiliza na kuwafuata mtafaulu kwa viwango vya juu sana,” amesema Rashid alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa kidato cha tano shuleni hapo.

Mkuu wa shule hiyo, Emil Rugambwa, amesema mafanikio ya shule hiyo kwenye matokeo ya kidato cha sita ni mwendelezo wa mafanikio kwenye matokeo ya kitaifa ambayo shule imekuwa ikiyapata kuanzia yale ya darasa la nne, darasa la saba, kidato cha pili na cha nne.

Kwenye matokeo ya kidato cha sita mwaka huu, Tusiime imefanikiwa kufanya vizuri kwenye matokeo ya kidato cha sita yaliyotangazwa na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) hivi karibuni kwa kufaulisha wanafunzi wote 518.

TCU Yawatoa Hofu Wanafunzi Wanaotarajia Kujiunga Vyuoni Mwaka Huu

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imesema kuwa haitegemei kufutiwa udahili kwa wanafunzi kwa baadhi ya vyuo, kutawakosesha baadhi ya wanafunzi watarajiwa nafasi au kozi walizodhamiria kwenda kuzisoma.

Akizungumza kwenye Viwanja vya Maonesho, Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari Mwandamizi, Edward Mkaku alisema TCU haitahusika na wanafunzi ambao watakosa vyuo kwa sababu kwa sasa wameratibu udahili na hivyo ni jukumu la mwanafunzi kutafuta chuo kulingana na ufaulu alionao.

“Hatutarajii mwanafunzi kukosa chuo, na pia kufutiwa udahili kwa baadhi ya vyuo siyo sababu ya wanafunzi kukosa nafasi kwenye vile vyuo vilivyopo,” alisema.

TCU: Udahili Vyuo Vikuu Kuanza Julai 22


Na: Lilian Lundo - MAELEZO.
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania ( TCU) umeutangazia Umma kuwa kuanzia Julai 22 mwaka huu vyuo vyote vya elimu ya juu hapa nchini vitaanza kupokea maombi ya udahili kwa mwaka wa masomo  2017/2018.

Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume hiyo Prof. Eleuther Mwageni ameyasema hayo leo, Jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongea na waandishi wa habari juu ya kuanza rasmi udahili kwa mwaka 2017/2018.

Prof. Mwageni amesema kuwa waombaji wanatakiwa kutuma maombi yao  kwenye vyuo husika na siyo tena TCU kama ilivyokuwa kwa mwaka jana na miaka mingine ya nyuma.

Aidha amesema kuwa waombaji wahakikishe wanaomba programu za masomo ambazo zimeidhinishwa na kutambuliwa na TCU na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).

"Tunavikumbusha vyuo kutangaza programu ambazo zimeidhinishwa na kutambuliwa na TCU na NACTE, ikiwa chuo kitatangaza programu ambazo  hazitambuliki na Tume, basi chuo husika kitachukuliwa hatua," amesema Prof. Mwageni.

Ameendelea kwa kusema kuwa, orodha ya programu hizo inapatikana katika tovuti ya TCU (www.tcu.go.tz) ambapo programu hizo zimegawanywa katika makundi mawili yaani Kidato cha Sita na Diploma.

Vile vile, Prof. Mwageni amewataka waombaji watakao chaguliwa kwa zaidi ya chuo kimoja, kuthibitisha kwa wakati chuo watakachokwenda ili kutoa nafasi kwa waombaji wengine.

Waombaji wamehimizwa kusoma kwa makini mwongozo wa udahili kwa mwaka 2017/18 ambao unapatikana kwenye tovuti ya Tume.  

Aidha Tume inawakaribisha wadau wote kushiriki maonesho ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yatakayofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja, Jijini Dar es Salaam kuanzia Jula 26 hadi 29 mwaka huu ambapo zaidi ya vyuo 80 vinatarajiwa kuwepo katika maonesho hayo.

VIDEO:SHULE YA SEKONDARI LONDONI YASHIKA NAFASI YA KWANZA KATIKA MATOKEO YA KIDATO CHA SITA KWA MANISPAA YA SONGEA

Shule ya sekondari LONDONI iliyopo katika manispaa ya SONGEA mkoani RUVUMA, ni kati ya shule zilizofanya vizuri katika matokeo ya kidato cha sita mwaka 2017 ambapo kwa mwaka 2017 imeshika nafasi ya kwanza katika manispaa ya SONGEA huku kimkoa imeshika nafasi ya nne.HABRI KAMILI HII HAPA VIDEO YAKE.

ELIMU SAHIHI ITUMIKE KWANZA KABLA YA MATUMIZI YA SHERIA KWA WAKEKETAJI.

 Mzee maarufu na mwenyeji wa Msange Bi Greta Musa Nyonyi akichangia hoja katika semina ya kupinga Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani Singida.
 Mratibu wa Mradi wa Kupinga Ukeketaji (WOWAP) Nasra Suleiman akizungumza na washiriki wa semina ya kupinga Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani Singida.
 Afisa Maendeleo ya Jamii kata ya Msange Magni Oisso akichangia hoja katika semina ya kupinga Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani Singida.
 Washiriki wa semina ya kupinga ukeketaji iliyoandaliwa na Mradi wa WOWAP wakifuatilia kwa umakini filamu fupi ya Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani Singida.
Mzee wa Kimila Hosea Mnyambi akichangia hoja katika semina ya kupinga Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani Singida.


Elimu sahihi juu ya madhara ya ukeketaji ya muda mfupi na mrefu inatakiwa itolewe kwa jamii kabla ya kuwachukulia hatua baadhi yao wanaoendelea kufanya vitendo vya ukeketaji licha ya uwepo wa sheria kali.

Rai hiyo imetolewa mapema leo na Mratibu wa Mradi wa Kupinga Ukeketaji (WOWAP) Nasra Suleiman katika semina ya kupinga Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani Singida, kwa ushirikiano wa Ofisi ya Ustawi wa Jamii Mkoa wa Singida na mradi huo kwa ufadhili wa shirika la WAAF-Japan.

Mratibu huyo amesema nguvu ya sheria itasaidia kuondoa ukeketaji endapo wananchi wengi watakuwa na uelewa wa kutosha juu ya madhara ya ukeketaji na kuamua kwa hiyari kuachana na mila hiyo.

“Sheria isiwe nguvu pekee ya kupambana na ukeketaji, tukifanya hivyo itafikia kipindi tutakwama kwa kiasi kikubwa kwa kuwa watu wataendelea kukeketa kwa kificho ili wasikamatwe, lakini kila mwana jamii akiwa na elimu ya kutosha ya madhara hayo, nguvu ya sheria itatumika tu kwa wachache watao kaidi”, amesisitiza Nasra.

Ameongeza kuwa Watendaji wa kata na vijiji wana uwezo mkubwa wa kubadilisha mtazamo na mila ya ukeketaji kwa kuelimisha wananchi wao hasa baada ya semina zinazoandaliwa na miradi au mashirika Fulani kwakuwa zinawajengea uwezo ili waweze kutoa elimu sahihi na mbinu za kuelimisha.

Nasra amesisitiza kuwa jukumu la elimu lisiachwe kwa sekta binafsi kama mradi wake wa WOWAP pekee bali liwe jukumu la jamii nzima huku akifafanua kuwa elimu inayotakiwa kutolewa ni ile inayoelezea madhara ya ukeketaji na sio kuwakataza kwa kigezo cha kutii sheria pekee.

Naye Afisa Maendeleo ya Jamii kata ya Msange Magni Oisso amesema katika kata hiyo ukeketaji umekufanyika kwa siri sana kwa kuogopa mkono wa sheria huku wahanga wakiwa watoto wachanga na wale waliomaliza kliniki.

Oisso amesema kumekuwa na usiri mkubwa huku wakeketaji wakibadili mbinu namna za kujificha wasigundulike kwa jamii ambayo elimu imeanza kuwafikia baadhi yao.

Aidha amependekeza kuwa ili kukomesha ukeketaji moja ya njia ni kutoa elimu katika vituo vya kutolea huduma za uzazi na mtoto ili mtoto aweze kunusurika pia elimu itolewe shuleni kwa ngazi zote kuanzia darasa la awali hadi la saba.

Akichangia mada katika semina hiyo mzee maarufu na mwenyeji wa Msange Bi Greta Musa Nyonyi amesema elimu ni bora zaidi kuliko kuwaogopesha wanajamii kwa kutumia sheria kwakuwa watatafuta namna ya kutekeleza azma yao kwa usiri ili kukwepa mkono wa sheria na sio kuacha.

Greta ameongeza kuwa kwa sasa kutokana na kuwa wakeketaji wamebainika kuwa wanakeketa watoto wachanga na hugundulika wakienda kliniki baadhi yao wanabadili mbinu na kusubiri mtoto amalize kliniki ndipo anakeketwa.

Naye Mzee wa Kimila Hosea Mnyambi amesema yeye amekulia katika familia ya wakeketaji na wamekuwa wakirithishwa mbinu za ukeketaji kizazi hadi kizazi ila kutokana na kuwepo kwa sheria, dini kuhubiri madhara ya ukeketaji, mila hiyo wameiacha.

Amesema wachache wanaoendelea kufanya vitendo hivy o ha wanawake wamekuwa wakifanya kwa usiri mkubwa huku akina baba wakiwa hawana taarifa ya kinachoendelea na endapo mtoto anafariki hudanganywa ugonjwa uliopelekea kifo cha mtoto.

Mzee Mnyambi amesema elimu iendelee kutolewa hasa kwa kutumia vyombo vinavyoaminika mfano vyama vya siasa, dini na vikundi vya kuweka na kukopa pamoja na kuiweka agenda ya ukeketaji kwa vikao vya Kata na vijiji.

Semina ya kupinga ukeketaji Kata ya Msange imefanywa na mradi wa WOWAP kwa ushirikiano wa maafisa ustawi wa jamii mkoa wa Singia kwa watendaji wa kata na vijiji, watoa huduma za afya, polisi, waalimu, wawakilishi wa viongozi wa dini, maafisa ustawi wa jamii na maendeleo ya jamii, wazee maarufu na wa kimila ili wawe mabalozi wa kusambaza elimu hiyo kwa jamii inayo wazunguka.

ZITAMBUE TABIA ZA WANAWAKE WAPENDA PESA

1. Huwa na tamaa ya mambo yasiyo ya lazima.
Wanawake wengi wapendao pesa huwa na tamaa ya mambo yasiyo ya lazima, mambo ambayo hayagusi maisha moja kwa moja. Hata nilipokuwa chuo wanawake wengi waliokuwa wanapenda pesa Sana walikuwa na tamaa za kusikitisha ambazo zilipofusha fahamu zao.
Unakuta mwanamke anaomba laki tano kwaajili tuu ya kununua Simu nyingine kubwa wakati akiwa bado na simu mpya.
Katika maisha ni bora uingie jehanam kuliko kukutana na mwanamke mpenda pesa kwani utateseka Sana kwa ajili yake na bado hata ona msaada wako.
Sio rahisi kujenga familia bora na mwanamke mpenda pesa.

2. Wengi hutoka familia masikini.
Wanawake wengi Kama sio wote ambao hupenda pesa kuliko utu wao hutoka familia kame Sana. Ukame wa kiuchumi mpaka kiakili. Wengi wao huweza kutoa hata rushwa ya ngono ili tuu wapate pesa wasijue miili yao inathamani zaidi ya zile karatasi.
Mtu ni masikini unandoto za kuwa na mwanaume mwenye pesa nani alikuambia wenye pesa wanataka masikini.
Umasikini wako usikufanye ujidharau au mtu akudharau. Lipo kundi dogo la wanawake wanaojitahidi kutetea thamani ya jinsia yao lakini wengi wao ni wakuonewa huruma tuu.

3. Wengi wao hawana elimu ya kutosha.
Mwanamke aliesoma akaelimika hawezi hangaika na pesa ya mtu. Ndio maana wanawake wachache huhangaika kwajili ya kujitegemea na sio kumtegemea mwanaume.
Wanawake wengi wenye elimu na vipato vizuri huwezi msikie akiongelea pesa Kama kigezo muhimu kwa mwanaume anayemuhitaji awe mume wake.

WANAFUNZI WA SHULE YA SEKONDARI YA NYANGAO WATEMBELEA BUNGE NA KUKUTANA NA MAJALIWA

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyangao iliyopo Jimbo la Mtama mkoani Lindi kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma Julai 4, 2017. Kushoto kwake ni Mbunge wa Kuteuliwa, Mama Salma Kikwete na wapili kushoto kwake ni Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 
  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye  wakisalimiana na wananfunzi wa Shule ya Sekondari ya Nyangao mkoani Lindi kwenye viwanja vya Bunge jini Dodoma Julai 4, 2017.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Nyangao iliyopo katika Jimbo la Mtama Mkoani Lindi kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma Julai 4, 2017. Wapili kushoto kwake ni Mbunge wa Kuteuliwa, Mama Salma Kikwete na kulia ni Mbunge wa Mtama Nape Nnauye.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Nyangao iliyopo katika Jimbo la Mtama Mkoani Lindi kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma Julai 4, 2017. Wapili kushoto kwake ni Mbunge wa Mtama Nape Nnauye.

Fahamu Biashara tano unazoweza kuzifanya ukiwa mkoa wa Dar es Salaam

Dar es Salaam kuna changamoto nyingi endapo hauna shughuli maalumu ya kufanya basi lazima utauchukia mji huu na kuona sio sehemu sawa kwa wewe kuwepo, ila ukifanikiwa kujua cha kufanya ukiwa hapa basi lazima utaona Mkoa huu ni mrahisi sana.



Zifatazo ni biashara za kufanya ukiwa hapa.

Biashara ya kwanza :-Kuuza vinywaji baridi



Jiji la Dar es Salaam limekuwa na asili ya kuwa na joto sana hivyo ni rahisi kwako wewe kuifanya biashara ya vinywaji baridi kama soda, maji na juisi hasa maeneo yenye pilika piliaka za watu na uhitaji wa vitu hivyo mara zote. Mfano unaweza kuuza katika eneo la soko, maeneo ya vituo vya basi pamoja na wakati wa foleni barabarani.

Biashara ya Pili : -Kuuza magazeti

Mara nyingi kumekuwa na uhitaji wa watu wa kupata habari, sio wote wenye simu wanajua njia za kupata habari na sio wote wanakuwa na uwezo wa kununua bando ilikuweza kuperuzi mitandao kujua kinachoendelea, hivyo bado kuna uhitaji wa magazeti ukizingatia wengi wanakuwa busy na shughuli zao.



Kupita kusoma gazeti ndiyo huwa muda pekee wao kujua mambo yananayoendelea na husoma magazeti hasa kwenye foleni za magari asubuhi wanapokwenda na jioni wanaporudi kwenye shughuli zao.

Biashara ya tatu ;- Uuzaji wa matunda


Kiafya ni moja ya hitaji kubwa sana katika mwili wa binadamu, hivyo biashara hiyo ni nzuri kuifanya ukiwa hapa na biashara hii ubadilika badilika kulingana na msimu wa tunda husika. Mtaji wa biashara hii ni mdogo na sehemu nzuri za kupatia wateja ni kwenye vituo vya mabasi, pembezoni mwa barabara, karibu na migahawa au karibu na ofisi.

Biashara ya nne ;- Uuzaji wa vocha ama muda wa maongezi

Japo imelalamikiwa kutokuwa na faida ila mkaa bure sio sawa na mtembea bure, Wakazi wengi wa jiji hili hutumia vocha kurahisha shughuli zao kwa kuwasilana na ndugu, jamaa ana rafiki. Hii hupelekea wanaouza vocha za muda wa maongezi kuwa na uhakika na biashara zao.

Biashara ya tano :- Uuzaji wa chakula.



Hapa ndiyo patamu sasa, kila mtu napenda kula, Biashara ya kuuza chakula ni nzuri kwani binadamu yoyote anahitjika kupata chakula.Lakini sio chakula tu hata vyakula vya baharini, kama pweza ni moja ya vitu vinavyoweza kukufanya ukaendela kuwepo hapa mjini.Pia biashara ya chakula aina ya chips ni nzuri pia kwani inawateja wengi.

MUHIMU:

Unatakiwa ujue kuwa kila biashra inachangamoto zake hivyo cha msingi ni kukabiriana nazo iliuweze kufika malengo yako.

Na Laila Sued